Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
APRIL 7, mwaka huu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philipo Mpango aliwasilisha mapendekezo ya mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17 ambapo alisema katika kipindi hicho serikali imekusudia kutumia Sh trilioni 29.539.
Katika bajeti hiyo, Sh trilioni 17.798 zitatokana na mapato ya ndani ambapo kati ya hizo Sh trilioni 15.105 ni makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kati ya fedha hizo Sh. trilioni 2.693 zitatokana na mapato yasiyo ya kodi, wakati Sh bilioni 665.415 zitatokana na mapato ya halmashauri.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango Serikali inakusudia kupewa mikopo yenye masharti nafuu kutoka nchi wahisani zinazochangia bajeti ya Serikali (GBS) ya Sh trilioni 3.6.
Inakusudia pia kutumia Sh trilioni 7.475 kwa ajili ya mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara, Sh trilioni 5.374 zitatokana na mikopo ya ndani na Sh trilioni 2.100 zitatokana na mikopo ya nje (ENC).
MTANZANIA limezungumza na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi, wadau pamoja na wananchi kupata maoni yao juu ya mwelekeo huo wa bajeti ya serikali katika mwaka wa fedha 2016/17.
Profesa Ngowi
Mtaalamu wa uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, anasema hatua ya serikali kupanga bajeti hiyo kutegemea makusanyo ya ndani ni lengo zuri ila changamoto ipo kwenye namna ya kupata fedha hizo.
“Lengo ni zuri lakini namna ya kuzipata fedha hizo ndiyo changamoto iliyopo, ni suala la kulitazama kwa kina kwa sababu wananchi wanaolipa kodi ni wachache, wengi wanakwepa hivyo juhudi zaidi zinahitajika ili kufikia lengo,” anasema Profesa Ngowi.
Anasema wigo wa ukusanyaji wa kodi bado ni mwembamba na kwamba lazima vyanzo vya ukusanyaji wa mapato hayo visimamiwe kwa haki.
“Sehemu nyingi tunakusanya kwenye kodi ya majengo ingawa kuna changamoto kwamba wamiliki wengi licha ya kukusanya kodi ya pango huwa hawalipi kodi inavyopaswa. Lakini serikali isije ikaingia kwenye mtego rahisi wa kufikiria kuongeza viwango vya kodi na ndio maana nasema visimamiwe kwa haki na uwazi ,” anasema.
Profesa Moshi
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mtaalamu wa masuala ya uchumi, Profesa Humfrey Moshi, anasema mwelekeo huo wa bajeti ni wa matarajio na uliojaa matumaini ya kutekelezwa kwa vitendo.
“Natarajia utatekelezwa kwa vitendo tofauti na miaka ya nyuma ya serikali zilizopita, serikali hii inaonyesha kuwa imejipanga kutekeleza kwa vitendo zaidi,” anasema Profesa Moshi.
Anasema kwa muda mrefu amekuwa akiiomba serikali pamoja na wachumi wenzake kwamba iongeze bajeti ya maendeleo lakini walikuwa hawasikilizwi.
“Tofauti na awamu zilizopita, awamu hii ya tano imeongeza bajeti ya maendeleo hadi kufikia asilimia 40, kwa hiyo iwapo wataisimamia na kuitekeleza ni wazi kwamba Watanzania tutapata maendeleo tunayoyatarajia,” anasema.
Anasema ingawa serikali inalenga kupunguza utegemezi kutoka kwa wahisani lakini kwa sasa bado inahitaji wafadhili angalau kwa mwaka mmoja.
Hata hivyo anasema suala la kuongezeka kwa deni la Taifa si jambo jema na akashauri serikali itafute washauri wa nje mbali na wale wa benki wanazopanga kwenda kupata mikopo hiyo.
Anasema serikali inapaswa pia kuangalia upya matumizi yake na kuyaondoa yale yasiyo ya lazima ili izidi kuokoa fedha na kuzipeleka kwenye maendeleo.
