Aveline Kitomary – Mwanza
HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa – Bugando, imeboresha huduma za matibabu ya figo hali iliyosaidia wagonjwa wa kanda hiyo kupata huduma.
Hadi sasa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 90 katika kliniki moja.
Akizungumza jana jijini Mwanza wakati wa kampeni ya ‘Tumeboresha sekta ya afya’ inayoendeshwa na maofisa habari wa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Daktari Mbobezi wa magonjwa ya figo, Ladius Ludovick, alisema awali walianza na mashine 10, lakini sasa wana 23.
“Kituo hiki cha figo kilianzishwa mwaka 2016. Tulikuwa na mashine 10 na tulianza na mgonjwa mmoja, ndani ya miaka minne tumeweza kuongeza mashine hadi 23 toka mwaka 2016, katika huduma ya kusafisha tunahudumia wagonjwa 40 hadi 45 kwa siku moja.
“Kati ya hao kuna wagonjwa wa tatizo la muda mfupi la mshtuko wa figo na kuna tatizo la muda mrefu la figo, asilimia 70 ya magonjwa ya figo yanatokana na tatizo la presha na kisukari,” alibainisha Dk. Ludovick.
Alisema asilimia kubwa ya wagonjwa wa figo wanaowaona ni wale wenye ugonjwa sugu wa figo, huku tatizo la mshtuko wa figo likitibiwa kwa muda mfupi.
“Mshtuko wa figo ni matatizo ya figo ya muda mfupi, figo inashindwa kufanya kazi kwa muda, mfano mama mjamzito aliyejifungua akapoteza damu nyingi figo inaweza kushindwa kufanya kazi kwa muda na sumu inarundikana mwilini, huyu unaweza kusafisha damu ndani ya wiki mbili au tatu anapona,” alisema Dk. Ludovick.
Hata hivyo Dk. Ludovick alisema kwa ugonjwa sugu wa figo, huwa wanahamasisha kwenda kupandikiza figo nyingine.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bugando, Dk. Bahati Wajanga, alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne, ni pamoja na utoaji kamili wa huduma za saratani.
“Bugando imekuwa hospitali ya pili baada ya Ocean Road kutoa huduma kamili za saratani kama mionzi ya ndani, nje na dawa hii ni baada ya usimikaji wa mitambo ya kisasa ya kutolea huduma.
“Kupitia Wizara ya Afya, Sh bilioni 5.5 zilitolewa kwa ajili ya kujenga jengo la saratani na kununua mashine nne za mionzi.
“Mafanikio mengine ni upanuzi na ujenzi wa vyumba vya upasuaji vya kisasa. Hii imefanya hospitali kuwa na vyumba 13 vya kisasa kutoka vyumba vya awali. Hii imepunguza muda wa kusubiri upasuaji kwa wagonjwa na kutoa matibabu ya kibingwa kupitia mitambo ya kisasa,” alisema Dk. Wajanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba.
Alisema uboreshwaji wa huduma za dharura umeweza kuokoa maisha ya watu kutokana na kuhudumia wagonjwa 100 kwa wakati mmoja.
“Awali tulikuwa tunaweza kupokea na kuhudumia wagonjwa wa dharura 50, lakini sasa idadi imeongezeka. Upanuzi huu umeongeza vitanda kutoka 14 hadi 24, kuweka mitambo ya kisasa ya huduma za dharura na vyumba vya upasuaji viwili katika idara hii.
“Huduma zingine zilizoboreshwa ni upasuaji wa macho ambapo takribani wagonjwa 12,000 wa macho wameonwa kwa mwaka 2019. Hata hivyo, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji ni 900 kwa mwaka huo,” alisema Dk. Wajanga.
Alisema uwepo wa mitambo ya kufua hewa ya oksijeni umesaidia utoaji bora wa huduma kutokana na kupunguza matumizi ya fedha za ndani.
“Kwa wastani hospitali hutumia mitungi 20 hadi 30 kwa siku na mtungi mmoja kwa bei ya soko ni Sh 45,000 na kwa sasa hospitali inaweza kuzalisha mitungi 2,100 kwa mwezi na gharama za uzalishaji ni nusu ya bei ya sokoni,” alibainisha Dk. Wajanga.