24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI BENKI ZINAYUMBA NCHINI

Benki Kuu ya Tanzania
Benki Kuu ya Tanzania

Na MARKUS MPANGALA,

JUNI 7, 2006, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alisaini Sheria namba 5 ya Benki Kuu kuhusu fedha za mashirika ya umma na Taasisi za Serikali.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo, kifungu cha 31 na 32 vinaelekeza mashirika ya umma na taasisi za Serikali kuweka fedha zao katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu.

Licha ya kusainiwa kwa sheria hiyo miaka 10 iliyopita, Rais mstaafu Kikwete hakuthubutu kuchukua uamuzi wa kutekeleza sheria hiyo ili fedha za mashirika ya umma na Taasisi za Serikali ziwekwe Benki Kuu.

Hata hivyo, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imetekeleza sheria hiyo na kuamua kuweka fedha za mashirika ya umma katika akaunti maalumu zilizopo Benki Kuu.

Tangu uamuzi huo ulipochukuliwa kumeibuka manung’uniko kutoka sekta ya benki na biashara ya fedha. Kumezuka manung’uniko kwamba benki zimepoteza sehemu kubwa ya fedha na faida, jambo ambalo linachangia mdororo wa uchumi.

Miongoni mwa benki zilizokumbwa na mtikisiko ni Benki ya Twiga Bancorp, ambayo ipo chini ya uangalizi wa Benki Kuu nchini (BoT).

Taarifa rasmi kutoka benki mbalimbali zinaonyesha kuwa kiwango cha ukopeshaji na urejeshwaji wa mikopo hakiridhishi. Inaelezwa kuwa, baadhi ya benki zimepunguza kiwango cha ukopeshaji kutokana na matatizo ya kiuchumi, yakiwemo ya idadi ndogo ya wakopeshwaji kurudisha mikopo.

Ndiyo kusema kitendo cha serikali kuondoa fedha za mashirika na taasisi zake katika benki za biashara kumesababisha kuyumba kwa baadhi ya benki hizo. Hiyo ikiwa ni tafsiri kuwa benki nyingi za biashara zilikuwa zinategemea zaidi fedha za mashirika na taasisi hizo kuendesha biashara zao; ukopeshaji, uhifadhi na kadhalika.

Je, uamuzi huo ulikuwa sahihi katika uendeshaji wa biashara ya fedha katika benki hizo? Je, utegemezi huo una maana kwamba benki zilishindwa kubuni au hazikuwa na ubunifu mwingine? Kwamba benki za biashara zimewekeza zaidi kwa tabaka la watumishi wa Serikali, Serikali yenyewe na watu wenye mitaji mikubwa ambao ni wachache huku kundi kubwa la wananchi likiendesha shughuli za kifedha bila kutegemea benki?

Maswali mawili ya mwisho ni haya; je, kuna matarajio yoyote ya Serikali kurudisha fedha za mashirika na taasisi zake kwa benki za biashara? Na je, nini kasoro za benki nchini na namna ya kurudi kwenye hali ya kawaida?

Jibu la swali la kwanza linaelezwa na wataalamu wa masuala ya fedha kwamba itakuwa jambo gumu kutokea, na kwamba haitegemewi fedha za mashirika ya umma na taasisi za Serikali kurudishwa benki za biashara kwakuwa Rais Magufuli ametekeleza matakwa ya kisheria.

Katika muktadha huo, ndipo anapoingia Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, ambaye katika andiko lake amependekeza kuwa Rais John Magufuli katika Bunge lijalo la mwaka 2017 apeleke bungeni hati ya dharura ya marekebisho ya Sheria Namba 5 ya Benki Kuu ya mwaka 2006 ili kurekebisha vifungu vya 31 na 32 na vifungu vyake vidogo ili iwe rasmi fedha za mashirika na taasisi za Serikali zibaki Benki Kuu, zisirudi tena benki za biashara.

Pendekezo hilo linatokana na tafsiri ya kisheria ya maneno “May be’ (pengine) yaliyomo kwenye vifungu vya sheria hiyo kwa madai ni laini na yanaifanya sheria isiwe na nguvu zake kwa asilimia 100. Anasema maneno hayo yaondolewe kabisa.

Jibu la swali la pili; je, nini kasoro za benki nchini na namna ya kurudi kwenye hali ya kawaida?

Uchambuzi unaonyesha kuwa, mikopo mingi ya benki ilikuwa ikiangalia wenye vipato vya hali ya juu na dhamana kubwa kuwa wenye vigezo vya kukopeshwa.

Benki zilisahau watu wa chini, vikundi vya akina mama ntilie, vikundi vya wafanyabiashara wadogo wadogo kuwa ndio wanaendesha uchumi wa nchi ngazi ya chini kwa sababu fedha zinazunguka haraka kwao na kurejesha mikopo.

Baadhi ya benki zimekuja na miradi mipya ya mikopo ya nyumba, huku utafiti wa ukopeshaji ukiwa unatiliwa shaka kama unawasaidia wakopaji. Mathalani kuna benki moja (jina linahifadhiwa) ili uweze kupata huo mkopo wa nyumba unatakiwa ujenge hadi upaue ndipo benki hiyo inakuja kukukopesha.

 MBINU MPYA ZA KUKOPESHA, KUREJESHA

 Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya biashara ya fedha na benki, Mussa Elijah Mbuya, amepata kusema benki nyingi zilikosa ubunifu wa namna bora ya kukopesha pamoja na kuvumbua njia mpya, ambayo anaipa jina la ‘The Art of Borrowing’.

