20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Wananchi Linga wawajengea walimu nyumba wasiwakimbie

Diwani wa Kata ya Linga, Edmund Magendo (mwenye koti jeusi), akiwa na wananchi nje ya moja ya nyumba za walimu zinazoendelea kujengwa.
Diwani wa Kata ya Linga, Edmund Magendo (mwenye koti jeusi), akiwa na wananchi nje ya moja ya nyumba za walimu zinazoendelea kujengwa.

Na AMON MTEGA – NYASA

ILI kufanikiwa kufikia malengo ya kuwa na elimu bora hapa nchini ni lazima changamoto zinazoziikabili sekta hiyo zitatuliwe kwa kushirikiana yaani serikali pamoja na wananchi.

Baadhi ya mikoa hapa nchini iliyofanikiwa kwa wananchi wake kupata elimu iliyo bora ni kutokana na ushirikiano wa pande mbili ambapo kila upande uliweza kufanya kazi ya kujitoa na bila kuutegea upande mwingine.

Hali hiyo inaweza kufanikiwa katika kipindi hiki cha Utawala wa Awamu ya Tano kwa kuwa umeonyesha njia namna ya kuzikabili changamoto zinazozikumba shule za serikali na kuzifanya ziwe na ufaulu mdogo huku shule zinazomilikiwa na watu binafsi au taasisi mbalimbali zikiwemo za dini zikifanya vizuri kiasi cha wananchi wengi kuvutiwa nazo.

Kwa kuliona hilo Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujitwisha mzigo wa kukabiliana na changamoto hizo ambazo wamebaini kutokuwepo kwa baadhi ya miundombinu kwenye shule zake kama vile upungufu wa madawati, matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za walimu.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya maeneo hapa nchini wameanza kujitoa kuunga mkono serikali kwa kufanya kazi za kujitolea ili kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu.

Wakazi wa Kata ya Linga Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ni mfano wa kuigwa kwani wameamua kujitoa kwa kujenga nyumba za walimu kwa nguvu zao wenyewe.

WAZO LA KUJENGA NYUMBA

Akizungumza na Mtanzania, Diwani wa Kata ya Linga, Edimund Magendo, anasema kabla ya kufikia uamuzi huo waliitisha mkutano na kupeana changamoto za kutokuwepo kwa elimu bora ambapo walibaini kuna vitu vinavyochangia kukwamishwa kwa upatikanaji wa elimu bora kama upungufu wa nyumba za watumishi.

Diwani huyo anasema baada ya kubaini changamoto hizo waliamua kuanza kujenga nyumba za walimu kwa kuwa tayari welikwishaanza kufyatua matofali kwa kila kijiji cha kata hiyo kwa malengo ya matumizi ya ujenzi wa nyumba za walimu.

Magendo anafafanua kuwa kata hiyo ina vijiji vitatu cha Lukali, Ngingama na Litumbakuhamba huku shule za msingi zikiwa mbili ambazo ni Ngingama na Litumbakuhamba.

“Shule zote hizi zimekuwa na upungufu wa nyumba za walimu, tumekadiria katika kila shule kutajengwa nyumba nane za walimu na kwa sasa tumeshajenga nyumba saba,” anasema.

Anafafanua kuwa katika Shule ya Msingi Ngingama zimejengwa nyumba nne na Litumbakuhamba zimejengwa nyumba tatu na tayari walimu wameshaanza kuishi humo.

Anasema mkakati wao ni kuhakikisha ndani ya miaka mitatu wanameondoa tatizo la upungufu wa nyumba za walimu na kuachana na tabia ya kubaki  kuendelea kuisubiri serikali ifanye kila kitu jambo ambalo linachelewesha kufikia malengo waliyojiwekea.

Kulingana na diwani huyo, gharama ya ujenzi kwa kila nyumba ni zaidi ya Sh milioni sita.

“Sisi tuna kila sababu ya kujenga nyumba ambazo garama yake inaonyesha kuwa ya chini ili kunusuru walimu wasiwe na visingizio vya kuyakimbia mazingira,” anasema.

WALIMU KUKIMBIA

Anasema changamoto hiyo ya ukosefu wa nyumba za walimu ilisababisha baadhi ya walimu kuripoti kasha kuondoka huku wakitoa visingizio mbalimbali kama vya ukosefu wa nyumba.

“Walikuiwa wakiripoti katani na wakikutana na changamoto ya kukosa makazi wana visingizio mbalimbali vya kiafya na wengine kudai kuwa wanaenda kusoma. Jambo hili limekuwa likirudisha nyuma masuala ya upatikanaji wa elimu bora katika eneo letu,” anasema.

