ELIUD NGONDO Na NORA DAMIAN, MBEYA/DAR
IKIWA imebaki miezi saba kabla ya Oktoba ambapo Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika, viongozi wa Chama cha NCCR – Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameonekana kuwa na vita ya maneno hali inayofifisha matumaini ya vyama hivyo kuungana kwenye uchaguzi huo.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita ambao upinzani ulitoa ushindani mkubwa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chadema na NCCR, walionekana kuwa nguzo ya ushirikiano uliokuwa umeundwa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hali hiyo ilitokea baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kujiuzulu siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni na kufanya chama hicho bara kuzorota huku upande wa Zanzibar uliokuwa ukiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalimu Seif Sharif Hamad, ukibaki na nguvu.
Katika umoja huo, pia kulikuwa na chama cha NLD, ambapo kwa mwaka huu ilitarajiwa umoja huo ungeongeza nguvu kwa kujumuisha chama cha ACT Wazalendo, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuwa gizani.
Hali ilivyo
Kwa siku za karibuni Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia, ameonakana kuwalaumu wenzake wa Chadema na wakati mwingine kuna watu wanaomtukana wakimwita msaliti.
Jana kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na taarifa zinazodaiwa kuwa za Mbatia zikieleza kuwa kiongozi huyo ametishia kutoa siri za Ukawa endapo ataendelea kuitwa msaliti lakini alipoulizwa na Mtanzania Jumapili, alisema taarifa hizo si zake.
Pia jana hiyohiyo alifanya mkutano na waandishi wa habari jijini Mbeya, akisema alitumia fedha zake kuhakikisha Ukawa inadumu lakini baadhi ya vyama vilipoungwa mkono na kushinda vilividharau vyama vingine vilivyoshiriki.
“Nimetumia fedha zangu za mfukoni kulipa madeni yaliyosababishwa na Ukawa wakati ilitakiwa nizipeleke kwenye familia yangu, lakini bado watu wanasimama na tunitukana,” alisema Mbatia.
Alisema chama hicho kilikuwa ni miongoni mwa vyama vilivyounda Ukawa lakini kutokana na muungano huo imekuwa ni changamoto.
Alisema kwa sasa chama hicho kimeamua kujipanga kuhakikisha kinashika dola kutokana na mambo ambayo yamekuwa yakifanyika ndani ya Ukawa.
Alisema Ukawa iliundwa kwa ajili ya kutaka Katiba mpya na sasa Serikali iliyopo haina mpango huo hivyo chama kinatakiwa kujipanga kuhakikisha malengo yaliyopo ndani ya katiba yake yanatimia.
“Lengo la kila chama ni kutaka kinatawala, hakuna chama kilichoambiwa kitatawala milele, hivyo sisi kama NCCR Mageuzi tumeamua kuanza mchakato wa kuhakikisha tunashirikai Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” alisema.
KILICHOMPELEKA MBEYA
Mbatia alisema amekwenda Mbeya kukiimarisha chama chake na wala hajatumwa na mtu kwenda kuvuruga Chadema kama inavyotafsiriwa.
“Mimi nimekuja hapa Mbeya kwa lengo la kukiimarisha chama changu na kuzungumza na wanachama kwa kutumia mikutano ya ndani na si kama maneno yanavyosemwa kuwa nimetumwa na Rais (John) Magufuli baada ya kutoka Ikulu,” alisema Mbatia.
Alisema yeye na viongozi wengine waliomba kukutana na Rais Magufuli ambapo waliruhusiwa na walizungumza mambo ya kitaifa ikiwa ni pamoja na suala la Tume Huru ya Uchaguzi na si kuzungumza kuuvunja Ukawa.
Alisema katika ziara yake aliyoifanya Jimbo la Rungwe, Busokelo na Kyela alivuna zaidi ya wanachama 3,300 na kwamba huo ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha wanasimama na kushiriki uchaguzi.
KAULI YA CHADEMA
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, aliliambia Mtanzania Jumapili kuwa Ukawa haukufa baada ya uchaguzi na kwamba waliendeleza ushirikiano mpaka bungeni ndiyo maana Mbatia ni waziri kivuli.
“Yeye alitegemea Chadema ikajenge chama chake, kila chama tulikubaliana kwamba kiendelee kujijenga, kifanye ziara zake, sasa anaposema alitengwa alichokuwa anataka ni nini?
“Mbatia anatafuta huruma ya wananchi, ndiyo maana ameishia kulialia anasema mara anatukanwa na hasemi nani anamtukana, mara anatishia ‘nitatoa siri zenu’ sasa tunashangaa ni siri gani yeye anazo Dk. Slaa (aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Wallboard) hakuwa nazo wakati alikuwa Ukawa mpaka mwisho.
“Kwa hiyo haya mambo mengine ni kulialia tu kutafuta huruma ya wananchi, ajenge chama chake,” alisema Mrema.
Alisema hata kama Mbatia hana nia ya kushirikiana na wenzake, asitafute sababu za pembeni kwa sababu ushirikiano haulazimishwi.
“Kama yeye hana nia asianze kutafuta vijisababu vidogo vidogo, kama ameshaamua chama chake anataka kwenda mwenyewe hana sababu ya kuchokoza watu, aendelee kujenga chama chake, sisi tunaendelea kujenga chama chetu na tutashirikiana na vyama ambavyo vitakuwa tayari baada ya kukubaliana,” alisema.
UKAWA YA 2020
Hivi karibuni Mbatia alikaririwa na vyombo vya habari akisema katika uchaguzi wa mwaka huu si lazima kushirikiana na vyama vilivyokuwepo 2015 bali wanaweza kujitokeza wengine au kupungua.
“Tutakwenda kwenye meza yeyote ambaye anataka tushikiriane kuna yale ya siri ya ndani ambayo tulishazungumza ndani, tutazingatia hekima pia na kuona namna gani tutashirikiana. Si lazima wale tu tuliokuwa kwenye ushirikiano wa 2015, wanaweza kujitokeza wengine zaidi au kupungua kwa masilahi endelevu.
“Ushirikiano tunaouhitaji kwa sasa ni wenye masilahi kwa wote ‘win win situation’, usiwe msindikizaji tu, masilahi ndani ya chama chako, umma na kustawisha taifa kwa ujumla,” alisema Mbatia.
Alisema pia iwapo watataka kushirikiana ni lazima umoja huo usajiliwe kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ili baada ya uchaguzi waweze kutekeleza waliyokubaliana.
“Ukawa ulikuwa ni zaidi ya vyama vya siasa makubaliano ya namna hiyo lazima yawe ya kisheria, yawe kwenye mkataba na lazima yawe ya kisheria na yanayotekelezeka.
“Nikiri mwaka 2015 hakutukuwa na mkataba wa kisheria, kwamba mnakubaliana lipi kwamba mkishiriki kwenye uchaguzi mtashirikiana vipi.
“Ushirikiano wenye masilahi ya pande zote hauwezi kuwa ushirikiano wa upande mmoja, usipokuwa na mkataba unaokubalika, tunaweza kuwaomba wenzetu kwa kuwa tuliwaunga mkono uchaguzi uliopita basi tuwaombe na wao wakati huu watuunge mkono sisi,” alisema.