25.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO 7 MUHIMU YA KUZINGATIA KAZINI-1

 NA ATHUMANI MOHAMED

KAWAIDA unapozungumzia maisha huwezi kukwepa mahali pa kazi, maana ni ukweli kwamba huchukua muda mrefu zaidi kwa siku kuliko hata nyumbani.

Nyumbani ni mahali pa kupumzika tu na asubuhi inapofika basi watu huondoka na kwenda kutafuta riziki zao za kila siku. Kwa mantiki hiyo basi, ni vizuri kujadili namna bora kuishi kazini ili kuepuka mikwaruzano, lakini pia ufurahia kazi yako.

Ukishindwa kuishi kazini kwa amani, ni wazi kuwa maisha yako kwa ujumla hayatakuwa na amani, maana muda mwingi zaidi unautumia kazini.

Chukulia kwa mfano mtu anayeishi Gongo la Mboto na kufanya kazi Posta Hhapa Dar es salaam. Mtu huyu itambidi aamke asubuhi na mapema ili awahi usafiri wa kwenda Posta. Hata kama ana gari lake binafsi, lazima awahi kuamka ili aweze kukabiliana na suala la miundombinu mibovu.

Mtu huyu akifika ofisini saa 2 au 3 asubuhi, atalazimika kukaa huko mpaka saa 10 au 11 jioni ambapo ataanza tena safari ya kurudi Gongo la Mboto ambako atafika usiku.

Lazima mahali pa kazi pawe sehemu salama, penye amani na usalama maana muda mwingi unakuwa huko. Yapo mambo mengi ya kuzingatia, lakini nimekuandalia yale ya muhimu zaidi saba.

 1  USHIRIKIANO

Acha kujitenga na wenzako, kuwa mshirika mzuri na wenzako. Kunapotokea tatizo lolote kwa mwenzako na ofisi ikaamua kupitisha mchango usikae pembeni, jitoe.

Wakati mwingine inaweza kuwa jambo la furaha mfano harusi au sherehe nyingine yoyote. Ikiwa ofisi imeamua kwa pamoja kumsaidia mwenzenu ni vizuri ukijitokeza kusaidia.

Inawezekana mwenzako akapata tatizo la kuugua ghafla ofisini, kuwa mstari wa mbele kumsaidia. Kwa kifupi, unapaswa kujitoa kwa hali na mali na kushirikiana nyema na wenzako nawe siku ukipata matatizo, wenzako wawe mstari wa mbele kukusaidia kwa kukumbuka namna nawe ulivyowasaidia.

Waswahili wana msemo wao usemao, Wema hauozi.

 

2 KUWA MBUNIFU

Ubunifu ni silaha muhimu sana mahali pa kazi. Unatakiwa kuwa mbunifu wa kiwango cha juu kazini. Katika kitengo au idara yako, unatakiwa kufanya kazi katika kiwango kizuri.

Ubora wako kazini, utakupa marafik wengi zaidi, lakini pia utajenga uaminifu kwa wakuu wako wa kazi. Ndiyo kusema ubunifu wako, utakujengea heshima, huku ukizidi kuipandisha thamani yako mahali pa kazi.

Kwa kawaida, watu wavivu, wanaowasema wenzao zaidi badala ya kuchapa kazi huwa hawana marafiki na huishi kwa hofu ya kufukuzwa kazi akati wowote.

 

3 HESHIMU BILA KUBAGUA

Wapo watu ambao huonyesha heshima kwa mabosi zao pekee, siyo sahihi. Ni kweli mabosi wanapaswa kuwaheshimu lakini usifanye hivyo kinafiki au kwa vile tu ni viongozi wako wa kazi.

Heshimu wote bila kujali vyeo. Heshima yako itakujengea sifa nzuri kazini na bila shaka itakupatia marafiki wengi. Hii ni siri kubwa na muhimu lakini wengi hawaijui.

Ukweli ni kwamba heshima haiigiziki. Unaweza kufanya hivyo kwa kipindi kifupi tu, lakini mwisho wa siku unarudia tabia yako ya awali. Jenga utamaduni huo ndani ya akili yako.

Kwamba heshima ni jambo jema na linalokuongezea sifa ya kuwa mfanyakazi mzuri, anayeshimu wengine bila kuwabagua.

Kwa leo naomba kuishia hapa, wiki ijayo tutamalizia mada hii kwenye sehemu ya pili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles