NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
BASI la Safari Njema namba T 990 AQF linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Dodoma, limeteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba saruji ambalo nalo liliteketea kwa moto.
Ajali hiyo iliyotokea jana jioni eneo la Kimara Stop – Over, Dares Salaam, imeacha simanzi huku wananchi waliokuwa kwenye eneo la tukio wakiangua vilio kwa hofu ya abiria waliokuwa ndani basi hilo kuteketea kwa moto.
Habari zinasema lori hilo namba T 534 BYJ liliteketea kwa moto na kubaki tela tu.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Denis Atiris, alisema ajali hiyo ilitokea saa 8:20 mchana baada ya lori kukosa mwelekeo na kuligonga basi hilo la abiria.
“Lile lori lilionekana kukosa mwelekeo, lilikuwa linatoka mjini kuelekea Mbezi, lilionekana likiyumba kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
“Dereva wa basi alikuwa anatoka kituo cha Gereji ambako aliingia kushusha abiria. Wakati anatoka kituoni kuingia barabarani ndipo akaona lori likiyumba, ikabidi alikwepe kwa kutoka kidogo nje ya barabara ili wasigongane uso kwa uso.
“….kwa bahati mbaya lile lori lilikwenda moja kwa moja kugonga sehemu ya ubavuni mwa basi, kukawa na kishindo kikubwa na ghafla moto ukaanza kuwaka ndani ya basi,” alisema Atiris.
Shuhuda huyo alisema kitendo hicho kilitokea ndani ya sekunde chache na baadhi ya abiria waliokuwa ndani ya basi walionekana wakiruka nje kupitia madirishani.
“Ikabidi mimi na mwenzangu anayeuza maua hapa jirani na kituo, tuingie ndani wakati huo moto ulikuwa… si mkubwa sana, tukafanikiwa kuwatoa watoto watano na wa-dada wanne,” alisema.
Alisema hata hivyo hawakuweza kuokoa wengi zaidi kwa vile moto ulizidi kuongezeka baada ya kama dakika 15.
Saruji yaibwa
“Watu waliongezeka kadri muda ulivyosonga lakini jambo la kusikitisha ni kwamba hawakuja kusaidia kuokoa badala yake walikimbilia simenti (saruji) iliyokuwa kwenye lori wakaanza kuiba,” alisema na kuongeza:
“Kwa kweli kitendo kile kimenisikitisha mno, watu tumekosa uzalendo na utu kabisa, tungesaidia tungeweza kuokoa wengi”.
Atiris alisema hata hivyo hakumbuki idadi ya abiria waliokuwamo ndani ya basi hilo.
“Gari la kwanza lililofika eneo la tukio ni la polisi ambao walitusaidia kubeba wale majeruhi na kuwawahisha hospitalini, walitupa ushirikiano mzuri.
“Lakini jambo linalonisikitisha ni hawa wa Zimamoto, tangu saa 8:20 wamekuja saa 11:20 gari lote likiwa limeshateketea kwa moto na hakuna kitu kilichosalimika,” alisema shuhuda.