Na MOHAMED HAMAD,
KILINDI
KAMANDA wa Polisi mkoani Manyara, Francis Masawe, amezima mapigano kati ya wananchi wa Kijiji cha Lembapuli, wilayani Kiteto, mkoani Manyara na Kijiji cha Mafisa, kilichopo Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, waliokuwa wakigombea mpaka.
Gari moja aina ya Noah lenye namba za usajili T 943 CAK, mali ya Saruni Saninyu (32) lilichomwa moto na baadhi ya wananchi wa Kijiji
cha Mafisa, wilayani Kilindi, waliokuwa na silaha za jadi na za moto, wakati wakiweka mpaka wa Wilaya ya Kiteto na Kilindi, baada ya kukataa
uliowekwa na Tume ya Waziri Mkuu.
Akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya ya
Kilindi na Kiteto, kilichofanyika wilayani Kilindi, Mgaya Nyange,
Katibu Tarafa wa Tarafa ya Kwekivu, aliwaambia wajumbe hao kuwa, Baraza
la Madiwani wa Halmashauri ya Kilindi walikataa mipaka iliyowekwa na
Tume ya Waziri Mkuu.
“Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Kilindi kilichofanyika
hivi karibuni, kwa pamoja madiwani walikataa taarifa ya tume ya Waziri
Mkuu, waliowasilisha baada ya kufanya kazi ya upimaji wa mipaka ambapo
walituma ujumbe wa kumtaka Waziri Mkuu afike kijijini hapo kusikiliza
kilio chao,” alisema Katibu Tarafa huyo.
Kufuatia hali hiyo, wananchi wa Kijiji cha Mafisa waliungana pamoja wakiwa na silaha za jadi na za moto, kwenda kuweka mpaka wao, kisha
kuteketeza gari aina ya Noah lililokuwa na wajumbe watatu wa Kijiji cha Lembapuli Kiteto, waliofika kuona jinsi mpaka huo unavyowekwa.
Akiwa katika Kijiji cha Lembapuli Kiteto, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Manyara, Fracis Masawe, aliambiwa na uongozi wa Kijiji hicho kuwa, hali si shwari, wananchi wamefunga shule yao ya Lembapuli na kuhamisha
familia baada ya kuambiwa muda wowote watavamiwa na watu wa Mafisa wakiwa na silaha za jadi na za moto.
Kamanda Masawe aliwataka wananchi hao kuwa na subira na wakae eneo moja wasitawanyike, kisha kuingia porini na kikosi cha Polisi wa FFU kusaka watu hao waliokuwa wamedaiwa kuwa porini wakiweka mipaka yao kinyume cha taratibu za nchi kati ya Mkoa wa Manyara na Tanga.
Akiwa katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama, aliwaambia viongozi wa pande hizo kuwa, matatizo hayo yanalelewa na baadhi ya viongozi ambao wanachelewesha kutatua matatizo ya wananchi kwa wakati,
hivyo wananchi kuamua kufanya watakavyo, wakijua hawawezi kufanywa lolote.
“Baadhi ya viongozi mmeshindwa kutimiza wajibu wenu… sasa wananchi
wameamua kututumbua. Nilipoambiwa kuwa kuna watu wachache wako porini
wana silaha, viongozi wa Lembapuli wakanisihi nisifike eti watatujeruhi
kama sio kutuua… nikasema hili halijafikia kuwa hivyo kwa nchi yetu
ya Tanzania,” alisema Masawe.
Alisema pamoja na jitihada zilizofanywa na Tume ya Waziri Mkuu,
kubainisha mipaka kati ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, bado kuna
tatizo linahitaji ufafanuzi kwa Waziri Mkuu, kwani hata alipofika
kuongea na wananchi hao, waliokuwa wanaweka mipaka hiyo, kabla ya
kuchoma gari walimhakikishia kuwa hapatakuwa na tatizo.
Kwa mujibu wa Tamimu Kambona, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiteto,
alimweleza Kamanda Masawe, mgogoro huo ulisababisha watu wanne
kupoteza maisha kwa vipindi tofauti, kufukiwa kisima kirefu cha maji pamoja na kuchomwa moto mashine ya maji na jana gari moja aina ya Noah kuchomwa moto.
Kamati hizo kwa pamoja walikubaliana, wahalifu wakamatwe na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria, mipaka ya kisheria iheshimiwe, mita 100
kutoka kwenye mpaka pasifanyike shughuli mpya ya uandaaji wa mashamba pamoja na kuheshimu maamuzi ya ngazi za juu yatakayotolewa na viongozi wao.