Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza safari za treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma huku nauli ya chino ikiwa ni Sh 31,000.
Safari hizo zilizoanza leo Julai 25,2024 ni utelelezaji wa maagizo aliyoyatoa Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa mwaka jana ambapo aliliekeza shirika hilo kuhakikisha ifikapo Julai mwaka huu linaanza safari hizo.
Treni hiyo iliyokuwa na mabehewa 14 na abiria zaidi ya 900 ilianza safari saa 12:00 asubuhi katika Stesheni Kuu ya Dar es Salaam.
Baadhi ya abiria waliozungumza na waandishi wa habari wamepongeza hatua hiyo na kusema itawarahisishia kwa kuokoa muda na gharama.
“Kilichonisukuma kusafiri na treni kwanza ni mara yangu ya kwanza, sijawahi kupanda treni kwahiyo ilikuwa ni kiu yangu kutumia usafiri huu. Nawashauri Watanzania wengine watumie usafiri wa treni kwa sababu ni bora na salama zaidi,” amesema Mchungaji wa Kanisa la Anglikana,
Naye Rose Mchau kutoka Mkuranga mkoani Pwani, amesema amefurahia kupanda treni hiyo kwa sababu ina mazingira mazuri na inatumia muda mchache.
Mkurugenzi Mtendaji wa TRC, Masanja Kadogosa, amesema wanajivunia kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kumshukuru kwa juhudi zake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.