*Kingunge asema yeye ni babu wa vijana Tanzania
NA FREDY AZZAH, BIHARAMLO
MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema Serikali atakayoiunda baada ya kuingia madarakani mambo yake yatakuwa mazuri.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliyasema hayo jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya soko jipya mjini Biharamulo, Mkoa wa Kagera.
“Naomba kura hata kama wewe ni CCM, nipe kura, nataka kura zote za Biharamulo, natamani kusema kama Wakristo wanavyosema namkataa shetani na mambo yake yote.
“Mimi nakataa umasikini na mambo yake yote, nikichaguliwa baadaye mwezi huu, kuanzia Januari hakuna kulipa hata senti moja ya ada, michango sijui ya maabara na nini, haitakuwapo. Mambo ya walimu yamecheleweshwa, sitaki kusikia wakiwa na malalamiko, nataka mambo yaende bambam, yaani yaende vizuri,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye jana alianza hotuba yake kwa kuwataka wananchi wasimame kwa dakika moja kumwombea Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki miaka 16 iliyopita, alisema kuondoa umasikini nchini ndiyo kiu ya Watanzania.
“Nataka kilimo kiwe cha kibiashara, sasa hivi mkulima anapanda, anapalilia hakuna anayemgusa, akianza kuvuna anaanza kuwekewa mageti, vikwazo, hivi vyote nitaviondoa wakulima wawe huru.
“Kwenye elimu ili utoe elimu bora na bure, unahitaji shilingi trilioni 1.4, lakini mwaka jana wamesamehe ushuru wa shilingi trilioni 1.6 na ukiweka fedha hizo kwenye elimu, kazi kwisha kwa sababu elimu ndiyo kila kitu.
“Tumesema tutatoa elimu bure na bora, tukihudumia elimu vizuri Taifa litakuwa bora. Siku hizi ukipeleka mtoto wa Tanzania nje ya nchi anapata sifuri, sasa mimi nataka watoto wetu waweze kushindana,” alisema.
Ampongeza Mwapachu
Katika hotuba yake hiyo, Lowassa alimpongeza Balozi Juma Mwapachu ambaye juzi alitangaza kuihama CCM na kujiunga na kile alichosema ni wana mabadiliko.
“Balozi Mwapachu ni msomi na mwanadiplomasia, kama yeye amehamia kwetu wengine waliobaki huko pia waje,” alisema Lowassa.
Akimzungumzia mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, Lowassa alimwita mwanabadiliko wa kweli kwani wakati CCM inatoka kwenye mfumo wa ubepari kwenda katika mfumo wa ujamaa, msemaji mkuu alikuwa Kingunge.
Kingunge
Akihutubia wananchi hao, Kingunge ambaye amekuwa mwanachama wa CCM na TANU kwa zaidi ya miaka 50, alisema yeye ndiye babu wa vijana wa Tanzania.
“Mimi ndiye babu wa vijana wote Tanzania, ujumbe wangu ni mfupi, huu ni wakati muhimu sana kwa Watanzania wote.
“Tumekaa chini ya uongozi wa chama kimoja, wakati umefika wa kufanya mabadiliko, nusu karne imetosha, uongozi wa sasa wa CCM umeishiwa pumzi, hawawezi tena kuongoza wananchi wa Tanzania,” alisema Kingunge.
“Hakuna zaidi yangu, nimeamua kuachana na CCM na sasa kazi ni moja tu, kuendeleza mabadiliko, kuiweka CCM pembeni ikae kwenye upinzani, wana mapinduzi wa mabadiliko washike usukani,” alisema.
Freeman Mbowe
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, alisema matunda ya kuijenga Chadema kwa muda mrefu yanaonekana sasa kwa viongozi wakubwa walioheshimika kujiunga nao.
“Mmekijenga chama, tumeendelea kusimama kwenye misimamo ya kichama mpaka watu kama Lowassa, Kingunge, Sumaye na wengine wamekuja Chadema, si kwa ajali ni kwa sababu mlijenga taasisi iliyoaminiwa ndani na nje ya nchi.
“Kwa misingi hiyo safari ya matumaini ambayo sasa ni ya uhakika, tumekubaliana kijiti kitashikwa na Lowassa akaikomboe Tanzania,” alisema.
Pamoja na hayo, Mbowe alizungumzia ilani ya Ukawa na kusema inasisitiza upatikanaji wa Katiba mpya aliyosema ilikataliwa na CCM.