Anasema kuwa changamoto kubwa ambayo wamekuwa wakikutana nayo katika ujenzi wa nyumba hizo ni kukosa wataalamu wa ujenzi wa kwenda kuwashauri pamoja na mahitaji ya vifaa vya viwandani kutokana na bei kuwa ghali hasa katika maduka ya vifaa vya ujenzi pamoja na gharama za kuvisafirisha hadi kijijini hapo.

Magendo ambaye amejipambanua kutatua changamoto zinazoikabili kata yake anasema kuwa licha ya kuwepo na upungufu wa nyumba za walimu lakini bado kuna chamoto ya mawasiliano ya simu za kiganjani, vyombo vya habari kutowafikia na kulazimika kusikiliza redio za nchi jirani ya Malawi.

“Hali hii inatufanya tuchelewe kupata taarifa muhimu za kitaifa kwa wakati huku baadhi ya watumishi wakihisi kuwa wametegwa jambo ambalo linawapunguzia morali ya kufanya kazi,” anasema.

Aidha ameelezea changamoto nyingine katika sekta ya kilimo kuwa kata hiyo imekuwa kwenye eneo ambalo mvua hunyesha kwa kiwango kidogo licha ya ardhi yake kuwa na rutuba nyingi yenye uwezo wa kuzalisha mazao mbalimbali.

Anaiomba serikali kupitia wataalamu wake kuangalia namna ya kuwawekea kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mto Ruhuhu ambao umekuwa mkombozi mkubwa kwao kutokana na shughuli mbalimbali ikiwemo kustawisha mifugo yao.

MRATIBU WA ELIMU

Kwa upande wake Mratibu Elimu wa kata hiyo, Onesmo Mbunga, anasema kuwa kumekuwepo na changamoto katika kipindi cha nyuma kwa walimu kushindwa kuwepo kutokana na kukosekana kwa nyumba za kuishi.

Anasema jambo limekuwa likisababishia wanafunzi kuwa watoro na kushusha viwango vya ufaulu.

Mbunga amesema baada ya wakazi wa kata hiyo kuweka mikakati ya ujenzi wa nyumba za walimu na kuchangia chakula cha wanafunzi wawapo shuleni, kumeamsha morali ya walimu kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupunguza utoro wa wanafunzi kwenye shule hizo.

Mratibu huyo amefafanua kuwa kutokana na vipato kuwa duni katika kata hiyo wanajikongoja kuhakikisha wanatatua kero za elimu kwenye shule zao.

“Wananchi wengi huku wana hali duni na hawana uwezo wa kuwapeleka watoto katika shule za watu binafsi ndiyo maana tunajitahidi kwa kushirikiana nao ili kutatua changamoto zilizoko katika sekta ya elimu,” anasema Mbunga.

Pia anasema wakazi hao wameweza kuchangia katika utengenezaji wa madawati 120 ambapo kila dawati limegharimu Sh 50,000. Anasema hadi sasa madawati 78 yameshakamilika huku mengine yakiendelea kutengenezwa.

WANANCHI

Mmoja wa wakazi wa kata hiyo ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Flolian Mapunda, anasema kuwa wao wataendelea kujitoa katika masuala ya elimu kwa kuwa serikali ya sasa imeonyesha njia hasa katika kuboresha shule zake.

“Hakuna muujiza wa ajabu utakaoweza kuwaletea kizazi hiki zaidi ya elimu bora hasa katika kipindi hiki kinachotarajiwa kwenda kwenye uchumi wa kati wa viwanda, hivyo tujitoe katika maendeleo ya elimu,” anasema Mapunda.

MBUNGE

Mbunge wa Nyasa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stela Manyanya, anasema; “Wako watu wachache ambao wanawakatisha tamaa wenzao hasa katika kuboresha sekta ya elimu, watu hao ni wa kuwapuuza. Jambo muhimu kwa wazazi ni kutoa ushirikiano kwa walimu kwa kuboresha mazingira kwa kujenga nyumba nzuri za walimu.

Anasema pia katika jimbo hilo kutakuwa na mashindano ya ufaulu kubaini shule gani imefaulisha vizuri na kutaka kila shule iwe na shamba darasa kwa ajili ya somo la kilimo.

Anasema serikali imejipanga vema ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 kila kaya hapa nchini ina mwanafamilia ambaye ana elimu ya sayansi.

“Tunakwenda kwenye uchumi wa kati wa viwanda hivyo ni lazima ifikapo mwaka 2020 kila kaya iwe na mwanafamilia ambaye amesoma masomo ya sayansi ili kukabiliana na changamoto za ajira ambazo asilimia kubwa zitawabeba watu wenye masomo ya sayansi,” anasema Manyanya.

Anasema kuwa ili kufika kwenye malengo ya uchumi wa kati ambao ni wa viwanda ni lazima kujitoa katika suala la elimu kwa kuhakikisha vijana wanawezeshwa kuzikabili changamoto zilizopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles