31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Chanjo ya homa ya ini yaadimika Simiyu

Derick Milton -Simiyu

 UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu, umesema kasi kubwa ya wananchi wanaojitokeza kupima na kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa homa ya ini, imesababisha kuwapo uhaba wa chanjo hiyo.

Kutokana na changamoto hiyo, hospitali hiyo inalazimika kutoa chanjo kwa vipindi kwani mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wake wa kununua chanjo hiyo kutokana na uchanga wake.

Akizungumza na waandshi wa habari hospitalini hapo jana, mtaalamu wa maabara, Raphael Kambona alisema wanakutana na tatizo la upatikanaji wa chanjo ya homa ya ini za kutosha hali inayowalazimu kusitisha huduma hiyo kwa vipindi.

Kambona alisema ndani ya miezi sita tangu hospitali hiyo ianze kutoa huduma, mwitikio wa wananchi wa kupima na kupatiwa chanjo umekuwa mkubwa sana na wamefikia hatua ya kusitisha kupokea wateja wapya.

“Kuna wakati tunalazimika kusitisha kupokea wateja wapya kuwapatia chanjo, akiba tuliyonayo ni kidogo na endapo tutawaanzishia chanjo wateja wapya, tutashindwa kuwakamilishia dozi wateja wa zamani.

“Tumekuwa tukiwarudisha wateja wetu wapya kwa sababu ya uhaba wa chanjo, na tunafanya hivyo ili wale waliokwisha anza waweze kupata kwa mtiririko unaotakiwa na tukishawaanzishia ni lazima tuwakamilishie dozi kwa  awamu tatu,” alisema Kambona.

Alisema mwitiko wa wananchi kuwa mkubwa unatokana na wengi wao kutangaziwa mara kwa mara kuhusu madhara ya ugonjwa huo na umuhimu wa kupata chanjo.

Kambona alisema ndani ya miezi sita, wananchi 251 sawa na asilimia 3.2 walijitokeza kupata huduma ya upimaji na chanjo ya homa ya ini na kati ya hao wanane waligundulika na homa hiyo na kupewa rufaa za kwenda Hospitali ya Bugando kwa matibabu zaidi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Matoke Mayenjwa alisema tatizo kubwa la changamoto hiyo ni uwezo wa kifedha wa hospitali unaotokana na uchanga toka imeanza kufanya kazi.

Lakini alieleza kuwa kadiri wanavyoendelea kufanya kazi, ndivyo watakavyoweza kujitosheleza kwa kila kitu.

“Uchanga ndiyo tatizo, bado hatujaweza kujitosheleza kibajeti, ila ni matumaini yetu tukiendelea kufanya kazi vizuri tutaboresha huduma muhimu ambazo kwa sasa bado hazijakamilika ipasavyo,” alisema Dk. Matoke.

Hospitali hiyo ilizinduliwa Septemba 2018 na Rais Dk. John Magufuli na ilianza kutoa huduma mbalimbali Juni, mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles