Na Mwandishi wetu
BODI ya Ushauri ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), imewashauri waajiri nchini, kuielewa vizuri dhana ya usalama na afya mahali pa kazi, ikiwamo kuhakikisha wanalinda afya na usalama wa wafanyakazi wao, ili waweze kuzalisha kwa wingi na kufikia malengo.
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini Morogoro Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Adelhem Meru wakati wa kikao kazi baina (OSHA) na Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA) mkoani Morogoro.
Kikao kazi hicho pia kilikuwa na lengo la kuitambulisha kampeni ya Vision Zero mkoani Morogoro kampeni maalumu ambayo inalenga kupunguza ajali na magonjwa sehemu za kazi.
Dk. Meru alisema endapo waajiri hawatazingatia masuala ya usalama na afya, hawataweza kufikia malengo yao waliojiwekea ambao ni lengo kubwa la mfanyabiashara.
“Nitumie fursa hii kuwahamasisha waajiri wote kuielewa dhana ya afya na usalama mahala pa kazi kiuhalisia, tukitoka hapa twende tukahamasiahane kuhakikisha kwamba wafanyakazi wetu wanakuwa katika mazingira ambayo ni salama siyo hatarishi iliwaweze kuzalisha kwa ufaniasi ili tuweze kufikia malengo na kuyavuka,” alisema Dk. Meru.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda alisema waliona kuna umuhimu OSHA kushirikiana na TCCIA katika kuhakikisha wanashughulikia kero na changamoto za wafanyabiashara nchini, kwani mchango wao ni mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
“Hapa kuna wajasiriamali wengi, na kama inavyofahamika kwmaba ndiyo inayoajiri wafanyakazi wengi sana, hivyo tunataka tuilee ikue na iwe rasmi ili iweze kuwa na mchango mkubwa katika Serikali.
“OSHA imetekeleza andiko la Blue print kwa kiasi kikubwa kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyabiashara nchini, kwa kuondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kikwazo kwa wawekezaji na wafanyabishara nchini,” alisema Khadija.
Naye, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro, Mwadhini Myanza ameishukuru OSHA kwa kutekeleza ipasavyo yale yote yalioelekezwa kwenye Blue Brint, na hivyo kuwasaidia wadau wao.
Upande wao baadhi ya washiriki wamesema kikao hicho kimewasaidia na kuwajengea uelewa mpana zaidi masuala ambayo walikuwa hawayaelewi na hivyo yatawasaidia katika shughuli zao wana zozifanya kwa kuhakikisha mazingira ya wafanyakazi yanaboreshwa.