25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wakunga watakiwa mstari wa mbele vita ya corona

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM 

WAKUNGA nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa kina mama wajawazito ili kuhakikisha kuwa wanawalinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Wito huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Meneja Kiongozi wa Miradi ya Huduma za Afya kwa Mama na Mtoto kutoka Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Felister Mbwana.

Alisema kuwa mkunga pia ana wajibu wa kumlinda mtoto mchanga dhidi ya corona.

“Ili kuepusha vifo vya watoto wachanga kabla na baada ya kujifungua, kila mkunga analo jukumu la kuhakikisha kuwa anamlinda mama mjamzito dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

“Kwani tunaaamini kuwa iwapo watatumia mwanya huo kutoa elimu kwa mama mjamzito dhidi ya maradhi haya ya corona, basi ni bayana kuwa itasaidia kupunguza maambukizi yasiyokuwa ya lazima kwa wajawazito.

“Sote ni mashahidi kwamba ukimwelimisha mwanamke basi unakuwa umeelimisha jamii nzima, hivyo wakipata elimu kwa usahihi hakuna shaka kwamba jambo hili litadhibitiwa,” alisema Felista.

Alisema kwa sasa UNFPA imejikita katika kutoa mafunzo kwa wakunga wataalamu kuhusu namna ya kumkinga mama na mtoto dhidi ya virusi vya corona pamoja na kuwawezesha vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Msaidizi wa UNFPA hapa nchini, Dk. Wilfred Ochan, alisema kuwa suala la ujauzito na kuzaa litaendelea wakati wa milipuko ya Covid-19. 

“Huduma hizi haziwezi kuahirishwa, UNFPA inawashukuru sana wakunga wote wa Tanzania, hivyo tunaungana nao kusherehekea siku yao, tumejitolea kuwaunga mkono kutoa huduma hizi salama,” alisema Dk. Ochan. 

Akizungumzia siku hiyo, Rais wa TAMA, Feddy Mwanga, alikiri kuwa wakunga wanafanya kazi katika mazingira magumu katika muktadha wa ugonjwa ambao haujajumuishwa katika mtaala wowote wa wakunga.

“Chama cha Wakunga wa Tanzania (TAMA) kinawashukuru wakunga wote kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, ya kuokoa maisha ya wanawake na watoto wachanga na watoto chini ya umri wa miaka mitano, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua kila siku na wakati wote wa janga hili la Covid-19,” alisema Mwanga.

Katibu Mkuu wa TAMA, Dk. Sebalda Leshabari akizungumza kwa niaba ya wakunga nchini, ameiomba Serikali kuwatatulia changamoto ya uhaba wa vifaa vya kujikinga na Covid-19 ili wakunga wanapotoa huduma kwa mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua waweze kujizuia na kuwakinga wanaojifungua wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.

Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani kwa mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘umuhimu wa mkunga katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles