31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

YA MAKONDA, GWAJIMA NA TAMTHILIA YA ‘SKENDO’

MAREKANI, kuna tamthilia moja ambayo imepata umaarufu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni, inaitwa Scandal.  Ni tamthilia ambayo inazungumzia mikasa ya kisiasa ya Marekani, ikiwa na wahusika mbalimbali kama vile Rais wa Marekani mwenyewe, Makamu wa Rais, Mke wa Rais, Katibu Kiongozi na Msemaji wa Ikulu.

Nyota wa tamthilia hiyo ni Mwanadada Kerry Washington, ambaye alisaidia kumuingiza Rais madarakani, lakini baadaye akaamua kuiacha kazi aliyokuwa nayo ikulu na kufungua ofisi yake mwenyewe, ambayo inahusika na “kuwasafisha” watu.

Kwa kifupi, Kerry Washington, anayeigiza kama Olivia Pope, anajulikana katika viunga vya Washington kama “fixer” Watu wenye majina yao na vyeo vyao na pesa zao wanapopatwa na matatizo, ama kashfa mbalimbali, humwendea Olivia Pope kwa ajili ya kuwasaidia waondokane na kashfa hizo. 

Na Olivia ni mzuri sana katika kazi yake: Aidha atamsafisha huyo mtu mwenye kashfa, au atampa ushauri mzuri kabisa wa kuueleza umma ukweli na kisha kupanga mikakati ya namna ya kuufanya umma uuchukue ule ukweli, uukumbatie na hatimaye kuukubali, hata kama ulikuwa mbaya kiasi gani.  Yaani kwa kifupi, anakushauri useme ukweli, kisha anakusaidia kuyatengeneza upya maisha yako na umma hatimaye unakukubali na kukusamehe dhambi zako zote.

Leo nimeamua nianze kuizungumzia tamthilia ya Scandal kutokana na kinachoendelea nchini.  Wiki kadhaa zilizopita nilisema kwamba sitaingilia mgogoro ulio dhahiri kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.  Nimeamua nibadilike na kulisemea kidogo, maana hali inakoelekea sasa, ni mbaya.

 

Sisi watazamaji na wasikilizaji hatukuwahi kujua kwamba kuna msuguano baina ya wawili hao.  Hata hivyo, baada ya Mkuu wa Mkoa kutaja majina ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na dawa za kulevya na jina la Askofu Gwajima kuwa mojawapo na Askofu huyo kulala ndani, hapo ndipo tulipoanza kusikia mengine ambayo hatukuyafahamu.

 

Hapo ndipo sisi wengine tulipoanza kulisikia jina la Daudi Bashite na kufahamu kwamba kumbe kuna eneo Tanzania linaloitwa Koromije.  Baada ya pale, Mkuu wa Mkoa akajipeleka kwenye makanisa kadhaa na kuonekana kama analia, huku wengine tukijiuliza anacholilia hasa nini nini. 

 

Baada ya pale, zikaanza kusambaa video kupitia mitandao ya jamii zikimwonyesha mama mmoja akiwa amebeba mtoto, akidai kwamba amezaa na Askofu Gwajima kwa hiari yake mwenyewe na kwamba Askofu huyo hasaidii matunzo ya mtoto.  Baada ya hilo, wengi tulikuwa na hamu ya kujua majibu ya Askofu yatakuwaje na hapo ndipo alipoeleza kwa kirefu Jumapili iliyopita, kwamba mama huyo alidanganya baada ya kuambiwa kufanya hivyo na Mkuu wa Mkoa.

 

Huenda hayo yote hayakunishangaza sana, lakini kilichonipa maswali mengi na kufanya niamue kuliandikia hili, ni kitendo cha Mkuu wa Mkoa kuonekana akienda kwenye ofisi za Kituo cha Televisheni cha Clouds usiku, kwa dhamira ya kulazimisha habari ya yule mama kurushwa hewani.  Inadaiwa kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Clouds waliokuwapo ofisini hapo walidhalilishwa.  Hayo, ni kwa mujibu wa “mahubiri” ya Askofu Gwajima.

 

Kama hayo ni ya kweli, naomba niseme wazi kwamba imefika hatua, Paul Makonda anatakiwa atafute “fixer” wa kumsaidia, na aachane na hao alionao ambao wanamdanganya na kuendelea kumharibia.  Kama anayafanya kwa kujishauri mwenyewe, basi ifike hatua aombe msaada wa watu ambao ni “strategists” wazuri na afuate ushauri wao, hata kama anaona utamdhalilisha, maana ameshajidhalilisha mwenyewe vya kutosha.

 

Kwanza ieleweke wazi kwamba kuzaa na mtu si kosa la jinai.  Kama kweli mtoto ni wa Askofu Gwajima na hatoi matunzo, basi hilo ni la Ustawi wa Jamii.  Lakini pili, suala wanalolitakia majibu Watanzania si la kukashifiana kati ya Makonda na Gwajima, bali wanataka kujua uhalali wa vyeti vya sekondari vya Paul Makonda.  Kumchafua Gwajima hakuondoi kabisa suala hilo, ambalo kama ni kweli, ni kosa la jinai.

 

Ushauri wangu wa bure kwa Makonda: Tafuta tamthilia ya Scandal uingalie, itakusaidia.  Kama huwezi kunyamaza, tafuta “fixer” kama Olivia Pope na uufuate ushauri wake.  Huu mchezo wa kitoto achana nao.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=c7F3DR2Y2P8[/embedyt]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles