29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

TAASISI YA SPE YALETA MAGEUZI MAKUBWA KWENYE NISHATI

NA ASHA BANI

WASIWASI  umetanda kutokana na ongezeko la taka ngumu zinazozalishwa na binadamu hasa katika maeneo ya Viwandani.

Taka hizo zimeelezwa kuwa na athari kubwa kibinadamu hasa kwenye masuala ya afya na za kimazingira.

Waatalamu wengi wamekuwa wakikuna vichwa kufahamu njia sahihi yenye manufaa ambazo zinaweza kuondoa au kupunguza taka .

Kama itakumbukwa kuwa Jiji la Dar es Salaam,limekumbwa na tatizo la kuelemewa kwa taka ikiwa ni pamoja na Halmashauri zote tano eneo kuu la kutupa taka ni Pugu.

Serikali imekuwa ikiumiza kichwa kupata suluhisho la sehemu ya kutupa taka,huku wananchi wanaoishi eneo zinapotupwa taka hizo Pugu huathiriwa na maradhi mbalimbali .

Maradhi hayo ni pamoja na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindu pindu, magonjwa ya ngozi, magonjwa ya saratani (Kansa)  na mengineyo kwa mujibu wa wataalamu.

Mbinu hizo ni pamoja na matumizi ya taka zilizooza ambazo huchakatwa au kurejelezwa na kugeuzwa kuwa nishati.  Taka hizo huweza kuwa mabaki ya chakula na vinyesi vya mifugo au majani yaliyooza kimsingi ni ya ukaa (organic).

 

Thabit Mikidadi Mratibu wa Mradi wa Nishati mbadala, (National Gender and Sustanaible Energy Network) anasema taka ni chanzo kikubwa cha nishati kwa nchi zenye teknolojia sahihi.

Mradi huo unaangalia uwezekano wa kutumia fursa zilizopo ili kuwasaidia wanawake kuondokana na umaskini wa nishati na kuzuia uharibifu wa mazingira.

Anasema wanawake wanatumia nishati duni  kama kuni na mkaa katika kupikia, lakini teknolojia hiyo  inahakikisha kuwa nishati endelevu zinapatikana na nishati hizo haziwaathiri wanawake au watumiaji wengine kwa namna yoyote.

Anasema takataka hasa zile zinazooza kama za vyakula au majani ya miti, huweza kugeuzwa nishati. Kwa mfano, majani ya miti au magome ya miti , husagwa vizuri na kubadilishwa kuwa mkaa. Mkaa huo hauna moshi, huwaka kwa muda mrefu na utasaidia  kuokoa gharama za nishati.

Kadhalika kuna taka za nyumbani, kama nyanya, mbogamboga au vyakula vingine. Anasema taka hizo husagwa na  kuwekwa katika mitambo maalum kisha kuwekwa bakteria ambao huzifanya taka hizo kutengeneza gesi ya ‘biogas’.

Anasema takataka  hutupwa kwenye majalala na husababisha uchafuzi wa mazingira.  Kadhalika anasema uchomaji wa taka hizo hutiririsha maji machafu katika vyanzo vya maji.

Hivyo ili kuepuka uchafuzi huo wa mazingira ni vyema taka hizo zikarejelezwa na kutumika kuleta nishati mbadala.

“Kadhalika taka hizi zikirejeshwa kwa namna zuri katika ardhi, hutumika kama mbolea.  Lakini nishati inayozalishwa na taka hizo ni safi na haina madhara kwa mtumiaji,” anafafanua Mikidadi

Katika mradi huo, Mikidadi anasema  Wilaya ya Mkurunga imetumiwa kama wilaya ya mfano, wakinamama walikusanywa na wakafundishwa kuhusu ujasiriamali wa nishati hizo mbadala.

