23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

ACHA TAMAA, JIFUNZE KURIDHIKA – 2

HAPA kwenye Love Talk ya Swaggaz ndani ya Mtanzania Jumamosi ni mahali sahihi kabisa pa kupanuana mawazo kuhusu maisha na mapenzi. Ukiwa mdau wa ukurasa huu utaendelea kuimarisha uhusiano wako siku hadi siku.

Napokea pongezi zenu wasomaji, mlizonitumia baada ya makala ya utangulizi wiki iliyopita. Zimenipa moyo sana. Naahidi kuboresha zaidi ili mpate kitu kizuri zaidi na uhusiano uwe wenye afya na amani.

Marafiki zangu, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza tofauti iliyopo kati ya urafiki au uchumba na ndoa. Mapenzi yale ya urafiki ni tofauti kabisa na kuwa ndani ya ndoa. Kwenye uchumba kuna mambo ya kufurahisha zaidi, lengo kuu huwa kupeana raha na starehe za hapa na pale.

Marafiki, mnapoingia kwenye ndoa, mapenzi yapo tena yanakuwa na nguvu zaidi lakini kuna vitu kidogo vinabadilika. Hata kama ukiona mwenzako kuna vitu hakufanyii, usikasirike, angalia yale ya msingi zaidi kama anakupatia.

Si rahisi akakupa kila kitu, ridhika naye kwa kuwa moyoni umewekeza upendo wako. Vipengele vifuatavyo, vinafafanua zaidi.

 

HAKUNA RUFAA

Kwanza kabisa unatakiwa kufahamu kwamba, hakuna rufaa katika ndoa. Ukishaingia umeingia. Ni vizuri kuwa mtulivu na kuangalia zaidi mambo ya msingi.

Achana na fikra mbaya kwa mwenzako, wekeza upendo wako kwake. Mwamini na ishi naye kwa akili huku ukijaribu kumshauri mambo mbalimbali ya maisha yenu.

 

FURAHA YA NDOA

Yapo mambo mengi ya muhimu kwenye ndoa, lakini jambo kubwa na la msingi zaidi ni pamoja na tendo la ndoa. Lazima wanandoa wawe na uhakika wa kupata tendo la ndoa.

Tendo lenyewe linatakiwa kufanyika vizuri na kwa usahihi. Siyo harakaharaka bila ubunifu. Kufanya hivyo ni kuacha mianya ya mmoja wenu kufikiria kutoka nje ya ndoa.

 

FAMILIA

Majukumu ya familia ni kati ya mambo yanayozidisha furaha ya ndoa. Kama wanandoa wanakuwa makini kuhakikisha familia inakuwa yenye furaha ni jambo zuri.

Lazima watoto wapatiwe elimu bora, uhakika wa lishe, malazi na mambo mengine kama hayo bila kusahau malezi mazuri ya kiimani.

 

MIPANGO YA BAADAYE

Maisha ni mipango, hamuwezi kufikiria starehe tena kama ilivyokuwa kwenye uchumba. Kwenye muunganiko wa ndoa kuna suala la maendeleo na mipango ya baadaye.

Hapo mnatakiwa kuwaweka watoto wenu mbele, maana lazima wawe na akiba yao ambayo mtawaachia. Lazima mfikirie kuhusu rasilimali kwa ajili yao.

 

KUJALIANA

Kila mmoja anaweza kukutana na changamoto kwa wakati wake. Kuna suala la matatizo kazini au msongo wa mawazo. Majukumu ya familia ya upande mmoja au ndugu wa mwenzako.

Mambo kama hayo mkishirikiana kuyatatua huongeza mapenzi ya dhati. Kwa mfano, mmoja wenu anaweza kuugua. Ni jambo zuri sasa kuwa karibu naye na kumpa furaha ili ajione yupo na chaguo lililo kamili.

Maisha ni zaidi ya starehe za kawaida. Majukumu ya familia ni muhimu zaidi kuliko yale mahaba ya mwanzo. Huu ni ukweli ambao wanandoa wengi (hasa wanawake) wanaukimbia.

Kama ulikuwa na mawazo hayo, yaondoe. Sasa weka kitu kipya kichwani mwako. Nashukuru sana kwa kunisoma.

Wiki ijayo nitakuwa hapa na mada nyingine, USIKOSE!

Je, ungependa kujiunga katika group letu la LOVE MOMENT katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwa masomo zaidi? Kama ndivyo andika ujumbe inbox ya namba yangu hapo juu, tutakunganisha ukutane na marafiki wengi na ujifunze zaidi kuhusu uhusiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles