27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DHAMBI YA KURUDI NA VYETI INATAFUNA TAIFA

Muhitimu akipokea cheti
Muhitimu akipokea cheti

Na RATIFA BARANYIKWA,

KUNA mambo yanatokea katika Taifa hili, ambayo yamenifanya nianze kuwaelewa wale waliopata kusema kwamba, juhudi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutukomboa kifikra kwa njia ya elimu ziligonga mwamba baada ya wale waliopelekwa kutafuta elimu katika pande mbalimbali za dunia kwenda kupambana na mitihani, matokeo yake wakarudi na vyeti bila fikra.

Mwenendo huo wa kupambana na mitihani badala ya utumwa wa fikra ndio unaotajwa na baadhi kuwa ni kiini cha wasomi wengi leo hii kugeuka tishio dhidi ya rasilimali na maendeleo yetu.

Leo hii kwa sababu ya baadhi ya taasisi kuongozwa na ‘wasomi vyeti’, wamejikuta wakitengeneza matatizo zaidi badala ya kuyatatua.

Ipo imani kwamba, hadi Mwalimu Nyerere anaaga dunia mwaka 1999, alikuwa ametuachia uhuru wa bendera tu na si ule wa fikra, ambao kwa bahati mbaya licha ya kuupigania kwa nguvu zote, lakini tulimwangusha.

Lakini wapo wanaolaumu warithi wake kwamba walishindwa kutekeleza dhana hiyo kwa kuwanyima Watanzania fursa ya kupata elimu inayohitajika.

Wanawalaumu kwa kufurahia maua ya vyeti na si kuweka mazingira ya kuwapatia Watanzania elimu yenye ubora ambayo itazalisha wasomi kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo katika jamii.

Dhana ya Mwalimu Nyerere ya ukombozi wa fikra, babu na bibi zetu, baba na mama zetu, kaka na dada zetu walishindwa kuitekeleza ipasavyo na ndiyo maana leo hii wapo wanaoamini kwamba, Watanzania wameendelea kuishi utumwani.

Kwa sababu hiyo, uhuru mkubwa kabisa tunaojivunia Watanzania leo hii ni kuwa na baadhi ya viongozi wanaofanya uamuzi kwa kumpendezesha fulani kwa sababu tu alimtoa kwenye kiofisi kimoja na akampatia kiofisi maslahi kingine au fulana na pombe kidogo.

Watu waliokwenda kutafuta fikra wanasema sehemu kubwa ya Watanzania, wakiwemo wale wenye vyeti, tuna uwezo duni wa kupambanua mambo na hivyo kuhitaji msaada katika kila jambo tunalotaka kulifanyia maamuzi.

Wanasema mwenendo huu umeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo yetu ya maisha ya kila siku.

Wanasema hata wale wachache ambao walirudi na fikra kasi yao ya kuwaambukiza wengine imekuwa ni ndogo kwa sababu wamegundua kuna makundi hatari ambayo yamekubali kuwa watumwa wa fikra na kwamba wao wanachoangalia ni kutunza hazina zao na kuangalia namna ya kuendelea kufaidi matunda ya nchi yao.

Miongoni mwa viongozi wa namna hii wapo wenye elimu kubwa, wengine ni madaktari wa falsafa, lakini utagundua kwamba, wanaishi katika fikra za kitumwa kupitia maamuzi yao yanayoongozwa kwa husda, chuki au kumbeba mtu fulani kwa maslahi yake.

Kitendo cha kupindishapindisha mambo ya uongo kutaka wayafanye yaonekane ni ukweli kwa sababu ya maslahi binafsi na si ya nchi ni ishara ya kwamba, wale tuliowapa mamlaka kutusimamia baadhi yao ni watumwa wa fikra.

Kutekeleza sheria kama kasuku, kutumia rasilimali zetu vibaya, kuleta wawekezaji matapeli na wezi wa rasilimali zetu ni udumavu wa fikra.

Kushangilia baadhi ya viongozi laghai ambao wake zao, ndugu na jamaa kwao ni mwiko kulipa kodi hata kama ni kontena nne tu ni umaskini wa fikra.

Kulamba miguu ya wanyang’anyi wa rasilimali zetu, kumsujudia mtu aliyesababisha maisha duni karibu kwa kila Mtanzania, vijana kukosa ajira, elimu kuyumba, mazao kukosa soko, hospitali kukosa dawa, vifaa nk ni upofu wa fikra.

Ameandika Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole kupitia akaunti yake ya Twitter kuwa: “Siku hadi siku namuelewa mfalme Suleiman kwanini hakuomba mali bali hekima na maarifa”.

Polepole amekwenda mbali na kusema; “Uongozi mtihani mkubwa kabisa ni humbleness au Kiswahili kujishusha wakati mwingine kwa maslahi ya umma una swallow pride yao”.

Leo hii kwa sababu ya kupambana na kutafuta vyeti, Taifa limejikuta lina viongozi wachache sana waliobahatika kutafuta fikra na ambao wanaweza kuona mambo kwa uhalisia wake.

Viongozi wa aina hii utawagundua kupitia matendo na maamuzi yao yasiyozingatia mioyo, bali kichwa.

Utawagundua kwa hekima, maarifa na kujishusha kwao, ni viongozi wachache sana ambao wanaweza kuendesha taasisi walizopewa kuzisimamia pasipo kufanyia kazi fitna, majungu, chuki na visasi.

Ni wachache mno ambao wanaweza kuunda timu ili kutoa maana halisi ya maisha.

Nimalizie kwa kusema, tunahitaji kujikomboa sisi wenyewe kifikra, tusiende shule kutafuta vyeti.

Bila fikra huru tutaendelea kushuhudia watawala dhalimu wakidhalilisha rasilimali na taifa letu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles