27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Nchi jirani zinavyotishia ustawi Bandari ya D’ Salaam

*Shehena ya mizigo yapungua kwa asilimia 50

 

Mwonekano wa Bandari ya Dar es SalaamNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MACHI 30, mwaka huu nilibahatiaka kuwa miongoni mwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ambao tulitembelea Bandari ya Dar es Salaam kujionea utendaji kazi wake.

Bandari ni moja ya sehemu yenye pilikapilika nyingi mno kutokana na kuwapo vitendo mbalimbali vya kuhudumia wateja.

Historia inaonyesha Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni kubwa kuliko zote nchini, inahudumia shehena za aina mbalimbali kutoka nchi zipatazo 10.

Nchi hizo ni Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda, Zimbabwe na Comoro. Lakini pia inahudumia kwa kiasi kikubwa  shehena ya Sudani Kusini.

Bandari ya Dar es Salaam ina gati 11 zenye uwezo wa kuhudumia tani 10.1 kwa mwaka ikijumuisha shehena ya kawaida tani milioni 3.1, maji tani 6.0 makontena 600,000 Bandari Kavu (ICDs).

ICDs zinatumika kuhudumia shehena ya makontena na kwa ujumla zinao uwezo wa tani milioni 1.0 kwa mwaka.

Akizungumza na ujumbe wa waandishi hao, Mkurugenzi wa Masoko wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Francisca Muindi, anasema kuna umuhimu wa kuwa na ongezeko la shehena kutoka nchi jirani.

Anasema ongezeko hilo husaidia kukuwa kwa pato la Taifa kutokana na Serikali kukusanya kodi kutoka kwenye biashara hizo.

Anasema ukuaji wa viwanda na huduma (multiplier effects) nyingine tofauti,kuongeza ushirikiano na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani

“Kupunguza gharama za usafirishaji kutokana na mzigo mkubwa, husaidia kupungua gharama kwa mlaji kwani huwa na bei bora katika ushindani kwenye masoko ya kimataifa,”anasema Muindi.

 

MIKAKATI YA KUVUTIA SHEHENA

Anasema kuna kila sababu ya kuboresha huduma za TPA kwa kutekeleza miradi mbalimbali na kwa wakati uliopangwa.

Anasema moja ya mkakati huo ni upanuzi wa bandari, kununua vitendea kazi vyenye uwezo mkubwa na vya kutosha na ujenzi wa bandari mpya,

“Kutekeleza “Customer Service Charter,” ikiwamo kutoa huduma za bandari kwa masaa 24 kwa siku saba kwa siki kwa kushirikiana na wadau wote muhimu ili kutoa mizigo kwa wakati…hakuna kitu ambacho wateja hupenda kama kutoa mizigo yao kwa wakati bandarini,” anasema Muindi.

Anasema mkakati mwingine ni kuimarisha ulinzi na usalama kwa ajili ya mizigo ya wateja, kutumia teknolojia ya ICT katika kutoa huduma. Mfano: “e-payment”

“Tunapaswa kuwa na wafanyakazi wenye elimu ya kutosha na ari ya kuhudumia wateja ipasavyo, kuzitangaza bandari za TPA kwa kushirikiana na wadau wote ili kutafuta biashara kwa kuwalenga wateja wa sasa, wapya na kuwarudisha wale walioacha kutumia bandari  zetu,”anasema Muindi.

Anasema moja ya mkakati mkubwa ambao TPA imeufanya ni kufungua ofisi nchi jirani ili kuwa karibu na wateja kwa lengo la kuwawezesha kupata taarifa sahihi.

Anasema wamefungua ofisi katika miji ya Lusaka  nchini Zambia na Lubumbashi  nchini DRC.

“Si hapo tu, TPA bado inafanya jitahada za kutosha ili kufungua ofisi mjini Kigali, Rwanda na nchi zingine ambazo zinatumia  Bandari ya Dar es Salaam…lengo letu tunataka kuhakikisha soko hili tunalikamata licha ya kuwapo na changamoto nyingi,”anasema.

