Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mbunge wa Bunda Mjini, Eser Bulaya (Chadema), amesema anakusudia kuwasilisha muswada binafsi bungeni kupinga matumizi ya vikokotoo vya pensheni kwa madai kuwa vinamnyonya mfanyakazi.
Akizungumza jijini Dar es salaam leo Jumanne Desemba 4, Bulaya amemtaka waziri husika kujitokeza na kusema kwanini mchakato wa uandaaji vikokotoo hivyo haukuzingatia ushirikishwaji wa wadau.
“Kwanini kumekuwa na malalamiko mengi… waache kutoa majibu mepesi kwenye hoja nzito. Mimi nikishikilia jambo huwa lina ukweli na nilikaa muda mrefu sijaongea nikifanya utafiti wa kina,” amesema Bulaya.
Kuhusu pongezi za Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema zimemuongezea nguvu ya kulishughulikia suala hilo.
“Pongezi za Spika nimezipokea na zimeniongezea kasi ya kukomaa na suala hili hadi dakika ya mwisho… na kufukuzwa bungeni nimezoea,” amesema Bulaya.