Kwamba ukosefu wa ubunifu umechangia kuyumbisha benki mara baada ya fedha za mashirika na taasisi za serikali kuondolewa katika benki za biashara.

“Na ndiyo sababu kubwa kwamba hawashughuliki na masikini kama wamachinga na wajasiriamali wa kiwango cha chini, wapo ‘busy’ na watumishi wa Serikali na wenye mishahara ya uhakika. Hawana muda wa kuunganisha mbinu mpya za ukopeshaji na uwekaji wa akiba kutoka watu masikini, ambao ni wengi. Si zaidi ya Watanzania milioni 15 kati ya milioni 45 wanaotumia akaunti benki. Tumeona M-pesa, Airtel Money, TigoPesa proved them wrong (zimewaumbua) kwamba Watanzania wanaweza kuweka akiba na wanakopesheka,” anasema.

Inaelezwa kuwa, njia mojawapo ambayo ingeweza kutumika ni kukopesha na kurejesha kwa saa, siku, au wiki kupitia namna mpya ya ukopeshaji na urejeshwaji mikopo. “Ninatamani hata kuanzisha workshop za aina hii kwa mameneja wa benki, ili wajue The Art of Borrowing (ujuzi mpya wa kukopesha na kurejesha).”

BENKI SI RAFIKI WA MASKINI

 Kila kona ya nchi hii kumekuwa na fikra hasi dhidi ya benki. Wapo wanaokumbuka maneno ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwamba benki si rafiki wa watu masikini. Lakini sasa hali inadhihirika benki hizo zitawahitaji watu hao kutokana na mdororo uliozikumba. Kupunguza kiwango na idadi ya utoaji wa mikopo maana yake inarudisha nyuma kasi ya ufanisi wa benki husika. Kwa vyovyote vile benki zitapaswa kubadilika kimtazamo kwamba kwa benki za biashara kuegemea biashara zao kwa mzunguko wa pesa za Serikali, kiuchumi haikuwa nzuri.

Benki nyingi zilikuwa zinafaidi fedha za Serikali bila hofu ya kupoteza, na pia uchumi unategemea benki zizungushe fedha kwenye vitega uchumi kama viwanda, miradi ambayo ingeajiri watu.

Badala yake benki ziliishia kutegemea fedha za bure zinazohifadhiwa na taasisi na mashirika ya umma. Hii inaathiri ajira, hali kuwa ngumu, ubunifu na ujasiriamali kuwa wa hali ya chini, woga wa kuthubutu kukopesha na hata kukopa, kwani benki hazina uzoefu huo zaidi ya kutegemea tu amana za Serikali na kukopesha huko serikalini pia kupitia Hazina.

KUBADILI MFUMO WA MIKOPO

Nilimuuliza mshauri wa masuala ya biashara nchini, Gabriel Mwang’onda, kwamba Sheria namba 5 ya Benki Kuu ilipitishwa Juni 7, 2006. Uamuzi wa Rais John Magufuli kupeleka fedha za mashirika ya umma Benki Kuu umetokana na sheria hiyo. Ghafla tumeona sekta ya benki inadorora. Nini udhaifu wa biashara ya benki zetu? Na namna gani zinaweza kurudi mstarini bila fedha ya mashirika ya umma?“Benki zetu nyingi zilikuwa zikitegemea fedha za Serikali na kwa upande wa kukopesha walikuwa hawajali sana vigezo, kitu ambacho kilisababisha NPL (Non Performing Loans) kukua kwa kasi sana, huku wakijiaminisha kuwa hayo madeni yatalipwa, kwahiyo kulikuwa na upotoshwaji mkubwa juu ya kuripoti taarifa za fedha, walikuwa hawatoi ripoti za madeni mabaya, badala yake walikuwa wakionyesha kuwa ni wadaiwa wa kawaida.

Anasema: “Kwa sasa BoT wana mfumo mpya wa udhibiti ambao unazilazimisha benki kuripoti vitabuni vitu katika uhalisia wake. Ndiyo maana benki nyingi zimepunguza kiasi cha faida na benki nyingine zilizokuwa zikitegemea sana fedha zilizokuwa zinawekwa na mashirika ya Serikali katika akaunti zake na baadaye benki zinaripoti hasara.

Anaongeza: “Lakini takwimu zinaonyesha kuwa, Watanzania wanaotumia mabenki si zaidi ya asilimia 10. Hao ni wenye akaunti na humo humo kuna wasiozitumia, na zisizowekwa au kutolewa fedha. Ujio wa ‘mobile money’ (huduma za fedha kwa njia ya simu za viganjani) umeleta shida zaidi.

“Kwahiyo, sasa ni kazi za benki kubadili mfumo wa ufanyaji biashara kutoka kwenye njia za kawaida za kiasili hadi kwenye matumizi ya teknolojia ili kukabiliana na ubunifu wa huduma za kifedha za simu za viganjani, pamoja na kushawishi umma kuwa benki ni sehemu sahihi na watumie hizo.

“Hatua zilizochukuliwa na Serikali Si mbaya, ni serikali nyingi tu hufanya hivyo. Hapa ni suala la hizi benki zaidi ya 53 tulizonazo kuwa wabunifu kuja na bidhaa adimu katika soko,” anasema Mwang’onda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles