NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SERIKALI imeagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji waliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini.
Wengine watakaohamishwa ni wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Kitengo cha Paspoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji, Dar es Salaam.
Uamuzi huo ulifikiwa jana baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kukutana na viongozi wa idara hiyo na wizara wakiwamo wakuu wa idara na vitengo vingine.
Waziri huyo aliagiza yafanywe mabadiliko makubwa katika vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika vitengo hivyo.
Aidha aliagiza pia wakuu wote wa vitengo vya upelelezi vya wilaya zilizopo Dar es Salaam na wale wa vituo vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine pamoja na watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika vituo hivyo.
“Huu ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na idara hii ambayo ni moja ya idara muhimu za Serikali.
“Katika kuisafisha idara hii uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lakini lengo kubwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wale wasiowajibika,” alisema Kitwanga.
Kwa mujibu wa Kitwanga utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, ambapo asilimia 20 ikiwa ni uongozi mbovu na asilimia 20 matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema asilimia 15 inahusisha vitendea kazi wa mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia 5 ukabila na upendeleo.
Waziri huyo aliwataka viongozi na watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi.