25.1 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

GONGO YAUA WATU 19 DAR

Na ASHA BANI

POMBE aina ya gongo inayotengenezwa kienyeji, imesababisha vifo vya watu 19 na kuacha wengine wakiwa vipofu baada ya kuinywa jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Stop Over, Kimara, katika Wilaya ya Ubungo,  ikiwa ni miaka 18 tangu 1999 ambapo watu 15 kwenye eneo hilo hilo walifariki baada ya kunywa pombe hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Godfrey Misana, alisema watu hao walifariki juzi usiku mara tu baada ya kunywa pombe hiyo inayodhaniwa kuwa na kemikali zenye sumu.

Alisema kati ya watu hao waliofariki ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, tisa kati yao wanatoka kwenye mtaa wake.

Alisema kati ya watu hao tisa, sita walifariki baada ya kufikishwa hospitali na wengine watatu walifariki dunia wakiwa kwenye eneo walilonywea pombe hiyo.

Misana  alisema waliofariki dunia kwenye mtaa wake ni Balewa Ramadhani, Fred Kiyondo, Stive ambaye jina lake maarufu ni  ‘Mzee wa Chuo’, Stanslaus Mayaya, Mtalebani,  Alex ambaye anajulikana zaidi kama Rasta na mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Mama Rama. Wengine ni walinzi wawili wa jamii ya Kimasai ambao majina yao hayakufahamika.

“Hapa kuna tetesi kwamba waliofariki ni 19, wengine wametokea katika maeneo ya mbali, lakini katika mtaa  wangu majina niliyonayo ni hayo, tunaendelea kutafuta wengine endapo watatokea,” alisema Misana.

Gazeti hili lilipofika kwenye eneo hilo la tukio, lilielezwa kuwa, baadhi ya waathirika wa pombe hiyo na miili ya waliofariki, imepelekwa hospitali mbalimbali, ikiwamo Tumbi, iliyopo Kibaha, Pwani, Kimara, Mwananyama na Muhimbili.

Muhimbili wapokea miili mitano

Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), John Stephen, alithibitisha kupokea miili mitano.

“Majira ya saa 9 alasiri tulipokea miili ya watu watano kutoka Hospitali ya Rufaa Mwananyamala ambapo kati ya hao, wanne ni wanaume na mmoja ni mwanamke,” alisema Stephen.

Polisi

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini hakutaka kulifafanua, kwa kile alichosema atazungumza leo.

“Hizo taarifa kwa sasa sijaletewa,” alisema Mambosasa na mwandishi alipomwambia kuwa polisi Kinondoni imemweleza kuwa taarifa zimepelekwa Kanda Maalumu, alisema: “Nitazungumza kesho kwa sababu taarifa nilizo nazo mimi ni kama ulizo nazo wewe za tukio kutokea.”

Hali ilivyo kwenye eneo la tukio

Katika eneo ambalo lilitumika kwa watu kunywa pombe hiyo, kwa sasa limejengwa mabanda ya kuishi kwa muda baada ya nyumba za wakazi hao kubomolewa na Wakala wa Barabara (Tanroads) ili kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro.

Mtoto wa marehemu Stanslaus Mayaya, Paulina Mayaya, alisema alimuona baba yake ambaye ni fundi cherehani akiwa anatapatapa baada ya kutoka kunywa pombe hiyo.

Alisema baada ya kumuona baba yake akiwa kwenye hali hiyo, aliomba msaada kwa majirani wakamlaza kwenye godoro.

Alisema baba yake akiwa na wenzake watatu, baada ya kuwa kwenye hali hiyo, waliwanunulia maziwa wakanywa, lakini ghafla walianza kutoka povu mdomoni, kuhara na kutapika, baadaye wakakata kauli.

Alisema baadaye lilikuja gari la polisi likawapeleka Hospitali ya Kimara huku wakiwa wameshafariki dunia.

“Baba yangu ndiye ambaye tulikuwa tukimtegemea, alikuwa fundi cherehani, alikuwa akishona nguo na tunapata fedha ya chakula, baada ya kubomolewa nyumba alianza kubadilika tabia na nikimuona akiwa anarudi nyumbani amelewa,” alisema Paulina.

MAJIRANI

Emanuel George, ambaye ni jirani, alisema walishangaa kuwaona wenzao wakiwa wanatoa udenda huku wakiwa wamefunga macho ghafla.

“Yaani baada ya kupatwa na tatizo kilichofanyika ni kuwanunulia maziwa na kuwapa, lakini kila wakiwa wanakunywa ndio walikuwa wakiharisha mfululizo, wakitapika, wakitokwa na mapovu na macho kuyafunga.

“Tulihisi watapona kwa kuwa walikuwa wakitapika, lakini haikuwa hivyo, wapo waliofia hapa na wengine waliofia Kimara Hospitali, wengine katika Hospitali ya Mwananyamala,” alisema George.

Akizungumzia kuchukua miili ya marehemu, alisema: “Tangu asubuhi tunahangaika lakini miili wamesema hawawezi kutupa wala hawawezi kuichoma sindano, hadi uchunguzi ufanyike, hivyo wametuambia twende asubuhi Muhimbili tukiwa na askari mmoja wa Kimara,” alisema George.

HISTORIA

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Amina, alisema anakumbuka tukio kama hilo liliwahi kutokea mwaka 1999 na watu 15 kufariki.

“Lilitokea mwaka 1999 na liliua watu pia, kwa sasa limejirudia tena, nafikiri serikali sasa na baadhi ya viongozi wataanza msako wa kukagua vibanda vinavyouza gongo.

 

Mpishi afariki

Baadhi ya majirani walisema, marehemu aliyefahamika kwa jina la mama Rama, ni mmoja wa wapishi wa pombe hiyo ambaye alifariki baada ya kuionja.

“Alionja vifuniko viwili tu, vifuniko vyenyewe ni hivi vya chupa ya maji madogo ya kunywa.”

Inavyotengenezwa

Jirani mwingine akiwa ameshika chupa ya maji ya lita moja na nusu, alisema huwekwa humo mchanganyiko wa spiriti kama ya kuweka kwenye vidonda na dawa ya kuondoa madoa ya Jik, kisha kudumbukizwa ndani sarafu za senti tano na senti 10 zenye tobo katikati.

“Mchanganyiko huu unaweza kutoa pipa moja moja la pombe, siku hizi hawapiki kama zamani ilivyokuwa wakipika na mitambo unasikia inakamatwa huko, hizo sarafu wanasema wanaziweka ili kuongeza ukali,” alisema.

“Mengine ulizeni kwa Mganga Mkuu, nimeshakwambia mama Rama ndio anatengeneza hiyo pombe na mwenyewe ameonja vifuniko viwili tu amefariki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles