Na Asifiwe George, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, ametaka wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mikoa yote washindanishwe kujua utendaji kazi wao.
Waziri Mabula, alitoa kauli hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa shirika hilo kilichokuwa kikijadili mipango na makisio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17 kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Alisema hatua hiyo itasaidia kutambua wakurugenzi ambao wanasubiri kubebwa na wenzao kwa kushindwa kufanya kazi kwa weledi.
Alisema ujenzi na ununuzi wa nyumba unahitaji fedha nyingi, wananchi hununua nyumba kupitia mikopo kutoka benki.
Serikali inatambua umuhimu wa taasisi za fedha katika kusaidia ukuaji wa sekta ya nyumba jambo ambalo hufanywa duniani kote, alisema.
Alisema Serikali inatambua bado kuna changamoto ya riba kubwa ya mikopo ya nyumba inayotozwa na benki ambayo sasa ni kati ya asilimia 18 hadi 25.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuona namna bora ya kuwezesha benki kupunguza riba katika mikopo ya nyumba.
“Serikali itahakikisha benki zote zinashiriki kukopesha wananchi waweze kununua nyumba, kufanya hivi kutachochea ukuaji wa uchumi na wananchi watatumia nyumba zao kupata mikopo ya benki kwa ajili ya kuanzisha miradi yao ya maendeleo.
Mkurugenzi Mkuu NHC, Nehemia Mchechu, alisema moja ya majukumu ya baraza hilo ni kujadili mipango na makisio ya mapato na matumizi ya wizara kabla ya kuwasilishwa bungeni.
“Serikali imeweka msisitizo zaidi katika ukusanyaji wa mapato, kupitia kikao hiki tutapata maoni na mikakati ya kuboresha ukusanyaji wa kodi za ardhi,” alisema.