33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Rweikiza abwagwa kesi ya madai aliyomfungulia kada mwenzake wa CCM

Na Renatha Kipaka -Bukoba

MAHAKAMA  Kuu Kanda ya Bukoba,  imetupilia mbali kesi ya  madai namba 12 ya mwaka 2016  ya fidia ya Sh bilioni 1.216 iliyofunguliwa  na Mbunge wa Jimbo la Bukoba vijijini  Jasson Rweikiza dhidi ya mjumbe wa Halmasahauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM )Mkoa wa Kagera, Novatus Nkwama, akidai alimdhalilisha.

Akisoma hukumu Jaji wa mahakama hiyo Dk. Ntemi Kilekamajinga, alisema msingi wa kisheria ni wajibu mdai kuthibitisha madai yake mahakamani.

Jaji Dk. Kilekamajinga, alisema katika kesi hiyo aliangalia hoja nne za kesi hiyo ambavyo ni je mdaiwa alimdhalilisha  mdai? Maneno yaliyosemwa yalikuwa na udhalilishaji? Je maneno hayo yalisababisha madhara yoyote ya madi? Na je maneno ya kushusha hadhi kwa jamii yajulikane na mtu zaidi ya mmoja?

“Nimechambua ushahidi uliotolewa na mdai yeye hakuwahi kuyasikia maneno ingawa alisikia kupitia kwa watu wakati huohuo anasema alisikia kipindi kikirudiwa katika radio, anasema kama yeye hakusikia kupitia masikio yake ushahidi wake unaleta ukakasi”alisema  Jaji Dk Kilekamajinga.

Alisema kifungu cha 62 (1) cha sheria za ushahidi alitakiwa kuijumuisha Radio Karagwe kwenye ushahidi mahakamani hapo.

Aliieleza mahakama kwamba mdai hakumpeleka mahakamani mtangajazi wa radio hiyo wala uthibitisho wowote toka Radio Karagwe kwamba ilirusha matangazo yaliyomdhalilisha.

Alisema kuhusu madai kuwa Rweikiza alitukanwa kwenye nyumba ya Nazir Karamagi wakati wa dua, mtu anaalikwa kusalimia halafu anaanza kuropoka na kuanza kutukana hilo jambo pia linaleta ukakasi.

Alisema shahidi mwingine wa mdai aliieleza mahakama kuwa akiwa njiani kuelekea Bukoba mjini alipita Itawa akasikia mdaiwa anamtukana mdai “sijui kilichomsimamisha kwa kweli, sasa nimejiuliza alitumia usafiri gani kwanza, hakuwa pale na ajenda ilikuwa moja ya kujadili wizi katika Kitongoji pia ushahidi wake ni wa ukakasi.”

Alisema mashahidi walioileza mahakama kuwa waliacha kazi kwa mdai baada ya kusikia maneno ya udhalilshaji  walishindwa kuithibitishia mahakama kama kweli waliacha kazi kwasababu hawakuwasilisha barua.

 Alisema mdai alishindwa kuithibitishia mahakama madai yake ya watoto 50 wa kiislamu waliokuwa wanasoma kwenye shule yake ya (Rweikiza primary school) waliohama baada ya kusikia maneno kuwa anawabagua Waislam na kumsababishia hasara kwa sababu hakuleta idadi ya wanafunzi waliokuwepo shuleni kabla ya maneno na waliohama baada ya maneno.

Alisema cha msingi ni uthibitisho wa jambo linalosemwa kwa msingi wa kisheria hivyo kesi hii imejaa msuguano wa kisiasa zaidi mdai na mdaiwa wanaongalia kugombea mwaka 2020.

Alidai kwa kutengeneza kesi sababu ya kumuumiza mwingine mahakama haiwezi kuliacha jambo hilo, mahakama imeshindwa kujiridhisha kama kweli maneno hayo yalitolewa na mdaiwa  na kama yalitolewa yanaweza kuwa yalikuzwa zaidi kwa sababu mdai hakusikiliza kwa masikio yake mwenyewe.

Alisema mahakama imeona madai hayana msingi wowote hivyo pande zote mbili ziweze kubeba gharama zake za kesi.

Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo jaji huyo alisema kesi hiyo ilishasuluhishwa na CCM, viongozi wa Serikali na mahakama pia ilisuluhisha ikashindikana.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Rweikiza akidai fidia ya Sh bilioni 1.216 akidai alidhalilishwa na Nkwama aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Bukoba Vijijini.

Rweikiza, alisema alitukanwa kuwa yeye ni mwizi na kwamba alimuibia mdaiwa gari, yeye ni mbagauzi anawabagua waislam na aliiba kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Upande wa mdai ulikuwa na mashahidi saba na mdaiwa mashahidi wanne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles