24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAAMINI SERIKALI ITATATUA SUALA LA DANGOTE KWA HEKIMA NA BUSARA

Kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited Tanzania
Kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited Tanzania

MOJA ya habari kubwa iliyoibuka wiki hii na pengine kuibua mijadala mizito na maswali magumu, ambayo bado tunadhani hayajapata majibu ya kuridhisha, ni hatua ya kiwanda cha kuzalisha saruji kinachomilikiwa na bilionea namba moja Afrika, Aliko Dangote, kusitisha uzalishaji.

Licha ya kiwanda hicho kueleza sababu ya kuchukua uamuzi huo, kuwa ilitokana na hitilafu za kiufundi katika mitambo yake, lakini majibu kutoka taasisi za Serikali kama Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Shirika la Maendeleo ya Petroli yaliibua mambo mengi mapya.

Katika majibu yao, taasisi hizo zilikishutumu kiwanda hicho kwa kukataa kutumia makaa ya mawe ya hapa nchini na kutaka kutumia yale ya Afrika Kusini, ambayo wanadai yana nafuu kwao kwa maana ya gharama na ubora.

Si hilo tu, pia zilikishutumu kiwanda hicho kutaka kuuziwa gesi kwa bei ya kutupa.

Katikati ya mjadala huo, liliibuka suala la vivutio vya uwekezaji ambavyo Dangote aliahidiwa.

Taarifa zimewakariri watendaji wa kiwanda hicho, wakiilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwapa mafuta kwa bei rahisi. Kwa mwezi wanadai kutumia dola milioni nne sawa na Sh bil 8.7.

Mbali na hilo la mafuta, pia wanalalamika kwa kushindwa kutimiziwa ahadi nyingine walizokubaliana.

Kwetu sisi, mzozo huu umetukumbusha kile tulichopata kukiandika siku za nyuma, juu ya umuhimu wa kuweka wazi mikataba ya wawekezaji.

Tunaamini kama mambo yote yanayokigusa Kiwanda cha Dangote yangewekwa sawa sawa, tusingeshuhudia mvutano wa aibu ulioibuka.

Hatutaki kuamini moja kwa moja kama Dangote kuna vitu alifanya kimya kimya, na kama alifanya hivyo, basi atambue kwamba nchi yetu haitaki mambo hasi.

Tukiwa tunaamini kwamba ipo mikataba inayopaswa kuwa wazi na mingine kwa sababu ya unyeti wake haipaswi kuwekwa wazi, lakini ukweli ni kwamba jambo hili bado halijaweza kutekelezwa ipasavyo kwa masilahi ya Taifa.

Leo hii nchi yetu imejikuta ni mhanga mkubwa kwa sababu ya mikataba ya ubabaishaji, kwani ndiko mapato mengi yanakopotea na kusababisha miradi ya maendeleo inayohudumia wananchi wengi kukwama ama kutotelekezwa.

Pamoja na yote yaliyojitokeza, hasa katika suala hili la Dangote, Serikali bado inayo nafasi kubwa ya kutafuta suluhu kwa kutumia hekima na busara wakati huo huo ikizingatia masilahi ya taifa.

Katika njia hizo hizo za hekima na busara, Dangote asikilizwe, kwani na yeye tunaamini pamoja na kuwa ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa Afrika na pengine duniani, anaelewa madhila yanayowakumba Waafrika wenzake, hasa kwenye suala la rasilimali zao ambazo zimekuwa zikipokwa na wajanja wachache.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles