Na RAYMOND MINJA- IRINGA
NINALIONA anguko la mtu huyu anayejiita mtumishi wa Mungu Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, GRC, Antony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako. Napata mashaka kidogo na huyo Mungu anayemwabudu ila nachelea kusema maana nyakati zitasema na hapo ndipo tutakapogundua Mungu wa kweli anayemwabudu.
Kwa wale Wakristo wenzangu na mimi wanaoisoma Biblia kuna maandiko yanayosema; “usihukumu usijekuhukumiwa.” Nashindwa kufahamu mtumishi huyu wa Mungu anapata wapi ujasiri wa kuhukumu hapa duniani ili hali anatumia Biblia takatifu inayokataza kuhukumu.
Mzee huyu wa upako hivi karibuni ameropoka ibadani na kudai “waandishi wote wa habari wanaonichafua na kudai nakunywa pombe watakufa kabla ya mwezi Machi, 2017 na kwamba wasipokufa nitaacha kuhubiri injili, nitaenda kuuza gongo.”
Lusekelo aliyezaliwa Mkoa wa Iringa zaidi ya mika 40 iliyopita, alikwenda mbali zaidi na kudai; “wajue wameingia choo cha kike. Mimi nina nguvu ndio maana hata Rais Magufuli alizijua nguvu hizo ndio maana alikuja hapa ibadani kwangu. Watashindanaaaa lakini hawatashinda.” Hahahahaha!!
Licha ya kwamba taarifa za mtumishi huyo kutumia kilevi zilikuwa mitaani lakini ukweli ni kwamba waandishi wa habari ndio wa kwanza kuibua “ulevi” wa Lusekelo hadharani na mwandishi wa kwanza alikuwa Happy Katabazi ambaye ndiye alimsaidia Mzee huyu asidhalilike siku alipokuwa akiwaporomoshea matusi mazito majirani zake alfajiri akiwa pekupeku akitokea huko alikokuita “ibadani” na kumsihi aingie ndani na aachane na matusi kwani anajiaibisha mbele ya jamii inayomzunguka.
Katabazi ndiye mwandishi wa kwanza kuandika kwa makini na akiwa na kila aina ya ushahidi wa “ugimbi” aliokuwa amegida mtumishi huyu wa Mungu uliokata mishipa ya aibu kichwani mwake na kuanza kuporomosha matusi yasiyokuwa na idadi na yasiyoandikika gazetini.
Baadaye Mzee Lusekelo alikubali kuingia ndani akimwambia Happy, “ahsante dada, ninaingia ndani kwa heshima yako lakini hawa watu ni wapumbavu sana, washenzi na nitawa….”.
Lusekelo baadaye alishikiliwa na polisi kwa kosa la kuhatarisha amani kwa majirani na wapita njia baada ya kusimamisha gari katika barabara nyembamba na kusababisha watu wengine kushindwa kupita alfajiri hiyo kuelekea katika majukumu yao ya kujenga taifa.
Hivyo anaposema waandishi “wanaomchafua” watakufa kabla ya Machi, 2017 ni kwamba anahukumu ili hali kitabu cha Mungu kinakataza kuhukumu na msiba wa kwanza kuupokea basi utakuwa ni wa dada Happy Katabazi na ndipo waandishi wengine wa magazeti ya Tanzania Daima, Mtanzania, Nipashe, Jambo Leo, Majira na Mwanachi watafuata. Habari haiwezi kutoka bila kuhaririwa na mhariri mwandamizi.
Hii maana yake tasnia yahabari inatarajiwa kupatwa na misiba sawa na wagonjwa wa kipindupindu maana “deadline” ya vifo vyao ni fupi mno. Februari 28, Jumanne 2017 saa 6:00 usiku.
Kaka Tony, naomba nikumbushe kuwa wewe ulizaliwa hapa mkoni Iringa miaka zaidi ya 40 iliyopita, umekulia Iringa umesomea Iringa na mambo hayo ya uchungaji pia ulianzia Iringa.
Kipindi hicho unaanza huduma ya kumtumikia Mungu, wakati huo hapa Iringa kulikuwa na makanisa mawili ya Kipentekoste, moja lilikuwa pale Mwembetogwa la Askofu mstaafu Amulike Mboya na lingine la TAG (Tanzania Assembles of God) pale kwa Askofu Mkane.
