Na Ramadhan Hassan, Dodoma
UTAFITI unaonesha kwamba kukosekana kwa maarifa ya kielimu kutoka katika vyanzo vya uhakika na vya kutegemewa kama sekta ya elimu kumesababisha waajiriwa na wanafunzi kutokuwa na utamaduni wa kujipanga kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Hayo yameelezwa leo ,Jumanne Desemba 8, mwaka huu, jijini Dodoma na Mtafiti, Dk.Mkumbo Mitula wakati wa uzinduzi wa utafiti wa ‘Umuhimu wa elimu ya mipango ya kustaafu na uzee bora kwa waajiriwa na wanafunzi wa elimu ya msingi na ya upili nchini Tanzania’.
Akisoma risala mbele ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Uwekezaji, Doroth Mwaluko ambaye alimwakilisha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Dk.Mitula amesema utafiti uliofanyika unaonesha kukosekana kwa maarifa ya kielimu kutoka katika vyanzo vya uhakika na vya kutegemewa kama sekta ya elimu kumesababisha waajiriwa na wanafunzi kutokuwa na utamaduni wa kujipanga kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Akiuzungumzia utafiti wake,Dk.Mitula alisema aliuanza Aprili mwaka huu ambapo amedai lengo kuu ni lilikuwa ni kuchunguza umuhimu uliopo wa elimu mipango ya maandalizi ya kustaafu na uzee bora kwa waajiriwa na wanafunzi wa elimu ya msingi na ya upili nchini Tanzania.
Amesema utafiti huo umetumia njia zote za ustahilivu na kitakwimu ambapo amedai kwa njia ya ustahilivu,sampuli mgao imetumika kupata sampuli ya washiriki 120 wa aina mbili ambao ni wafanyakazi na wanafunzi kutoka katika maeneo manne tofauti yaliyofanyika utafiti huo.
MAPENDEKEZO KWA SERIKALI
Mtafiti huyo amesema utafiti huo unapendekeza iundwe timu ya pamoja miongoni mwa watafiti,watengeneza mitaala na wadau,Serikali iingilie kati suala hilo kwa miguu yote miwili kwenye kuboresha sera ya hifadhi ya taifa sera ikutane na hitaji lililoko.
“Pia elimu ya mipango ya kustaafu na uzee bora itolewe kwa waajiriwa kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora na kwa wanafunzi kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia iliingize somo hili katika mitaala yake ili lifundishwe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na elimu ya upili,”amesema.
AIOMBA SERIKALI
Katika hatua nyingine, Mtafiti huyo ameiomba Serikali kugharamia tafiti mbalimbali zinazofanywa na watafiti ili kulisaidia Taifa kupata maendeleo.
“Nitumie nafasi hii kuiomba Serikali kuwasaidia watafiti kwani michakato ya kukamilisha utafiti ni gharama sana.Kwa wale wasomi wenzangu watafiti walio katika taasisi za kielimu wanaelewa,kuna mafungu yametengwa maalum ili kugharamia tafiti,”amesema Dk.Mitula.
Amesema iwapo Serikali inanuia kupata tafiti zaidi kutoka kwa wasomi kwa maendeleo ya Nchi basi ni lazima iingize mikono yake kirasilimali fedha kwa makusudi maalum ili kulisaidia Taifa.