 

CHANGAMOTO

Anasema kumekuwapo na ushindani mkali kutoka bandari za nchi jirani kama vile Mombasa (Kenya), Nacala/Beira (Msumbiji), Walvis Bay (Namibia), Durban (Afrika Kusini) na Lobito (Angola) , ambazo zinatishia biashara ya TPA.

“Ushindani wa shehena iliyopo ambao umejikita kwenye kanda (corridors) za usafirishaji wa mizigo za nchi jirani,Mombasa/Northern Corridor (Kenya), Lamu – LAPSSET) Corridor (Kenya), Nacala –Beira-Maputo Corridors (Msumbiji), Durban Corridor (Afrika Kusini), Walvis Bay/Trans Kalahari /Trans-Kaprivi Corridors (Namibia)…tunapaswa kujifunga mkanda ili kuhakikisha hawa wapinzani wetu tunapambana nao kila siku,”anasema.

Anasema ukosefu wa miundombinu inayohitajika katika kanda za kusimamia usafirishaji wa mizigo ya nchi jirani kunachangia huduma kurudi nyuma.

Anasema kwa mfano kwenye ukanda wa Kati, ukanda wa TAZARA (TAZARA Corridor), ukanda wa Tanga (Tanga Corridor) na ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor.

Anasema kanda hizi zikiimarishwa ni wazi TPA itapiga hatua kubwa za kuhudumia wateja wake bila wasiwasi.

“Naamini kanda hizi zikiwa imara tunaweza kukabiliana na wapinzani wetu wote ambao wanatuzunguka. Hapa ndiyo unaona umuhimu wa kuwapo na reli kama vile ukanda wa Tazara,”anasema Muindi.

 

 

SHEHENA

Kwa upande wake Kaimu Meneja Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, anasema idadi ya mizigo katika bandari hiyo imepungua tofauti na matarajio yao ambayo wamejiwekea.

Kwa mfano,anasema shehena ya magari yanayokwenda DRC imepungua licha ya nchi hiyo kutumia bandari yake.

nasema shehena ya magari yaliyopelekwa DRC Januari 2015 na Januari 2016, imepungua kwa asilimia 50.

“Ukiangalia kwa namna moja au nyingine, utaona ambavyo shehena imepungua kwa kasi kubwa,hapa tunapaswa kupambana zaidi.

“Hata shehena ya Zambia nayo imepungua kwa asilimia 46,”alisema.

Anasema wamefanya uchunguzi wa kina na kubaini sababu ya kupungua kwa shehena hiyo na kubaini kuwa sehemu ya shehena hiyo hasa iliyokuwa ikienda Zambia, DRC na Malawi, inashushwa katika Bandari ya Beira nchini Msumbiji ambao kwa siku za karibuni wameonekana kuwa washindani wakupwa wa TPA.

Anasema sababu za kushushwa katika Bandari ya Msumbiji, badala ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndiyo yenye unafuu wa umbali kutokana na jiografia yake,unatokana na shehena nyingi kusafirishwa kwa reli  kutoka  Bandari ya Beira hadi Malawi.

“Kwa kweli hapo ndiyo tunaona umuhimu wa kuwa na reli,wenzetu wamejiimairisha vizuri wakati sisi tunatumia zaidi barabara.

Anasema usafirishaji wa reli una unafuu mkubwa kwa sababu ni asilimia 30, ikilinganishwa na usafirishaji wa barabara.

Anasema Serikali ya Msumbiji tayari wameshakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa,ambayo wafanyabiashara wameona kuna unafuu wa kupitisha mizigo katika Bandari ya Beira kuliko ya Dar es Salaam,jambo ambao linahatarisha biashara yake.

“Kunaweza kuwa na athari katika Bandari ya Dar es Salaam,kama ujenzi wa reli ya kisasa inayoanzia Bandari ya Mombasa mpaka DRC ukikamilika,tunahofu kubwa itaongeza unafuu wa kusafirisha mizigo  kutoka Tanzania.

