BERN, USWISI
ZIKIWA zimebaki hatua tano kumalizika kwa michuano ya Tour de France, nyota wa michuano hiyo ya baiskeli, Fabian Cancellara, ametangaza kujitoa akidai kuwa anataka kujiandaa na michuano ya Olimpiki.
Hii ni siku ya pili mfululizo kwa nyota wa mchezo huo wa baiskeli kujitoa wakidai kuwa wanakwenda kujiandaa na michuano ya Olimpiki ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Brazil.
Jumanne ya wiki hii Mark Cavendish naye alitangaza kuachana na michuano hiyo na leo hii ni Cancellara, ambaye ameachana na michuano hiyo na kukimbilia kwenye Olimpiki.
Cancellara, mwenye umri wa miaka 35, raia wa nchini Uswisi, ambaye aliwahi kushinda tuzo ya dhahabu mwaka 2008, amedai kuwa huu ni wakati wake wa kujiandaa na Olimpiki.
“Haya si maamuzi rahisi kuyatoa, lakini najisikia kuwa ninafanya jambo sahihi kwa muda huu, najua kuwa timu yangu inashika nafasi ya pili katika michuano hii ya Tour de France, lakini ni bora niachane nayo.
“Najua nitaiacha timu yangu katika wakati mgumu, lakini ninawataka mashabiki kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa kipindi chote kilichobaki toka sasa.
“Ukweli ni kwamba mwili wangu umechoka, hivyo kama nataka kushinda kwenye michuano ya Olimpiki lazima nipate muda wa kupumzika na kama nikisema niendelee na Tour de France nitakosa muda wa kupumzika na sitoweza kufanya vizuri kwenye Olimpiki,” alisema Cancellara.
Hii ilikuwa ni hatua ya mwisho kwa nyota huyo kushiriki michuano hiyo mikubwa ya kimataifa, hivyo amewashukuru wote ambao walimpa sapoti.
“Katika miaka 12 ambayo nimeshiriki michuano hii, nimejifunza mambo mengi sana, lakini maamuzi haya yananifanya niwe na hisia kali kwa mashabiki wangu kwa kuwa wengi wao walikuwa hawakutegemea jambo kama hili.
“Napenda kuwashukuru viongozi wa mashindano ya Tour de France kwa kipindi cha miaka yote na ubingwa ambao niliuchukua, najua hii ni historia kwangu,” aliongeza.