“Tumeandaa mwelekeo wa bajeti ni sawa lakini linapokuja suala la utekelezaji wa bajeti hiyo huu ni ugonjwa unaotusumbua. Serikali ihakikishe fedha zinazoombwa na wizara zinakwenda kama zilivyoidhinishwa na Bunge,” anasema.
Profesa Temu
Naye Mhadhiri na mtaalamu wa masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Andrew Temu, anasema kwa kuwa viwanda ni kipaumbele katika serikali ya Dk. Magufuli, ni vema akaelekeza bajeti pia katika sekta ya kilimo ili kuhakisha viwanda vinapata malighafi za kutosha kuviwezesha vijiendesha kwa gharana nafuu na ufanisi.
“Naamini viwanda ni ushindani na vitahitaji malighafi mbalimbali ambazo nyingi zinatokana na kilimo, hivyo inabidi tukiboreshe kilimo chetu ili viwanda vipate malighafi za kutosha,” anasema Profesa Temu.
Wananchi
Simon Katunzi mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, anasema mwelekeo huo wa bajeti umeonesha nia ya serikali katika kupunguza utegemezi kwa kiwango kikubwa.
“Nashukuru kiwango cha kuwategemea wahisani kimepungua ingawa tunawahitaji katika baadhi ya mambo,” anasema Katunzi.
Naye mkazi wa Kisarawe mkoani Pwani, Sauda Karim, anasema mwelekeo huo wa bajeti unadhihirisha namna serikali ilivyojipanga kuwapatia wananchi wake maendeleo.
“Nimesikia wakisema kwamba wamepanga kujenga viwanda katika sehemu mbalimbali, hivyo nashauri mipango hii isije ikaishia kwenye makaratasi pekee,” anasema Sauda.
Miradi ya kipaumbele
Miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbe kwenye bajeti hiyo ni ule wa magadi soda katika Bonde la Engaruka, mkoani Arusha ambao umetengewa Sh milioni 700 ili kukamilisha tafiti za uchimbaji na upembuzi yakinifu.
Mradi huo ukikamilika serikali inatarajia kuingiza Sh bilioni 400 kwa mwaka.
Sh bilioni 2 za fedha za ndani zimetengwa kukarabati majengo na mitambo ya Kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha ili kukifufua, ambapo mradi huo utaendeshwa kwa ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na sekta binafsi.
Sh milioni 600 fedha za ndani zitatumika kuendeleza mradi wa kiwanda cha Viuadudu Kibaha mkoani Pwani ili kiweze kuzalisha wadudu hao kwa asilimia 100.
Sh bilioni 6 zitatumika kuendeleza Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) ili kuimarisha na kuendeleza maeneo ya viwanda hivyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Morogoro.
Sh bilioni 450.3 ya fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HLBS) ambapo serikali inakusudia kuwakopesha wanafunzi 270,000 watakaoomba mikopo hiyo, huku bodi hiyo ikitarajiwa kukusanya Sh bilioni 43.8 zitakazotumika kuwakopesha wanafunzi hao.
Sh bilioni 3.4 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi na Sh bilioni 2.5 zitakarabati na kupanua vyuo vya ualimu vya Kitangali, Ndala, Shinyanga na Mpuguzo.
Pia serikali imepanga kuboresha hospitali za rufaa ikiwemo ya Mkoa wa Mbeya ambayo imetengewa Sh bilioni 5, Mtwara Sh bilioni 2 na Kibong’oto Sh milioni 800 na hospitali nyinginezo.
Pamoja na mambo mengine, serikali inatarajia Pato la Taifa (GDP) kukua hadi asilimia 7.2 mwaka 2016/17 kutoka asilimia 7.0 kwa mwaka jana huku mkakati ukiwa ni kupunguza kasi ya mfumuko wa bei ili ufikie asilimia 6.0.