33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

NANI MKWELI DANGOTE NA SERIKALI?

Aliko Dangote
Aliko Dangote

Na MARKUS MPANGALA,

SAKATA la kusitishwa uzalishaji wa saruji katika Kiwanda cha Dangote mkoani Mtwara limezua malalamiko makubwa dhidi ya Serikali, huku yenyewe ikijitetea. Taarifa rasmi ya kiwanda cha Dangote inalalamikia gharama kubwa za uendeshaji na uzalishaji wa saruji.

Taarifa ya Kiwanda cha Dangote iliyomkariri Ofisa Mtendaji Mkuu, Harpreet Duggal, imeeleza mambo makubwa matatu.

Kwanza wametoa taarifa juu ya hitilafu ya kiufundi (ubovu wa mitambo) katika mitambo ya kiwanda hicho, lakini hawajasema mitambo hiyo ni mipya au chakavu.

Pili, taarifa hiyo imeeleza gharama kubwa za uzalishaji wa saruji hapa nchini kulinganisha na nchi nyingine 16 ambako wanazalisha saruji gharama ndogo. Kwanini  hatujaambiwa gharama halisi ni kiasi gani kati ya kiwanda cha Dangote na vingine kama vya Cameroon au Zambia?

Tatu, taarifa hiyo ilieleza inatumia jenereta inayotegemea mafuta ya dizeli kuendesha uzalishaji wa saruji kiwandani hapo. Kwa maana hiyo tunaambiwa kiwanda cha Dangote hakijapata umeme wa Tanesco.

Nne, taarifa ya kiwanda cha Dangote inasema kuwa soko kuu la simenti lipo mbali, hali ambayo inaongeza gharama kwa kiwanda hicho. Ndiyo kusema wateja wengi wa saruji ya Dangote hawapo Mtwara wala kanda ya kusini. Kwa mantiki hiyo, wateja wao wapo Dar es Salaam kama mji mkubwa kibiashara au maeneo gani ambayo yanauzwa zaidi saruji hiyo na kiasi gani tangu wameanza kuzalisha?

Tano, tunafahamu ujenzi wa viwanda huambatana na utafiti wa kina kokote duniani. Hakuna mwekezaji anayejenga kiwanda mahali fulani bila kuangalia namna ya kuendesha, soko kuu na mazingira yake kwa ujumla. Ni kwanini mwekezaji aliamua kwenda kujenga kiwanda mkoani Mtwara, kisha anakuja kulalamika leo kuwa kiwanda kipo mbali na lilipo soko la saruji?

Tukiachana na suala hilo, tunakuja upande wa utetezi wa Serikali. Tumeambiwa kuwa, Serikali imeamuru kutumia makaa ya mawe yaliyopo hapa nchini, tofauti na mpango wa kiwanda cha Dangote kinachotaka Makaa ya Mawe kutoka Afrika Kusini.

Mawaziri wawili wa Serikali wametoa ufafanuzi wa kusimama uzalishwaji wa simeti wa Kiwanda cha Dangote. Waziri wa Biashara, viwanda na uwekezaji, Charles Mwijage na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, wamejibu sababu zilizotolewa na Dangote.

Baada ya hapo tunaweza sasa kuanza kutafakari kwa pamoja ili kukubaliana ama kupingana na kile kinachosemwa na pande zote mbili.

Kwanza, kulingana na historia ya ujenzi wa viwanda vya saruji vya Dangote, tunafahamu kuwa kati ya mwaka 2014 na 2015 amejenga viwanda vipya katika nchi mbalimbali, zikiwemo Tanzania, Zambia na Cameroon. Hapa nchini kiwanda cha Dangote ni kipya ambacho mitambo yake mingi ni mipya.

Je, ni uharibifu gani mkubwa kiasi hicho umetokea katika kiwanda hiki mpaka kusimamisha uzalishaji au mmiliki alinunua mitambo chakavu na kuanza uzalishaji?

Pili, kwa mujibu wa Waziri Muhongo, tuna hazina ya makaa ya mawe ya kutumia kwa miaka 200 ijayo. Je, ubora wa haya mawe na bei yake kulinganishwa na yale ya nje ukoje? Ni kwanini Waziri Muhongo hajaliambia taifa juu ya ubora huo ili kutatua kadhia ya Dangote?

Tatu, Waziri Muhongo aliviambia vyombo vya habari kuwa Dangote wameweka oda ya makaa ya mawe tani 5,000 katika mgodi wa Ngaka. Je, Dangote hawataki kutumia makaa hayo au Serikali inajaribu kujinasua kwenye makosa yake ya kushindwa kuhudumia wawekezaji?

Serikali ilitakiwa kutoa umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa kwa gharama nafuu. Je, ni kwanini halikutekelezwa hilo hadi mwekezaji ategemee umeme wa jenereta?

Nne, tumeambiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kuwa Dangote itatumia gesi asilia na wataanza kuuziwa Februari 2017. Ni kweli serikali itatekeleza ahadi ikiwa ile ya umeme wa gridi ya taifa wameshindwa?

Tano, taarifa ya Dangote inasema kuwa Serikali inaangalia suala hilo ili kupunguza mzigo. Hii inatuletea mantiki kuwa tunahitaji gesi kuongeza uzalishaji wa saruji katika kiwanda hicho. Je, kuna ugumu gani kutumia gesi kiwandani hapo?

Baada ya kuangalia utetezi wa pande zote mbili, tunaweza kujipatia majibu ya kila namna ili kufikia kukata kiu. Kwanza tunapata jawabu kuwa kama kuna gharama za uendeshaji wa kiwanda cha Dangote, maana yake kuna mikakati ya kupandisha gharama au bei ya uuzaji wa saruji ya kiwanda hicho.

Aidha, Serikali inafahamu fika mikakati hiyo na kwa namna ya kipekee tunaona mchanganyiko wa taarifa kutoka wamiliki wa kiwanda na serikali kwa upande mwingine. Vilevile inafichua makosa ya Serikali ya kuchelewesha ufanisi wa viwanda, lakini inakuwa nyepesi kuwalaumu wawekezaji.

Hatuwezi kuwahukumu Dangote kwamba hataki kutumia makaa ya mawe ya hapa nchini kwakuwa kwenye taarifa yake hakutaja kutotumia makaa hayo kama moja ya sababu ya gharama kubwa.

Msingi mkuu hapa tunaupata kwenye; mahali kilipo kiwanda, soko la saruji na bei ya saruji ya Dangote. Kama mahali kilipo hakuna soko kuu maana yake gharama zinatakiwa kupanda. Kama soko la saruji yake ni zuri lakini gharama za uzalishaji ni kubwa maana yake anataka kupandisha bei.

Saruji ya Dangote ndiyo ilichangia kupungua kwa bei ya saruji hapa nchini, kwa maana hiyo, sasa mambo yamebadilika na gharama inatajwa kuwa kubwa. Ununuzi wa gesi na makaa ya mawe sitarajii kama itakuwa sababu ya kushusha bei ya saruji yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles