24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Bashungwa: Wapangaji wa nyumba za TBA mlipe kodi kwa wakati

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka wapangaji wanaoishi katika nyumba na majengo ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya pango ili fedha hiyo itumike kujenga majengo mapya na kuboresha huduma katika majengo mengine ya Wakala huo.

Bashungwa alitoa agizo hilo leo, Julai 23, 2024, katika hafla ya ufunguzi wa jengo la makazi ya watumishi wa umma la Magomeni Kota Awamu ya Pili B, lenye ghorofa saba, katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.

“Serikali itaendelea kufanya kila jitihada za kujenga makazi bora ya watumishi, lakini watumishi mliopata fursa ya kukaa kwenye nyumba za TBA, kulipa kodi ni wajibu. Mkilipa kodi inatupa uwezo wa kuboresha huduma ya makazi bora,” alisisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameielekeza TBA kusimamia ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wadaiwa sugu kulingana na mikataba waliyojiwekea ili kodi hizo ziweze kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu na nne (Block C na D) yanayoendelea katika eneo la Magomeni ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 15.

Aidha, alisema Serikali imerekebisha sheria za TBA na kutoa fursa kwa kuingia ubia na sekta binafsi ili kurahisisha ushirikishwaji wa sekta binafsi na taasisi za fedha kwa ajili ya uendelezaji wa milki na kuwahudumia watumishi wa umma wenye uhitaji wa makazi.

Bashungwa alieleza kuwa ujenzi wa jengo la makazi ya watumishi wa umma la Magomeni Kota Awamu ya Pili B, lililogharimu kiasi cha Sh Bilioni 5.6, ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025 na ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha makazi bora.

Kadhalika, Bashungwa aliipongeza TBA kwa matumizi bora ya ardhi na mipango mizuri ya majengo ya kisasa katika eneo la Magomeni lenye ekari 32,000 lililokuwa na wakazi zaidi ya 645 kwa kuweza kutumia ekari 9 kutosheleza wakazi hao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema kuwa mkoa huo unatakiwa kupangwa upya kwa kuwa na mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na mashirika ya kiserikali na sekta binafsi ili kuuwezesha kuwa miongoni mwa miji mikubwa Afrika kufikia mwaka 2030.

Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, alieleza kuwa kazi zote katika mradi huo za ubunifu, ujenzi, na usimamizi zimetekelezwa na TBA kwa kutumia wataalam wake wenyewe kwa kuzingatia mabadiliko chanya ya ukuaji katika sekta ya uchumi, mipango miji, na teknolojia ya ujenzi, mawasiliano, na miundombinu.

Kondoro alieleza kuwa jengo hilo limefungwa mfumo wa kisasa wa ‘Payless’ ambapo itakapofika wakati wa kulipa kodi ya pango na mpangaji akawa hajalipa, moja kwa moja anakosa huduma ya umeme na maji katika nyumba yake na akilipa kodi ya pango, huduma ya umeme na maji inarejea mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles