Asha Bani
Serikali imeitaka Bodi ya mikopo kutoa mikopo pindi vyuo vitakapofunguliwa kuanza wakati wowote.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua ofisi mpya za Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu zilizopo eneo la Tazara jijini Dar es Salaam na kuitaka Bodi hiyo kujiandaa kulipa wanafunzi wakati wowote vyuo vitakapofunguliwa.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo leo baada ya kukagua ofisi hizo na kufanya kikoa cha pamoja na menejimenti ya Bodi hiyo.
”Katika kipindi hiki ambapo vyuo vya elimu ya juu vimefungwa, HESLB ihakikishe inatumia muda huu kufanyia kazi changamoto zote za wanafunzi ili vyuo vitakapofunguliwa malipo ya mikopo ya wanafunzi yafanyike kwa wakati,” amesema Waziri Ndalichako
Pia ameipongeza HESLB kwa kutekeleza agizo la Serikali la Kuhakikisha Taasisi zote za umma zinahamia kwenye majengo ya Serikali ili kupunguza gharama.
Amesema anaamini watafanya kazi kwa utulivu na kutaongeza ufanisi katika tendaji wa kazi zao.
Prof. Ndalichako pia alitumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi wa HESLB kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Akiongea katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema HESLB ipo tayari kuwahudumia wanafunzi muda wowote vyuo vitakapofunguliwa kwa kuwa fedha zinazohitajika, mifumo na taarifa za wanafunzi zipo.