20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

RC aliyetemwa na JPM azua jambo  

Mkuu+wa+MkoaNA GUSTAPHU HAULE, PWANI

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, amezua tafrani katika Kijiji cha Mboga kilichopo Msoga mkoani Pwani  baada ya kuzuia mradi wa Kiwanda cha Matunda cha Sayona kisijengwe mpaka alipwe fidia ya Sh milioni 150.

Dk. Rutengwe anataka alipwe  fidia hiyo kwa ajili ya kupitisha nguzo za umeme katika shamba lake pamoja na barabara inayochongwa mbele ya shamba hilo.

Alisema kamwe bila malipo hayo mradi huo utasimama.

Hali hiyo imewafanya wakazi wa kijiji hicho kumjia juu Dk. Rutengwe wakisema wao wanataka kiwanda ambacho kitawasaidia kukuza uchumi wao na vijana kupata ajira.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara  uliofanyika juzi kijijini hapo kwa ajili ya zuio la mradi wa umeme na barabara  unaotakiwa kwenda kiwandani hapo, Diwani wa Kata ya Msoga, Hassan Mwinyikondo (CCM), alisema Dk. Rutengwe ameliandikia barua Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Pwani, akilitaka lisipeleke nguzo za umeme eneo hilo ambako kiwanda kinatarajia kujengwa hadi alipwe fidia.

Alisema baada ya kupata malalamiko ya Dk. Rutengwe, alilazimika kukutana na halmashauri ya kijiji hicho ambako wajumbe walikiri kumtambua mwekezaji huyo kutokana na kufuata taratibu zote.

“Namshangaa Dk. Rutengwe, maana yeye ni mzaliwa wa hapa halafu leo anakataa kijiji chetu kisipate kiwanda, tunaamini  kiwanda hiki kina manufaa kwa wananchi wetu… siwezi kumvumilia maana anakwamisha maendeleo ya kijiji na wananchi kwa ujumla,” alisema Mwinyikondo.

Alisema wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, alikwenda kijijini hapo na kupitisha nguzo za umeme na bomba la maji  katika mashamba ya watu, lakini hakuna fidia aliyodaiwa, sasa iweje sasa hivi sasa azue mgogoro wa aina hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Jijiji hicho, Rashid Hemed, alisema wamejaribu kumwelimisha Dk. Rutengwe kuwa barabara hiyo ni mali ya Serikali kwa sababu ilikuwa ikitumika tangu enzi za ukoloni kusafirishia mizigo yao, bado alikataa  kwa kumwandikia barua ofisa mtendaji wa kata na Tanesco wasimamishe mradi huo.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Idd Hulela, aliyezaliwa mwaka 1933 alisema barabara anayoitaka Dk. Rutengwe ni mali ya Serikali tangu enzi hizo.

Meneja Mradi  wa kiwanda hicho kutoka Kampuni ya Sayona, Aboubakary Mlawa, alisema ujenzi wa kiwanda umepitia hatua zote, mbali na barua hizo, Dk. Rutengwe amekuwa akimtumia ujumbe kwa njia ya simu ya kiganjani akimtaka asimamishe mradi huo.

Alisema kama kiwanda hicho kitakamilika kitaajiri Watanzania 800 hatua ambayo itasaidia kupunguza tatizo la ajira.

Kwa upande wake mwakilishi wa Dk. Rutengwe, Said Hemed, alisema  bosi wake  hataki tena fidia hiyo.

Alisema naye anataka mradi huo uendelee kufanyika  wananchi wapate maendeleo, lakini alitaka haki itendeke kwa wananchi waliopo kijijini hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles