Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetangaza kuwa ina wajibu wa kuikopesha serikali mkopo wa muda mfupi usio wa kibajeti wa asilimia 18 na kwamba serikali imekuwa ikilipa madeni hayo kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 22,2024, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BOT, Agathon Kipandula, alieleza kuwa mkopo huo hutolewa kwa mujibu wa sheria sura ya 197 ya mwaka 2006. Sheria hii inaruhusu benki hiyo kutunza fedha za serikali zote mbili na mashirika ya umma, na kuwapatia mikopo wanapokuwa na uhitaji.
“Sheria hii pia imeweka ukomo wa kukopa ambao ni asilimia 18 ya mapato ya mwaka uliopita,” alifafanua Kipandula. Aliongeza kuwa utaratibu huu unafuatwa na benki kuu zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na duniani, kwani wote wanatumia sheria moja.
Kipandula alibainisha kuwa kwa kuwa na mteja ambaye ni serikali, sheria hiyo imetoa nafasi ya kutoa mkopo wa muda mfupi kwa lengo la kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya serikali.
“Kwa mambo yanayoendelea, sheria inatusimamia katika kuendesha shughuli za serikali, ikiwemo kutoa huduma ya mkopo wa muda mfupi kuziba pengo au nakisi,” aliongeza Kipandula.
Amesema kuwa mkopo huo unahitaji kurejeshwa ndani ya siku 180 na kwamba kila mwisho wa mwezi serikali inarejesha mkopo huo. “Mkopo huu sio ule ambao tunadhibiti kiasi, bali unarekebisha mtiririko wa fedha. Kama serikali inahitaji kulipa Sh 10,000 na ina Sh 5,000, basi Sh 10,000 itatolewa kama overdraft na serikali itarejesha fedha hizo inapo zipata,” alieleza Kipandula.
Pia, Kipandula alisisitiza kuwa si kweli kwamba serikali ilikopeshwa kiasi cha fedha na BOT kwa aina tofauti, na kwamba hata kwenye vitabu vya serikali hakuna kiasi hicho kilichorekodiwa. Aliongeza kuwa mkopo wa aina hiyo hauhitaji kupitishwa na Bunge isipokuwa utaonyeshwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Kwa sasa tunaeleza ili kuongeza uelewa wa masuala yanayoendelea BOT, baada ya taarifa kutolewa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Fedha kutoa ufafanuzi,” alimalizia Kipandula.