Katika moja ya nukuu zako unasema kuwa “wakati mimi naokoka, Kanisa la TAG lilikuwa na mgogoro mkubwa pale Iringa kati ya miaka ya 1970 na 1980”.
“Nilipopata wito wa kumtumikia Mungu, mimi nikaangukia upande wa Moses Kulola (marehemu). Unajua pale Iringa kulikuwa na upande wa Lazaro na Kulola hivyo mimi nikaangukia kwa Kulola.”
Kaka yangu Lusekelo umepeleka wapi busara alizokuachia baba yetu Kulola, umepeleka wapi hekima alizokuwa nazo mzee wetu Kulola, hivi leo hii unathubutu kusimama na kusema ulikuwa muumini mzuri wa mzee Kulola, aliyetangulia mbele ya haki huku nyuma akiacha heshima kubwa katika makanisa aliyoyaanzisha.
Hivi unaweza kusimama na kusema wewe ni zao la mzee Kulola “mzee huyu aliyetembea usiku na mchana kuhubiri neno la Mungu aliye hai, aliyezunguka Tanzania nzima akifungua makanisa na kuhubiria amani na upendo huku akitaka watu wamrudie Mungu na kuwasamehe walio waliowakosea.
Wewe ni kitabu gani unachotumia kuhukumu waandishi wa habari, angalia Yesu alipokuwa pale msalabani licha ya kupigwa na kuteswa na kusulibiwa lakini alisema: “Baba wasamehe hawa maana hawajui walitendalo” wewe leo hii umeguswa kidogo unasema “baba waue hawa la sivyo nitakwenda kuuza gongo” ni kitabu gani unachotumia wewe katika kulitangaza neno la Mungu lenye maneno hayo.
Hakika narudia kusema napata shaka na Mungu unayemwabudu, hata mafundisho yako wakati mwingine huwa yanaacha watu njiapanda maana kuna baadhi ya mahubiri yako unasema: “Mwanamke ni sawa na chama cha siasa, kisipokuwa na mpinzani hakiwezi kuimarika” ina maana unataka Wakristo wawe na wake wawili??
Malipo ya mwanadamu wakati mwingine ni hapa hapa duniani, hakika umekanyaga patakatifu bila kuvua viatu, umenajisi hekalu na bahati mbaya umemchokoza Mungu tarajia majibu.
Huwezi kuwatishia maisha wanahabari wanaotekeleza majukumu yao, busara za mzee Kulola na roho wa Mungu angekutuma kukaa kimya au kujibu hoja za Happy kwa hoja, lakini si vitisho vya kuwaua kabla ya Machi 2017.
Kaka Lusekelo usilolijua ni kwamba waandishi wa Tanzania ni ndugu, jamaa, marafi na ni wamoja mno hasa linapokuja suala linalogusa masilahi yao na pia wanamjua Mungu wa kweli.
Umegusa uhai wao. Tegemea nguvu ya umoja wao huo kuwakabili maana kalamu zao tayari wamejaza risasi za kila aina. Sidhani kama utaweza kushinda vita hii maana unaposema, “watashindana lakini hawatashinda” tulidhani ni vita ya kiroho kumbe ni vita ya nyama, jasho na damu?
Lusekelo nani kakudanganya kuwa unaweza kuwanyamazisha waandishi na kuwatishia kifo? Kwani wewe hutakufa? Lusekelo umelewa nini, konyagi, sadaka au Roho Mtakatifu? Maana vyote hulevya kama bhangi au shisha! Lusekelo umeudhi mno tasnia ya habari nchini Tanzania.
Nikwambie tu kaka yangu watumishi wa Mungu huwa hawapigani vita ya damu na nyama bali hupigana vita vya kiroho na dhambi hiyo kama unaitenda haitakuacha kamwe mpaka pale utakapotubu.
Ninaamini wandishi wa habari wa Tanzania hawatakufa kwa matakwa yako wala matakwa ya binadamu yeyote bali kwa matakwa ya Mungu, maana tuna Mungu aliye hai tunayemwabudu na kumtumikia, hata hivyo nami nasubiri maono yako yapate kutimia.