IKIJULIKANA kwa tamaduni mtambuka, India ni Taifa lina mila na desturi nyingi zinazotambulisha jamii mbalimbali ziishizo humo.
Kuanzia jimbo la Kashmir hadi Kanyakumari – taifa hilo lina aina nyingi za ibada za kidini na kitamaduni zinazorudi nyuma miaka 700 iliyopita.
Wakati baadhi ya ibada zikiwa na maana ya kisayansi, vitendo vingi vya kitamaduni au kiimani vinaonekana vimekuwa zikifuatwa tu ili mradi.
Ni kwa vile jamii zimezikuta baada ya kutumika kwa miaka mingi na zinaendelea bado kufuatwa na kundi kubwa la watu nchini humo.
Ibada kama vile urushaji vichanga chini kwa umbali wa futi 30, unaonekana kukosa maana yoyote ya kisayansi lakini jamii nyingi huiendekeza katika sehemu tofauti za nchi hii.
Watoto wachanga wanaopiga kelele wakiwa na nyuso za hofu na kihoro huku wakiangua vilio husukwa sukwa huko na huko na wanaume waliovalia lubega ambao ni viongozi wa kidini kabla ya kuwadondosha kutoka roshani umbali wa futi 30 kutoka ardhini.
Huu si mchezo wa filamu za kutisha, bali ibada kongwe inayoendeshwa kusini mwa India, ikidaiwa kuwa na uwezo wa kuwaletea vichanga hao bahati njema, afya na ustawi.
Kwa wasio na mioyo migumu huwawia ugumu wa kuangalia kitendo hicho kinapofanyika, ambacho hushuhudiwa kila mwaka katika jimbo la Karnataka.
Kutokana na kutisha kwake, kumeyafanya makundi ya watetezi wa haki za watoto kukiita kuwa cha ‘kishenzi’ na kutaka kipigwe marufuku na serikali ya India.
Kitendo hicho kinaaminika kurudi nyuma karne nyingi zilizopita na kinafanyika kote nchini India kikihusisha dini zote za Hindu na Uislamu.
Jina halisi la ibada hii ya urushaji mtoto mchanga inabakia kutofahamika, lakini imekuwa ikiendeshwa kwa miaka 700 iliyopita na dini zote Wahindu kwa Waislamu katika majimbo hasa ya Karnataka na Maharashtra.
Pia hudai huhakikisha ustawi wa familia nzima. Ibada hiyo, ambayo kwa kawaida hulenga watoto wenye umri chini ya miaka miwili, machoni mwa wakosoaji inaonekana kuwa ya kijinga mno.
Ni kwa vile haina msingi wowote wa kueleweka zaidi ya kubakia kuwa imani potofu tu kwa waiendekezao.
Lakini waumini na wakazi wa maeneo husika bado wanaiamini pamoja na kelele zinazopazwa kila uchwao na makundi ya haki za binadamu.
Katika video inayoonesha sherehe ya mwaka 2009, wanaonekana makuhani wakisuka vichanga huku na kule vikiwa na nyuso za hofu na kihoro kabla ya kuvirusha chini ardhini, ambako wakazi wanasubiri kwa blanketi ili vidondokee humo.
Kwanza mmoja wa mmoja wa makuhani humshikilia kichanga mikono na miguu mithiri ya kikapu kinachosukwa sukwa huko na huko hewani, kisha akipaza sauti ya kumsifu Bwana. Na kisha hukirusha chini kichanga husika.
Wakati watoto wanapotua salama, kundi lililo huko chini husherehekea kwa nguvu mithiri, wakikipitisha kichanga kutoka kwa mmoja miongoni mwao hadi mwingine kabla ya kukirudisha kwa mama yake.
Kwa ujinga wao, hawajui kuwa inachukua dakika kadhaa kabla ya kichanga kurudia hali ya kawaida kutokana na mshituko kiliopata wakati wa usukasukaji na urushaji kwa umbali huo.
Wanaharakati walifanikisha kupigwa marufuku kwa ibada hiyo potofu na ya kikatili kwa mtoto mwaka 2011, lakini ikarudi katika mahekalu ya Digambeshwara katika Kijiji cha Nagrala mwaka uliofuata.
Hilo lilimkatisha tamaa mtu kama Lov Verma, kutoka Tume ya Taifa ya Kulinda Haki za Mtoto, ambaye yu mstali wa mbele kukemea vitendo hivyo.
Verma alisema: “Nimeshtushwa na kitendo hiki. Hii si kazi ya serikali pekee. Tunahitaji kushirikiana kuelimisha wale wote wanaoshiriki katika kitendo hiki cha kishenzi hasa hawa viongozi wa dini na jamii hizi.”
“Niliangalia picha ya sherehe ya urushaji watoto mwaka 2009, hakika namna watoto wanavyotendewa, nalazimika kusema, ni kitendo cha kutisha kwa kweli.”
Ijapokuwa hakuna mtoto aliyeumizwa hadi sasa, inaonekana si kitendo salama, kwa sababu matokeo yanaweza kuwa mabaya wakati wowote, anasema.
Lakini washiriki wanadai ni wajibu wao wa kidini kuhudhuria sherehe hizo.
Mmoja wa waumini alisema: “imani ya dini yetu huvuta wengi wetu kuhudhuria sherehe hii kila mwaka.”
Kwa kweli, mamlaka za mahekalu zinaamini, “kwa kufanya hivyo, watotio watakuwa na afya, wenye nguvu na kuishi miaka mingi.”