26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA DANGOTE LAFICHUA SIRI NZITO

aliko-dangote

NA EVANS MAGEGE

SAKATA la Kiwanda cha Saruji cha Dangote kusitisha uzalishaji wa bidhaa hiyo sasa limechukua sura mpya, baada ya kubainika kuwa msingi wake umechochewa na vita inayopiganwa dhidi yake na washindani wake kibiashara.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata na ambazo zimethibitishwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, zinaeleza kwamba, hasira za washindani wake kibiashara zimechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea uamuzi wa kiwanda hicho kusitisha kwa muda uzalishaji.

Dodoso lililofanywa na timu ya gazeti hili, limebaini kuwa nyuma ya makampuni hayo ya washindani yamo ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Mwijage naye alikiri  kufahamu jambo hilo na akasema kuna watu wenye hasira zao za kibiashara wametumia mwanya huo kusambaza taarifa hasi dhidi ya mwenendo wa uwekezaji wa Dangote hapa nchini.

Mwijage alikwenda mbali na kusema hata uamuzi wa Kiwanda cha Dangote kusitisha uzalishaji kwa muda ili kupisha matengenezo limekuzwa kwa namna hiyo hiyo.

“Tatizo ni kwamba, hili suala linakuzwa mno na watu wengine wana hasira na watu  wao wanataka  wawapige kupitia kwenye suala hili…actually mimi najiingiza kwenye ugomvi wa watu wengine, mimi sina tatizo na mtu lakini wanaopigana. Nawajua kwamba wanamlenga fulani, kwa hiyo mimi najiingiza tu kutuliza temperature (joto).

“Kuna watu wana visa vyao huko wanapigana, sasa mimi naingia katikati ili kutuliza mvutano, kwa sababu mchezo wao si mzuri kwa industry (sekta ya viwanda),” alisema Mwijage, pasipo kuwataja hao walioingia katika vita hiyo.

Wakati Mwijage akisema hayo, Mfanyabiashara wa saruji ya Dangote, aliyepiga simu chumba cha habari cha gazeti hili akijitambulisha kwa jina la Khalfan Ali, naye alieleza jinsi ambavyo amekuwa akipata ugumu wa kusafirisha bidhaa hiyo hadi kufika eneo lake la kazi, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa wakala huyo, gari za Dangote za tani 30 zimekuwa zikizuiwa kuwapelekea saruji katika maeneo yao kwa kile kinachoelezwa kuwa barabara wanazozitumia si za Tanroad.

“Huu mzigo tunautoa Mtwara hadi Dar es Salaam, lakini cha ajabu wanasema tusishushe kwa sababu barabara tunazotumia si za Tanroad, ambazo hazina uwezo wa kupokea  gari la tani 30, barabara zenyewe ni za vumbi lakini wanatuzuia.”

Mfanyabiashara huyo, ambaye kwa mwezi anauza tani zaidi ya 60 za saruji ya Dangote, alisema anadhani suala lililoibuka sasa limechochewa na mambo mengi kuliko yale ambayo yanazungumzwa.

“Nimemsikia Waziri leo (jana) anasema hili suala tuwaachie wao, sisi wananchi tunyamaze, naomba Serikali iwe wazi, ajira zinapotea, hali mbaya, wale waliokuwa viunganishi wetu katika biashara hii sasa hivi hawapokei hata simu…haiwezekani mtu atoke Nigeria kote huko aje awekeze hapa halafu tumchezee,” alisema Ali.

Wakati mfanyabiashara huyo akisema hayo, kwa upande wake Waziri Mwijage alikwenda mbali na kuitaja nchi jirani ya Kenya kuwa nayo imeingia katika vita hiyo.

Alisema alishtukia hilo baada ya kuona baadhi wakisherehekea mvutano uliojitokeza kupitia mitandao.

“Ukisoma mitandao ya Kenya wanasherehekea hizi habari tunazozungumza sisi, mimi hili suala nilikuwa nimelisusia, halikuanza jana, lilianza juzi, lakini nimeingilia baada ya kuanza kuona mitandao ya Kenya imeanza kuingilia kati.

“Ndiyo maana nikatamka kwamba nitawaacha kondoo 99 nimfuate mmoja, nilisema hiyo kauli, maana ya kuisema hivyo ni kwamba niliona watu wa Kenya wameanza kushabikia hili suala la Dangote,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwijage, Dangote  amemuandikia barua inayoeleza sababu ya kuzima mitambo kwamba ni matatizo ya kiufundi.

Alipoulizwa sababu za Wakenya kushabikia sakata hilo, Mwijage alisema Tanzania ni soko la Kenya, hivyo ujenzi wa viwanda nchini unawanyima ulaji.

“Unajua sisi ni soko la Kenya, kwa hiyo mnapojenga viwanda, Wakenya wanasikitika kwa sababu wangependa muendelee kuwa soko… na ujue unapokuwa soko maana yake wewe unaua ajira zako, ndiyo maana sasa hivi nina asilimia 65 ya vijana ambao umri wao uko chini ya miaka 35, wote hawana kazi, unakuta  kuna madaktari wanauza mirunda,  hebu jiulize wewe unasoma udaktari halafu matokeo yake unakwenda kuuza mirunda pale Manzese,” alisema.

