24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Utafiti wafichua ukubwa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto

Christina Gauluhanga – Dar es Salaam

TAFITI zinaonyesha wajawazito wanaoishi na virusi vya Ukimwi ambao hawajaanza kutumia dawa za kuvifubaza, wana uwezekano wa kuambukiza watoto watakaojifungua kwa asilimia 45.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa kongamano la kujadili tafiti za udhibiti maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (EMTCT), lililoandaliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas), Mhadhiri wa chuo hicho, Dk. Augustine Massawe, alisema tafiti zao zimebaini endapo mama ataanza kumeza dawa mapema kabla ya kujifungua, uwezekano wa kumwambukiza mtoto ni asilimia mbili.

Dk. Massawe ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, alisema katika utafiti wa afya ya mama na mtoto kuhusu maambukizi ya Ukimwi waliofanya, walibaini uwezekano wa mtoto kupata maambukizi hayo akiwa tumboni ni asilimia 15, wakati wa kujifungua 20 na anaponyonyesha ni 40.

“Tafiti zinaonyesha hali ya maambukizi kwa mjamzito ambaye ameathirika na hajaanza kupata dawa, uwezekano wa kumwambukiza mtoto ni mkubwa tofauti na yule ambaye ameanza kutumia dawa,” alisema Dk. Massawe.

Alisema zipo njia nyingi zinazochangia uwezekano wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika kipindi cha kunyonyesha, ikiwamo kujamiiana na mtu mwenye maambukizi, kuchanganya maziwa ya bandia na ya mama, lishe duni na nyinginezo.

“Maziwa bandia hayana kinga halisi, hivyo ukichanganya na ya mama kisha kumpa mtoto kwenye ile chupa ni rahisi kupata michubuko ambayo inaweza kumsababishia maambukizi wakati wowote,” alisema Dk. Massawe.

Alisema katika tafiti zao pia walibaini udanganyifu wa wenza umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa.

“Wapo baadhi ya wanawake wamekuwa wakibeba ujauzito, lakini hawana uhakika wa baba wa mtoto, hivyo kushindwa kuongozana naye kliniki na kusababisha idadi ya wanaume wanaoungana na wenza wao kliniki kupungua,” alisema Dk. Massawe.

Pia alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakichangia kuzidi kukithiri kwa maambukizi kwa sababu ya kuhofia kuwapima Ukimwi watoto wao wiki ya sita baada ya kuzaliwa.

“Hii imekuwa changamoto kubwa kwani wanawake wengi wanapojifungua na kuambiwa warejee baada ya wiki sita, wengi wamekuwa wakitokomea, hivyo kushindwa kufahamu hali ya kiafya ya watoto,” alisema Dk. Massawe.

Alisema wanaishukuru Serikali na wadau wa afya kwa jitihada mbalimbali ambazo zimechangia kushuka kwa maambukizi ya Ukimwi katika mikoa mbalimbali nchini.

Naye, Ofisa Upelembaji na Tathimini kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mukome Nyamuhagata alisema jitihada za wadau wa afya zimechangia kushuka kwa maambukizi ya Ukimwi kutoka asilimia 26 mwaka 2011 na kufikia asilimia saba mwaka huu.

Alisema wakati wanaanza mkakati wa kutokomeza maambukizi ya Ukimwi mwaka 2017, maambukizi yalikuwa ni asilimia 7.6, mwaka 2018 ni asilimia 11.05 na mwaka jana asilimia 7.46.

“Mkakati wetu hadi kufikia asilimia 2021 angalau kiwango cha maambukizi kishuke na kufikia asilimia  nne,” alisema Nyamuhagata.

Alisisitiza kuwa wanaendelea na jitihada kuongeza ubora, upimaji watoto na wajawazito pamoja na kuwaunganisha kwenye matibabu pindi wanapobainika kuishi na virusi vya Ukimwi.

Nyamuhagata alisema wanawake wengi hawapendi kuwaleta katika vituo vya afya watoto wao walioathirika kwa kuogopa unyanyapaa jambo ambalo linahatarisha maisha ya watoto hao na kuchangia ongezeko la wagonjwa huo.

Aliongeza kuwa pia wanakabiliwa na changamoto ya utoaji huduma, utumishi huduma na uchache wa watoa huduma ambao wapo asilimia 54 nchi nzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles