25.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

BoT kutoa elimu ya fedha shuleni

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki Kuu ya Tanzania(BoT) imedhamiria kutoa elimu ya fedha kuanzia ngazi ya elimu msingi hadi vyuo vikuu kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa nidhamu ya kusimamia fedha.

Hayo amesemwa leo Aprili 17, 2024 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akifungua warsha kuhusu uchopekaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali na taasisi na elimu ya juu nchini.

Waziri Kipanga amesema serikali ya awamu ya sita imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii.

“Wizara tutahakikisha elimu ya fedha inafundishwa katika mfumo wa elimu nchini hivyo twende kwa haraka kuhakikisha vijana ambao ni sehemu ya jamii nchini wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha hivyo natarajia wakuu wa vyuo mtabeba uelewa huo muhimu kwa vyuo vyetu nchini,” amesema Kipanga
.
Amesema BoT, itaendelea kusimama na vyuo na taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii hata katika elimu zisizo rasmi.

Ameviagiza vyuo vikuu kushirikiana na BoT kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo ili kuboresha mbinu na nyenzo za kufikisha ujumbe huo kwa jamii.

“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipatiwe taarifa ya tathmnini mtakazofanya ili itusaidie katika kufanya maamuzi, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii,” amesema.

Naye Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema elimu ya fedha inakuwa ni sehemu ya masomo yafundishwe ngazi zote na somo hilo liingizwe kwenye mfumo ya elimu msingi hadi vyuo vikuu.

“Aprili mwaka jana, BoT iliwashirikisha wakuu wa taasisi za Elimu ya Juu nchini, kwa uwakilishi wa wakuu wa vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTIVET kwa lengo la kukubaliana juu ya azma ya kufundisha somo la elimu ya fedha ngazi ya elimu ya juu nchini.

“Hadi hivi sasa taasisi tatu za elimu ya juu zimechukua hatua za kuingiza somo la elimu ya fedha katika mitaala yao, hivyo warsha hii ni kuchochea uwepo wa elimu ya fedha kwa vyuo vingi nchini kuendana na mabadiliko ya mageuzi ya kiuchumi nchini,”amesema.

Sauda amesema takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 inaonesha takribani watu asilimia 34.5 ni vijana walio na umri kati ya miaka 15-35 hivyo ili kuleta tija na ufanisi katika masuala ya uchumi ujuzi na uzoefu wa masuala ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azma hiyo.

Amesema elimu ya fedha kwa Watanzania kutachochea maendeleo kwa kuongeza utumiaji rasmi wa huduma za fedha na kuwawezesha watu wengi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi kukuza uchumi kwa ujumla.

Sauda amesema elimu kwa vijana wa vyuo vikuu itawasaidia kuweka akiba, kupanga bajeti na kufanya uamuzi wa masuala ya fedha kwa kuzingatia viashiria hatarishi na kuelewa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za fedha ili kufanya maamuzi sahihi ya fedha ili waitawale.

” Tunatarajia kujenga ‘displine’ ya fedha kupitia elimu ya fedha kwani watakuwa na uwezo wa kutawala fedha sio fedha kuwatawala vijana hao,” amesema.

Pia amesema BoT kwa kushirikiana na wadau wengine wa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha, imetoa muongozo na mtaala wa elimu ya fedha kwa wakufunzi ambao utatumika na taasisi za elimu ya juu kwa kuwafundisha watoa huduma za elimu ya fedha kuwafikia wananchi wote walio nje mfumo wa elimu.

“Tayari tumeingia makubaliano na baadhi ya taasisi zaa elimu katika mtaala huo wa kufunzi wa fedha na tulioingia nao makubaliano ni Chuo Kikuu cha Iringa, Zanzibar, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha(IFM) na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania ,” ameseama.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), Felix Adam amesema warsha hiyo ni muhimu kwake kwa sababu hayo maeneo yanayojadiliwa yatawasaidia kuwapa elimu ya fedha wahitimu wao.

” Sisi SUA tuliona changamomoto na tukaanza maandalizi ya mitaala yetu ya elimu na kubuni mambo kadhaa hivyo mafunzo hayo yatasaidia kwenda kuboresha mitaala yetu ikiwa kubadilisha tabia za wahitimu kufanya maamuzi ya matumizi na uwekaji wa akiba ya fedha,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles