Na TUNU NASSOR-DARES SALAAM
TAASISI ya Dawa Asili na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO) imesema uwezekano wa kupatikana kwa tiba ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona nchini unategemea ushirikiano baina yao na taasisi za Serikali.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo alisema iwapo Serikali itaratibu vizuri ushirikiano huo, ni rahisi kupatikana kwa tiba mapema.
Alisema tayari kama nchi ina ujuzi, dawa na wataalamu wa tiba asili ambao wana uwezo wa kutumia maarifa waliyonayo katika kutafuta matibabu ya ugonjwa huo.
“Tunahitaji kuongeza ushirikiano baina yetu na Baraza la Tiba asili na Tiba Mbadala, Taasisi ya Utafiti wa Dawa Asilia iliyopo katika Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (ITM), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR) pamoja na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema Mwalongo.
Alisema dawa mbalimbali za asili zina vimeng’enyo vya kupambana na kutibu magonjwa ambayo yanafanana na athari za Covid-19, hivyo uwezekano wa kupata tiba nchini upo.
“Tuna dawa za mafua, kukohoa, kifua na mapafu ambazo hutibu na iwapo zikiratibiwa kwa kushirikiana, tunaweza kupata dawa ya kuutibu ugonjwa huu,” alisema Mwalongo.
Mwalongo ambaye pia ni mtaalamu wa tiba asili, alisema tayari wamepokea maelekezo kadhaa kutoka Wizara ya Afya baada ya kuwasilisha maombi yao serikalini.
“Tayari wataalamu 20 walio tayari na dawa mbalimbali za mapafu tumewapa maelekezo ya kuwasilisha dawa zao kwetu,” alisema Mwalongo.
Hadi sasa Tanzania inaaminika kuwa na miti na mimea dawa 12,000 inayotumika katika matibabu ya tiba asili, jambo linaloleta matumaini kupata tiba ya corona.