Nyemo Malecela -Kagera
KUTOKANA na ongezeko la abiria wa usafiri wa anga mkoani Kagera, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limeongeza ndege ya pili ili kukabiliana na kiwango cha abiria.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladisraus Matindi amesema Mkoa wa Kagera una zaidi ya abiria 2,400 kila mwezi sawa na asilimia 70 ya ujazo wa ndege kwenda na kurudi.
Matindi aliyasema hayo jana mkoani Kagera, alipofanya ziara ya kawaida ya kikazi.
Alisema katika kipindi cha msimu wa sikukuu, shirika limelazimika kupeleka ndege mbili ili kumudu wingi wa abiria.
“Kwa mujibu wa meneja wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba, ndege zote zimejaa hadi Januari 15.
“Biashara ya usafiri wa ndege ni sawa na biashara nyingine, kwani nayo inakuwa na msimu kama ilivyo biashara nyingine, tumelazimika kuongeza ndege ya pili kipindi cha sikukuu kwa kuwa ndicho kipindi ambacho kinakuwa na abiria wengi mkoani Kagera,” alisema Matindi.
Alisema kwa mkoa huo, mara nyingi kuanzia Desemba 15 hadi Januari 15 ni kipindi ambacho kinakuwa na abiria wengi na baada ya hapo kiwango cha abiria kinapungua, hivyo baada ya msimu huo kuisha ndege ya pili itaondolewa.
“Tutaendelea na utaratibu wa ndege moja hadi msimu wa Pasaka utakapofika ndipo tutarudisha utaratibu wa ndege ya pili,” alisema Matindi.
Pia alitolea ufafanuzi malalamiko ambayo yamekuwepo kwa abiria kuhusu mizigo yao kukwama uwanja wa ndege.
“Ndege inaporuka kuna uzito wa ndege unaotakiwa ili iweze kuruka, ambao unatokana na uzito wa ndege yenyewe, abiria, mafuta na mizigo.
“Sasa mara nyingi inatokea abiria wamejaa ndege, ukiweka mizigo ndege hiyo haitaweza kuruka, ndiyo maana mara nyingi kunatokea tatizo la mizigo kushindwa kusafirishwa,” alisema Matindi.
Alisema changamoto hiyo inatokana na Uwanja wa Ndege wa Bukoba kuwa mfupi.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliwaomba wakazi wa mkoa huo kutumia usafiri wa anga kiuchumi zaidi.
“Wafanyabiashara wengine ambao wanatumia mashirika mengine ya ndege kwenda nje ya nchi na kurudi kibiashara, tunawaomba kutumia ndege za ndani,” alisema Gaguti.