Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM
JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limeandaa Sera ya kitaifa ya ushiriki wa wanawake , Vijana na Walemavu katika siasa na uteuzi.
Sera hiyo ambayo itawakilishwa serikalini ikiwa na mapendekezo mbalimbali kwa lengo kuwasaidia watu wa makundi hayo ili waweze kuingia katika nafasi mbalimbali za uwakilishi bungeni na serikalini.
Akizungumza na Waandishi wa habari mwasilishaji mada mbalimbali wakati wa uchambuzi wa Sera hiyo Deus Kibamba alisema lengo la sera ni kutaka usawa kwa makundi maalum Ili kuwepo na uwakilishi sawa katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Alitolea mfano katika mchakato wa uchaguzi uliofanyika sasa hakuna chama cha siasa hata kimoja kilichoweka uwiano sawa kati ya wagombea wanawake na wanaume.
Alisema Sera hiyo imeishauri Tume ya taifa ya Uchaguzi kwamba katika kipindi cha uchaguzi wakipelekewa majina wayahesabu na kuhakikisha wanawake wanakua na asilimia 30.
“Vyama vya siasa vilitakiwa kuanza na haya kuhakikisha kuwa wanawake wasipungue asilimia 30 ili kuwepo na uwakilishi wao, ” alisema Kibamba.
Aliongeza pia kunatakiwa kuweka upendeleo maalum na hata ikiwezekana kuwepo na mabaraza ya wanawake kitaifa.
Kibamba alisema Sera hiyo inataka pia serikali kuweka utaratibu kwamba kwa kuwa vyama vya siasa vina ruzuku basi vihakikishe sehemu ya ruzuku itengwe kwa ajili ya kuwapa wanawake wagombea ili kuwafanikishia katika kampeni zao.
Pia katika nafasi mbalimbali za uongozi za siasa vyama karibuni vyote vimeweka viongozi wanaume katika nafasi za juu hali ambayo haiwezi ikaleta usawa katika Jamii.
Kibamba pia alizungumzia suala LA uwakilishi wa watu wenye ulemavu ambapo kwa sasa anaweza akachaguliwa mmoja akawakilisha makundi yote.
“Katik sera hii tumependekeza kuwa kuna makundi 10 ya watu wenye ulemavu katika makundi hayo ni vyema kila kundi likapata mwakilishi wake, ” alisema Kibamba.
Pia Sera hiyo imegusia wanahabari kwa kutakiwa kufanya kazi katika weledi hasa katika kipindi cha uchaguzi kwa kutoripoti matusi, kuandika takwimu mbalimbali kwa usahihi na kutokuwa na upendeleo katika kuripoti matukio hayo ya uchaguzi.