“Kama nilivyosema hapo juu ya umuhimu wa reli, leo dunia nzima bandari nyingi zimekuwa na mafanikio kwa sababu zinatumia mfumo wa reli za kisasa unaotoa mizigo bandarini hadi kwa mteja, jambo linalokosekana katika Bandari ya Dar es Salaam, nadhani umefika wakati mamlaka zinazohusika katika suala hili zichukuwe haraka, tunapenda kuona reli ya kati inafanya kazi,”anasema.

 

TISHO LA RAND

Anasema mshindani wao mwingine ni Bandari ya Durban ya Afrika Kusini ambayo nayo imeanza kuchukua shehena nyingine iliyokuwa ikipitia nchini.

Anasema sababu kubwa ya kupelekwa huko ni kutokana na unafuu uliotokana na matumizi ya fedha ya nchi hiyo, Rand, katika utozaji wa gharama za kutoa mizigo, tofauti na Tanzania ambako gharama hutozwa kwa Dola ya Marekani.

Anasema hivi sasa Rand imeshuka thamani, mfanyabiashara mwenye Dola ya Marekani anatumia Dola chache za Marekani kulipia tozo.

“Ukiangalia kwa makini gharama za utoaji mizigo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Durban zinalingana,mfanyabiashara akipitisha mzigo kule Afrika Kusini atatakiwa kubadilisha Dola ili apate Rand ya kulipa gharama zake, hili nalo tunapaswa kuliangalia kwa umakini,”anasema.

 

UTAMBUZI WA MIZIGO

Anasema wanakabiliwa na changamoto ya utambuzi wa shehena zilizoko katika meli, unaotumiwa kukadiria gharama za utoaji wa mizigo bandarini na kodi.

Anasema siku zote mzigo unapopakiwa katika nchi unakotoka,mpakiaji anapaswa kueleza aina ya mzigo katika fomu maalumu ya kutambulisha mzigo.

“Fomu hii hujazwa na mpakiaji ikifika Dar es Salaam kabla ya kupakua mzigo, hutumiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kukadiria kodi.

“Fomu hii ikikosewa kidogo tu na mpakiaji, TRA wakati wa kuhakiki mzigo huhisi harufu ya ukwepaji kodi, kitendo ambacho husababisha utaratibu wa utoaji mzigo husika huchukua muda mrefu,”anasema Mhanga.

Anasema fomu hiyo husababisha athari kubwa kwani mzigo husika huchajiwa adhabu ya kukaa bandarini kwa muda mrefu na kama ni wa nje ya nchi, mteja hulazimika kukaa Dar es Salaam kwa kosa lililofanywa na mpakiaji wa mizigo jambo ambalo hapendi kuona linatokea.

“Unajua mzigo unaporuhusiwa pale TRA, mteja wao hujui anapelekewa ujumbe gani nje ya nchi,kwanza unakuta ameingia gharama ya kuishi Dar es Salaam kwa muda mrefu, akifika bandarini na kukutana na adhabu ya kuhifadhi mzigo ambayo hakuisababisha hukereka sana, wengi hukasirika na hujui wanapeleka ujumbe gani kwa wateja wengine katika nchi zao,”anasema Mhanga.

Anasema 2011, mteja moja alitumia siku nne kusubiri mzigo wake utoke bandarini, lakini  hivi sasa mteja huyo huyo anasubiri siku mbili mpaka apate mzigo wake, jambo lililochangiwa na uboreshaji wa utaratibu wa kupata vibali vya nyaraka ambao unafanyika kwa mtandao tofauti na zamani.

Anasema hivi sasa wanakamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa 35, ambalo litakuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati, litakalohifadhi wadau wote wa bandari katika jengo moja, ili mteja akiingia katika jengo hilo, akitoka akatoe mzigo wake moja kwa moja.

Kwa sasa mteja anaweza kujikuta akihangaika na nyaraka zake kwa wadau mbalimbali wa Bandari ya Dar es Salaam kupata vibali, ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Idara ya Uhamiaji, Idara ya Afya, Mkemia Mkuu na wengine.

 

Itaendelea wiki ijayo.

 

0714 207 553

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles