Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WILAYA za Chamwino, Bahi na Kongwa mkoani Dodoma, zimepinga mfumo wa stakabadhi ghalani katika msimu wa mavuno wakidai si rafiki kwao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, White Zuberi, alisema katika Wilaya ya Kongwa wakulima wataendelea kuuza mazao yao minadani na magulioni ikiwemo soko la mahindi la Kibaigwa.
White alisema katika baraza la madiwani hawajapitisha mpango wa stakabadhi ghalani, hivyo wakulima wana uhuru wa kuuza kwa maslahi yao kulingana na gharama za uzalishaji.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi katika kijiji cha Mpwayungu wilayani Bahi, wakazi wa eneo hilo walidai bado hawana mpango wa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani katika msimu wakidai si rafiki kwao.
Juma Ramadhan alisema mfumo huo si rafiki kwa wakulima kwani unawataka kuwa na akaunti za benki wakati wengi ni wazee na huduma za mabenki ziko mbali na maeneo yao.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omari Badwel (CCM) alisema katika halmashauri yao bado hawajapitisha mfumo huo na kuwataka wakulima wanaendelea kuuza mazao yao katika maeneo ambayo wanaona yanafaa.
Badwel alisema msimu huu ni wa mavuno hivyo wakulima wameshaanza kuuza mazao yao kwenye minada na maeneo ambayo wamekuwa wakiyatumia siku zote.
Awali Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, alikiri kuwa licha ya uzuri wa mfumo huo, bado una changamoto kwa wakulima.
Mgumba alisema mfumo mzima na jinsi ulivyoratibiwa ni mzuri kwani unatoa tija kwa wakulima kama utekelezaji wake ungefanyika bila mizengwe.
Alisema Serikali haitaki kumpangia mkulima bei ya kuuza na namna ya kuuza mazao yake bali inataka kuona usawa ukitendeka na wakulima wakiuza mazao yao katika vipimo vinavyokubalika.