29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Tatizo ni “Panya Road” au mfumo  

panyaroad-1NI mara nyingine tena tunasoma habari za “panya road”. Nakumbuka, wakati wa Kamanda Kova na kabla ya hapo makamanda wengine walioshughulika na “panya road”, kuandika kuwa njia za kiusalama, kwa maana matumizi ya nguvu na kuwakamata kusingeweza kusaidia kuliponyesha donda hili la vijana wanaoleta hali ya hatari katika jamii.

Polisi wamekuwa na tabia ya kujivuna kuwa wamevunja mtandao wa wahalifu, wamepata habari za kiintelijensia kuwa kuna tukio lingetokea na hivyo wameliharibu kwa kuwakamata wahusika, kuwa kiongozi wa mtandao amekamatwa; lakini kila wakitangaza kukamatwa kwa wahalifu, baada ya muda mfupi au mrefu kidogo makundi hayo ya wahalifu yanajitokeza tena. Na sasa yamerudi tena kutishia usalama na kuhatarisha mali  na maisha. Na tatizo ni kuwa hatufanyi uchambuzi wa kina wa sababu(causal analysis), baada ya tukio na kutoa jibu la uhakika na la mwisho.

Nilishawahi andika mara nyingi kuwa ili kuweza kutatua tatizo la kijamii… ni vizuri sana kuhakikisha kuwa utafiti unafanyika. Utafiti kama huo wa tatizo la panya road ungehusisha kujua makundi hayo yanajitokeza katika maeneo gani ya mji, watu wenye umri gani, kiwango gani cha mapato na katika nyakati gani  na watu wanaowazunguka wana uhusiano gani na jamii. Lakini nilisema hata ukilichambua jina lenyewe – Panya Road, lina maana kubwa sana. Kuwa ni kielelezo cha maisha yasiyo na uhakika kwa wanaohusika na hivyo huishi kwa kutegemea kuvamia kisicho chao.

Kwa nini panya roda wasitokee Oysterbay au Masaki au Upanga au Mbezi Beach. Kwa nini wanatokea maeneo ya watu masikini. Kuna uhusiano gani kati ya kujitokeza mara kwa mara kwa panya road na maeneo wanakoishi na kiwango cha uchumi cha jamii au watu wanaoishi huko? Je vijana hao wamemaliza darasa la ngapi kwa wastani na wana historia yoyote ya kufanya kazi? Kuna aina gani ya shughuli ambazo vijana wanafanya? Na kama wavulana wanajiingiza kwenye “panya road” wasichana wanashughulika na nini? Wazazi nao wanashughulika na nini? Je, hao vijana wanaishi na wazazi wao au wanaishi peke yao kwenye magheto?

Maswali ni mengi sana ambayo polisi wangejiuliza? Najua polisi hawakusoma kwa undani sosholojia kwa ujumla lakini kama wamesoma sosholojia ya uhalifu (sociology of crime).. wangeweza kupata majibu kama wangeona kuwa kutumia nguvu ni moja ya njia na sio mbinu pekee. Kama Serikali walikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya utafiti kwa kuwatumia wataalamu utafiti kutoka vyuo vikuu. Tunajua kuwa “panya road” ni makundi yaliyojificha (hidden communities),  basi watafutwe wataalamu wa kufanya utafiti katika makundi kama hayo na majibu tunayopata yatasaidia kutoa majibu juu ya sababu ya kuwapo na kujitokeza mara kwa mara kwa tatizo na  namna ya kuliondoa tatizo.

Kuna namna nyingi ya kuliondoa tatizo kama hilo, au kwa kutumia polisi, au kwa kuanzisha programu za maendeleo na za kijamii katika maeneo ya watu masikini.  Kila mara ninapenda kusema kuwa matatizo katika ngazi ya kitaifa yanatakiwa kuondolewa kwa kuwa na programu. Tukishafanya hatua ya kwanza ya kulisimamisha tatizo lisiendelee kwa kufanya ukamataji na kuwapeleka polisi, tukae chini kubuni mkakati wa kudumu na huu ni wa kuchunguza sababu na kutoa majibu na kuwekeza fedha na kuanzisha taasisi. Kumbuka kuwa wengi wa panya road ni vijana masikini, wasio na uhakika wa leo na kesho. Kuwakamata na kuwapeleka polisi ni sawa na kuwarahisishia maisha tu. Angalau watakula bure na wakirudi kutoka jela watakuwa wamepanda kidato cha juu cha usugu, na pengine uhalifu, maana watarudi kwenye mazingira yale yale ya umasikni waliyoyaacha na kuwasababishia kuwa panya road.

Niliwahi kuandika pia kuwa jeshi la polisi polisi linatakiwa kuwa na wataalamu waliobobea katika maswala ya saikolojia, falsafa, siasa, sosholojia na kadhalika, ili waweze kuendesha mambo yao kitaalamu sana. Na hilo kwangu ni muhimu kwa sababu polisi sio tu chombo cha Serikali, bali pia wanaweza kuwa wakandarasi wa Serikali wakiishauri juu ya namna bora ya kutatua matatizo kama hayo ikionekana mbinu za kipolisi peke yake hazitoshi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles