Na RAPHAEL OKELLO
MKUU wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, ameliagiza jeshi la polisi kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wazazi na walezi ambao watoto wao wanajihusisha na ajira migodini.
Alisema lengo ni kukomesha uvunjaji wa haki za watoto.
Akizungumza na wachimbaji wa Kijiji cha Kamkenga jana, Bupilipili alisema agizo hilo linahusisha wamiliki wa migodi ambao wamekuwa na tabia ya kuwaajiri watoto na kuwatumikisha biashara au kufanya kazi mbalimbali za ndani badala ya kuwapeleka shule.
“OCD nakuagiza kuanza sasa mtoto yeyote atakayepatikana mgodini akifanya kazi mkamate ili amtaje mzazi wake naye akamatwe.
“Lakini aliyempa ajira hiyo naye hakikisheni anakamatwa kwa sababu wanawachochea watoto kuacha shule na kujiingiza katika biashara hizi,” alisema Bupilipili.
Alisema mtoto anapaswa kusoma shule na siyo ajira, hivyo haiwezekani wazazi kuwatumikisha watoto ili wapate riziki kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha.
DC alisema watoto hata wakiwa kwenye ajira hawana uwezo kujadiliana na mwajiri kupata malipo stahiki lakini pia ni kinyume na sheria.
Bupilipili pia alitangaza kufunguliwa mgodi wa Kamkenga ambao ulifungwa kwa takribani wiki moja kupisha ukaguzi wa usalama wa mgodi.
Alisema shughuli za uchimbaji ziliruhusiwa katika maduara 22 yaliyothibitishwa kuwa salama na mengine 44 yakiagizwa kufanya marekebisho kadhaa kabla ya serikali kuruhusu shughuli hizo kuendelea.