Alipoulizwa kama kuna jitihada zozote zinafanywa za kukutana na Dangote ili kuweka sawa mambo yaliyojitokeza, Mwijage alisema tayari Katibu Mkuu wa wizara yake amewasiliana na bilionea huyo na amemhakikishia kwamba hakuna tatizo lolote.

Alipoulizwa ukweli wa madai kuwa Dangote anataka kununua makaa ya mawe ya Afrika Kusini na si Tanzania, Waziri Mwijage alikiri suala hilo.

“Ni kweli Dangote anataka kununua makaa ya mawe ya Afrika Kusini, huo si uwongo, ni ukweli na hiyo inasababisha msuguano. Lakini akinunua makaa tani 36 elfu  kutoka Afrika Kusini,  ajira kwangu inakuwa si nyingi.

“Katika Ilani ya CCM mimi niliambiwa nitengeneze ajira 40 elfu, sasa hiyo ajira nitaipata wapi? Kama asilimia 40 ya ajira naambiwa itengenezwe kutokana na viwanda sasa kama makaa yanatoka Afrika Kusini, wenye kiwanda cha kuchimba makaa ya mawe hapa nyumbani watapata wapi ajira?

“Wanazungumzia makaa ya mawe, nimewaleta wanasayansi hapa nimewaonyesha wanahabari jana (juzi) wamekuja na vitabu vinavyoonyesha parameter za nishati kwamba ni bora na thamani ya makaa ya nishati yetu kwa mahitaji ya viwanda mbalimbali yanaonekana makaa ya kwetu yako juu,” alisema Mwijage.

Gazeti hili lilipomuuliza juu ya uhuru wa mwekezaji katika kuchagua aina ya nishati anayoitumia na mahala anakoitoa, Waziri Mwijage alijibu kwa kifupi kwamba kama anataka makaa ya mawe aende Ngaka.

Kutokana na jibu hilo, MTANZANIA Jumamosi  lilimuuliza tofauti ya gharama za makaa ya mawe ya hapa nchini na Afrika Kusini, ambapo Waziri Mwijage alilifafanua kuwa hadi katikati ya wiki hii Afrika Kusini waliuza tani moja kwa dola za Kimarekani 83 na usafiri kwa njia ya meli hadi hapa nchini ni dola za Marekani 20 kwa tani.

Alisema kwa hapa Tanzania tani moja inanunuliwa kwa dola za Kimarekani 39 na gharama za usafirishaji kwa tani moja ni dola 45.

Katika hatua nyingine, gazeti hili lilimtafuta aliyepata kuwa Waziri wa Uwekezaji Ofisi ya Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Mary Nagu, ili kufahamu undani wa uwekezaji huo wa Dangote.

Dk. Nagu, ambaye alianza kufafanua majukumu aliyokuwa akiyabeba kama kuvutia mazingira ya uwekezaji, huku utekelezaji ukifanywa na sekta ambazo mwekezaji alitaka kuwekeza, alisema uwekezaji wa Dangote waliufanya ili kudhibiti bei iliyokuwa ikipandishwa kiholela na makampuni ya saruji.

“Kuhusu Dangote tulifanya kila tunaloliweza ili kuondoa group (kundi) ambalo walikuwa wanaweza wakaamua bei wao, bei ya saruji Tanzania ilikuwa juu sana na wale waliokuwapo kwa maana ya uzalishaji walikuwa wanapanga bei kama group, sasa bei ikawa inapanda, tukaona namna pekee ya kuifanya bei ishuke ni kumpata mwekezaji atakayewekeza kiwanda chenye kuzalisha saruji nyingi na kutafuta bei ya kujitegemea mwenyewe,” alisema Dk. Nagu.

Alisema walifanya kazi kubwa ya kumshawishi sana Dangote, hasa ikizingatiwa kuwa mikoa ya kusini, licha ya kuzalisha gesi wakati huo hakukuwa na kiwanda.

“Hivyo tuliona kwamba ni vyema kupata mzalishaji mkubwa kwa kusini ili kusaidia watu kupata ajira,” alisema Dk. Nagu.

Gazeti hili lilimuuliza mazingira ya Dangote kupewa incentives (vivutio vya uwekezaji) kama ni kweli na kwamba vingine havikuwa vya maandishi, ambapo alijibu kwa kusema Serikali haiwezi kutoa incentives kwa mdomo.

“Serikali gani inatoi kitu kwa mdomo? Ujue kuna hisia nyingi sana, unaweza ukakuta yapo mengine, lakini si rahisi sana, haya ni mambo ya kibiashara, kama kuna walioingia kienyeji kwenye hiyo mikataba mimi nitawashangaa sana.

“Ila kwa kweli kama watachezea uwekezaji wa Dangote, watarudisha tena kupanda kwa bei ya saruji hapa nchini, kwa sababu hakuna kiwanda kinachozalisha kwa ukubwa ule, halafu ukizingatia huyu ni mwekezaji kutoka Afrika, sasa sisi Waafrika hatutawahi kuendelea kama kila mtu anashika shati ya mwingine, lakini kama ana makosa kwa maana kuna vitu amefanya kimya kimya basi unayo nafasi ya kutafuta, nchi yetu haitaki mambo ya siri, hasa yale hasi,” alisema Dk. Nagu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles