Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Social Action Trust Fund (SATF) lenye makazi yake Mikocheni Dar es Salaam, limetoa msaada wa madawati 100 ili kusaidia juhudi za Serikali pamoja na wadau wengine kumaliza tatizo hilo.
Akipokea msaada huo juzi, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob (Chadema), alisema msaada huo ni muhimu sana kwa wakati huu ambapo manispaa yake inafanya juhudi za kumaliza uhaba wa madawati na viti kwa walimu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
“Mpango tulionao katika manispaa yetu ni kuhakikisha hadi Agosti mwaka huu, hakuna mwanafunzi atakayekaa chini kwani tutakuwa tumejitosheleza.
“Nawashukuru sana SATF kwa msaada wenu, sisi kama manispaa tunawaomba wadau wengine wa elimu kujitolea kuchangia madawati mengi zaidi ili watoto watakapovunja wapewe mengine maana ni watundu sana,” alisema.
Aidha, alisema wazabuni waliopewa kazi ya kutengeneza madawati zaidi ya 16,000 katika manispaa hiyo, wanaendelea na kazi ambapo muda wowote yatagaiwa kwa shule mbalimbali za manispaa hiyo haraka iwezekanavyo.
Awali Meneja Programu wa SATF, Rogasian Massue, alisema msaada huo umo kwenye mpango wao wa kusaidia wilaya mbalimbali ili vijana waweze kupata elimu na kuwa wataalamu wa baadaye.
Alisema walikuwa na programu ya kutoa msaada wa madawati 150 katika Halmashauri ya Chato mkoani Geita na baadaye walifuatia Kinondoni Dar es Salaam ambayo imepewa madawati 100.
Meneja huyo alisema wanajiandaa kupeleka msaada kwa Manispaa za Temeke na Ilala zote za Dar es Salaam pamoja na Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma na Kaliua iliyopo Tabora.