Wanawake wanafundishwa kutengeneza mkaa unaotokana na magome ya miti na majani na nishati ya gesi inayotokana na taka zilizooza na watatumia mkaa au gesi hiyo kwa matumizi ya nyumbani lakini pia watafaidika na kujiongezea kipato cha kilasiku.

Urejelezaji wa taka unafanyika hata nchini Kenya, eneo la Naivasha. Hili ni eneo la kilimo cha kisasa cha maua pamoja na mbogamboga ambapo mabaki yatokanayo na maua pamoja na mboga  hizo hurejelezwa na kuwa nishati.

Mabaki hayo huchukuliwa na kuwekwa katika mtambo maalum (digester) unaozalisha gesi ya kutosha kiasi cha megawati mbili ambazo hutumika katika shamba hilo na ziada huuzwa kwenye gridi ya taifa.

Baada ya kuchakata gesi, mabaki yake hurudishwa tena ndani ya shamba kwa ajili ya kurutubisha ardhi.

Kadhalika hili limewahi kufanyika nchini Rwanda, ambako  mwaka 2015, tani takribani 300 za taka  zilikusanywa jijini Kigali kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Reuben Ahimbisibwe, Mkurugenzi wa Miundombinu nchini humo alinukuliwa akisema tayari wawekezaji wameonyeshwa dampo lenye taka hizo, likiwamo la Nduba ili kuanza uzalishaji huo ambao utasaidia kupeleka umeme katika gridi ya taifa.

Jinsi  taka zinavyorejelezwa na kuwa nishati

Mikidadi anasema mabaki ya chakula huchukuliwa na kusagwa vizuri katika mashine, kisha huwekwa katika mtungi maalum.

 

Baada ya kuwekwa katika mtungi maalum, bakteria maalum huwekwa, ambao husaidia kuzibadilisha zile taka kuwa mbolea kwa kuvunjavunja molekuli ndani ya takataka.

Katika kile kitendo cha kubadilisha taka hizo kuwa mbolea inazalishwa hewa ya methane. Hewa ya methane ndiyo huzalisha gesi ya kupikia.  Baada taka hizo kubadilishwa kuwa nishati, mabaki hutumika kama mbolea.

Wataalamu wanasema  mabaki yanayopatikana baada ya utengenezaji wa biogas ni mbolea nzuri hasa kwenye bustani na mashamba.

Anasema inaweza kuwa mbolea ya majimaji au kwa kiingereza ´slurry´ na mbolea ngumu, hii ina maanisha, kwa kutumia mfumo wa biogas takataka zinazooza hazitaishia jalalani bali zitarudi kwenye mazingira yetu zikiwa na faida .

Anasema kuna mabaki ambayo hayawezi kuoza, hayo anasema huvunjwa vunjwa  na kutengeneza mkaa  (briquettes) ambao hauna moshi na huwaka kwa muda mrefu.

Mkaa huo hutengenezwa baada ya takataka ngumu kukusanywa na kisha kukaushwa vizuri.

Baada ya hapo huchanganywa na gundi maalum ili kuzipa ubora zaidi wa kushikamana (bonding).

Anaongeza kuwa mkaa huo unawaka vizuri, bila moshi na ni wa bei nafuu kuliko mkaa wa kawaida.

Utunzaji wa misitu na matumizi ya nishati mbadala utasaidia kuweka nchi katika hali salama  kwani itaondosha kuwa jangwa na hata kuzuia mabadiliko ya tabia nchi yasitokee.

Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Januari Makamba ameshafanya mazungumzo na taasisi mbalimbali hasa za serikali kuhakikisha nishati ya gesi ndio itumike katika taasisi hizo.

Alizitaja baadhi ya taasisi ikiwa ni pamoja na mashule, Magereza, majeshi na baadhi ya taasisi zinazotumia nishati ya kuni kwa sasa  na kwamba itapunguza matumizi ya rasilimali za misitu ikiwa ni pamoja na kuni na kuhamia kwenye nishati mbadala kama vile nishati ya gesi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles