Na Walter Mguluchuma, Katavi
MKOA wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya minne iliyoanzishwa mwaka 2012, ambao unakabiliwa na tatizo la mimba za utotoni zinazosababishwa na mila na desturi za baadhi ya makabila yalioko katika mkoa huo.
Baadhi ya makabila yaliyoko mkoani hapa yanaona ni jambo la kawaida kwa watoto wao kuolewa wangali bado wadogo kutokana na tamaa ya wazazi ya kutaka kujipatia fedha na mifugo.
Wapo wazazi ambao wamekuwa wakiwaozesha watoto wao bila kujali umri kama ilivyotokea mwaka jana katika Shule ya Msingi Mwamkulu, ambapo mwanafunzi wa darasa la nne alinusurika kuozeshwa na wazazi wake ndoa ya kimila.
Hata hivyo, Ofisa Elimu wa Manispaa ya Mpanda, Vicent Kayombo, ndiye alimwokoa msichana huyo kufungishwa ndoa hiyo.
Pia wapo baadhi ya wanaume ambao wamekuwa wakitumia vibaya mwanya wa dini unaoruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja na kuamua kuacha wake zao na kuoa watoto wadogo na kwenda kuishi nao maeneo ya mashambani.
Muuguzi Mkuu mstaafu wa Wilaya ya Mpanda ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kawajense, Pius Buzumalle, ni miongoni mwa wakazi ambao wameshtushwa na taarifa iliyotolewa hivi karibuni ya Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu (DHS) wa mwaka 2015/16, ambao unaonyesha mkoa huo una asilimia 45 za mimba ya utotoni.
Anasema hana shaka na takwimu hizo kutokana na wakazi wa mkoa huo kuchelewa kupata elimu ya umuhimu wa uzazi wa mpango toka miaka ya nyuma.
Anatoa mfano wa waliokuwa raia wa Burundi ambao wamepewa uraia wa Tanzania wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mpanda na wale wa Mishamo kutokana na imani za mila zao.
“Wanaamini kuwa mwanamke mmoja anatakiwa kuzaa watoto kuanzia saba na kuendelea, akizaa watoto sita wanadai alikuwa anasafisha tumbo hivyo wanahesabu mtoto wa saba ndio humwita kuwa ndio mtoto wa kwanza.
“Hivyo ili afikie idadi ya watoto saba na kuendelea humlazimu mwanamke aanze kuzaa huku akiwa na umri mdogo,” anasema Buzumalle.
Mwaka jana Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, wakati alipokuwa kwenye ziara yake kwenye makazi ya wakimbizi ya Mishamo alishtushwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu.
Alilazimika kuwauliza wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara wale waliongia nchini wakati wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyotokea nchini Burundi wanyooshe mikono, lakini walionyosha walikuwa wachache huku kundi kubwa likiwa halikuonyosha.
Hivyo, walizaliwa baada ya mwaka huo hali iliyomfanya Pinda ashtuke na kuwaambia ‘mnazaliana sana’.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenelali Raphael Muhuga, anasema kwa kiasi kikubwa tatizo hilo lipo zaidi kwenye makazi ya wakimbizi ya Katumba na Mishamo na katika jamii ya wafugaji.
Anasema wamejipanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutambua masuala ya uzazi wa mpango na madhara ya mimba za utotoni.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwa mkoani humo hivi karibuni, aliagiza wanafunzi wa kike walindwe na kwamba mzazi yeyote atakayemuoza binti yake akiwa na umri mdogo akamatwe na kufungwa jela miaka 30.
Elias Kifunda ambaye ni wakili wa kujitegemea, anasema uzazi wa mpango ni muhimu ingawa kwa muda mrefu haukuonekana kutiliwa mkazo na kuwaacha watu kuzaa hata katika umri mdogo suala ambalo linayumbisha maendeleo endelevu ya Taifa.
“Tanzania imejikuta ikikumbwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu huku nusu yao wakiwa ni vijana na watoto wenye umri mdogo, hivyo kusababisha Serikali kubeba mzigo mkubwa wa kuwahudumia,” anasema Kifunda.
Anasema kuwapo kwa idadi kubwa ya watoto na vijana wenye umri wa kwenda shule maana yake ni kwamba kuna wategemezi wengi katika Taifa yaani idadi ya wazalishaji ni ndogo kuliko wategemezi.
Mganga Mkuu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Yahaya Hussein, anasema wamekuwa wakipokea wajawazito wengi wanaoshindwa kujifungua kutokana na pingamizi la uzazi linalosababishwa na kubeba ujauzito wangali wakiwa wadogo.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya wajawazito kupoteza maisha au watoto na kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa fistula.
Mbaya zaidi wasichana wengine wenye umri mdogo wamekuwa wakiolewa na watu wazima matokeo yake wanalazimika na wao kuwa watu wazima pasipo kutarajia kutokana na kuishi maisha ambayo hayalingani na umri wao.
Mratibu wa Marie Stopes Mkoa wa Katavi, Seif Mjune, anasema tatizo hilo mbali ya kuwapo kwenye makazi ya wakimbizi pia lipo katika Kata ya Majimoto wilayani Mlele ambako kuna jamii ya wafugaji.
Marie Stopes kwa kutambua uwepo wa tatizo hilo imeweka mikakati mbalimbali itakayosaidia kupunguza tatizo la mimba za utotoni.
Wameteua baadhi ya vijana na tayari wameshawapatiwa mafunzo ili waende kutoa elimu kwa vijana wenzao.
Wamefanya hivyo baada ya kugundua vijana wamekuwa wakishindwa kwenda kwenye maeneo yanayotoa elimu ya afya ya uzazi kama vituo vya afya na zahanati kwa kuhofia kukutana na wazazi wao.
Marie Stopes kila mwezi wamekuwa wakituma wataalamu kwenye halmashauri zote za Mkoa wa Katavi na kila halmashauri kwa lengo la kutoa elimu ya afya ya uzazi.
Pia anashauri wajawazito waache tabia ya kunywa dawa za kienyeji pindi wanapopata uchungu kwani wapo baadhi yao wamekuwa wakiamini kuwa wakinywa majani ya chai huwasaidia kuongeza uchungu ili wajifungue haraka jambo linalosababisha vifo vya akina mama na watoto wachanga.