31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Ewura tafsiri sahihi kuelekea uchumi wa viwanda

Na Shermarx Ngahemera


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ndiyo taasisi ya umma inayoshughulikia kwa karibu upatikanaji nishati na maji safi kwa wananchi wa Tanzania majukumu ambayo inayafanya kwa uadilifu mkubwa na weledi usiotia shaka hasa ukizingatia ukubwa wa majukumu yenyewe na usimamizi wa mashirika zaidi ya mia chini yake nchi nzima.

Ukitazama kwa juu juu utafikiri Ewura ni  shirika dogo, lakini ukifanya tathmini ya kina utaona kuwa maendeleo au starehe ya maendeleo ya Watanzania yanategemea kwa kiasi kikubwa namna shirika hilo linavyofanya kazi zake kwa sekta hizo muhimu kwa maisha ya kila siku. Kwani ufanisi wa Ewura upo ofisini kwako, nyumbani na barabarani kwa maana ya umeme, maji, petroli kwa magari na nishati ya kuendesha mashine na mitambo ya viwanda na viyoyozi.

Udhibiti wa bidhaa

Ewura inaendelea na jukumu la kusimamia na kudhibiti ubora wa bidhaa za mafuta aina ya petroli yanayouzwa nchini kwa kutoa leseni na kusimamia bei ya mafuta ili kutoa  urari kwa wote na kufanya maisha yawe mazuri kwa wote.

Ewura hivi karibuni kupitia ofisi yake ya uhusiano inakemea biashara holela ya mafuta inayojitokeza nchini kwani kimsingi ni kosa kisheria kuuza au kusambaza mafuta bila kuwa na leseni toka Ewura.

Hii inafanyika ili kulinda ubora wa bidhaa ya mafuta kwani bila udhibiti huleta fujo na ukosefu wa uwajibikaji kwa umma na kuharibu malengo yaliyokusudiwa ya shirika hili.

Adhabu kali huchukuliwa kwa mfanyabiashara yeyote anayekutwa anauza mafuta kiholela. Aidha, Ewura inawataka watumiaji wa mafuta kuacha mara moja kutumia mafuta yanayouzwa kiholela kunusuru ubora wa injini za magari yao na kuhakikisha kodi ya Serikali inapatikana kwa kununua mafuta kwenye utaratibu ulioratibiwa nayo (Ewura).

Uongozi wa Ewura unauelezea uuzaji holela wa mafuta ni kule kutozingatia matakwa ya sheria na kanuni zinazosimamia  biashara  hiyo nchini kwani kisheria biashara hiyo inaratibiwa  nayo.

Ewura inashangaa kuona  hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la uuzaji wa mafuta kiholela katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwa ni katika maeneo ya mijini na vijijini.

Uuzaji huo unahusisha; uuzaji wa mafuta kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwa kisheria; uuzaji wa mafuta kwa kutumia vyombo vya kuhifadhia mafuta ambavyo havijaruhusiwa kisheria kama vile chupa (za kioo na plastiki), madumu, matanki makubwa ya plastiki na uuzaji wa mafuta kutoka kwenye magari  yanayotembea huku na kule (mobile trucks).

Mamlaka imetoa hadhari juu ya athari zitokanazo na uuzaji wa mafuta kiholela ambazo ni nyingi ikiwamo kuhatarisha usalama wa wananchi na mali zao kutokana na ajali za moto zinazoweza kutokea. Husababisha uchafuzi wa mazingira na huathiri ushindani kibiashara kwa kuwanyima fursa wafanyabiashara halali wenye vituo vya mafuta na hivyo kuleta ushindani usio sawa kwa kuvuruga utambarare wa soko husika.

Isitoshe biashara  holela inayohusishwa kwa karibu na magendo, huinyima Serikali na taasisi zake mapato halali yanayostahili kulipwa na wafanyabiashara hao na vile vile kwa kutaka kujinufaisha vilivyo huwafanya walaji kununua mafuta kwa ujazo usio sahihi na hivyo ni dhuluma kwao.

Ewura imeendelea kuainisha athari za kuwanyima walaji uhakika wa ubora wa mafuta ambapo mojawapo ya athari za kutumia mafuta yasiyokidhi viwango ni kuharibu ufanyaji kazi wa injini za magari au mitambo.

Biashara hiyo kutoka vyanzo haramu kama vile magendo na wizi ni batili.

Viwango mafuta

Ewura inasimamia viwango vya ubora wa mafuta ya taa, dizeli na petroli kama ilivyoainishwa na  kutolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuzuia mafuta yasiyokidhi viwango stahiki  ambayo huleta athari kiafya, uchafuzi wa mazingira na husababisha ushindani usio sawa. Pamoja na hayo, mafuta yasiyokidhi viwango huathiri utendaji kazi wa injini za magari na mitambo.

Biashara ya mafuta

Kwa sasa, Tanzania haina kiwanda cha kusafisha mafuta. Hivyo basi, nishati hiyo  huagizwa kutoka nje ya nchi kupitia kampuni  halali zilizopewa leseni ya uagizaji wa mafuta kwa jumla na Ewura nazo ndizo huruhusiwa kuagiza mafuta kupitia Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) yaani Petroleum Bulk Procurement Agency.

Ewura inasema kama zilivyo nishati nyingine, ni muhimu kuzingatia misingi ya usalama ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea wakati wa upokeaji, uhifadhi, usafirishaji na utumiaji wa bidhaa za mafuta ya petroli.

Kanuni za biashara mafuta

Kanuni ndio msingi wa uendeshaji  kazi za mamlaka na hivyo zimewekwa  kwa kila shughuli zake za uendeshaji kwa zinazosimamia uendeshaji wa biashara ya mafuta nchini kam ifuatavyo:

Kanuni za mwaka 2014 zinalenga  madhumuni makuu ya kuhakikisha kuwa waagizaji wa jumla (Petroleum Wholesalers) wanakuwa na leseni za Ewura.

Kuhakikisha kuwa waagizaji wa jumla wanawauzia mafuta wafanyabiashara wenye vituo vya mafuta na watumiaji binafsi (consumer installations), wenye leseni.

Kuhakikisha kuwa usalama na afya za watu pamoja na mali zao vinazingatiwa na kwamba hakuna athari za kimazingira zinazoweza kutokea wakati wa uendeshaji wa biashara hii.

Kuhakikisha kuwa mafuta yanapatikana kwa walaji wakati wote, katika ubora uliothibitishwa na Shirika la Viwango la Taifa (TBS) na kwa bei halali.

Kutokana na utendaji mzuri wa Ewura, nchi ina uhakika wa mafuta na usalama wake kwa watu na mali zao ni wa uhakika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles