28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mabadiliko makubwa CCM

kikwete na magufuliNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajia kufanya mabadiliko makubwa ya ndani, huku wajumbe wengi wa Sekretariet wakitajwa kuwa huwenda wakapoteza nafasi zao, MTANZANIA limebaini.

Kutokana na hali hiyo hivi sasa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, yupo katika maandalizi ya kukabidhi mikoba ya chama hicho kwa Rais Dk. John Magufuli.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa Dk. Magufuli huwenda akakabidhiwa chama Juni mwaka huu, kwani hivi sasa viongozi wa juu wa CCM wapo katika maandalizi ya kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu unaotarajiwa kufanyika kati ya Mei na Juni mjini Dodoma.

Chama hicho kinatarajiwa kufanya uchaguzi wake wa ndani mwakani, kwa ajili ya kuchagua viongozi mbalimbali wa chama kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa.

Kitendo cha Kikwete kumwachia chama hicho Dk. Magufuli kabla ya mwaka wa uchaguzi ni utaratibu ambao chama hicho kimejiwekea kwa Rais kukabidhiwa chama mapema.

Hii imetokea kwa Rais wa awamu ya kwanza Hayati Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, ambapo walikabidhiana chama hicho kabla ya mwaka wa uchaguzi.

Hatua hiyo ya kukabidhiwa chama kwa Rais Magufuli inaelezwa ni moja ya mkakati wa kuimarisha ufanisi na utendaji wa serikali yake ya awamu ya tano  inayoongozwa chini ya falsafa ya Hapa Kazi Tu!

Taarifa hizo za uhakika zililiambia gazeti hili kwamba, Kikwete amekuwa na uhakika wa kasi ya Magufuli tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana.

Chanzo hicho kilisema kwamba mabadiliko hayo huwenda yakawaathiri baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu (NEC) na wengine kujikuta wakipoteza nafasi zao.

Katika safu hiyo mpya, aliyekuwa mgombea urais ndani ya CCM, Makangoro Nyerere anatajwa kuwa huwenda akawa Makamu Mwenyekiti (Bara), kuchukua nafasi ya Philip Mangula ambaye huwenda akarudishwa kuwa Katibu Mkuu wa chama.

“… pia wapo kama Nape ambaye kwa sasa ni waziri katika Serikali ya Rais Magufuli lakini kwenye chama ndiyo mwenezi, kwa utaratibu wa sasa mtu akiwa serikalini kwenye chama lazima atoke wewe ni shahidi haya yamefanyika.

“Lakini pia kuna nafasi finyu ya kurudi kwa Katibu wa Oganizesheni Dk. Muhamad Seif Khatib, pamoja na sababu nyingine lakini sababu kubwa ni kutokana na umri wake,” kilisema chanzo hicho kutoka Kamati Kuu (CC).

Licha ya Mangula kudaiwa kuchukua nafasi ya ukatibu mkuu, lakini inadaiwa kuwa Rais Magufuli bado anamuhitaji Katibu Mkuu wa sasa Abdulrahman Kinana, aendelee na nafasi hiyo, ingawa kiongozi huyo anadiwa kuendeleza msimamo wake wa kutaka kupumzika.

“Zipo juhudi kubwa zinafanywa pia za kubembeza mzee Kinana ili aendelee na ukatibu mkuu wa chama na ukumbuke hata Rais Kikwete, alifanya kazi kubwa sana ya kumwomba kwa wakati ule aivushe CCM 2015 na alikubali kwa shida sana na sasa sisi kama wana CCM tunajivunia uwepo wake na kila mmoja anajua kazi kubwa aliyoifanya.

“Ilifika mahali wana CCM walikuwa wakiogopa hata kuvaa sare za chama lakini Kinana alisimama kupitia ziara zake mikoani na hatimaye kila Mtanzania na mwana CCM ni shahidi sasa kama ataendelea na msimamo wake kuna kila dalili za Mangula kurejea kwenye ukatibu mkuu wa chama,” alisema.

Kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za CCM mwenyekiti wa chama ndiye mwenye mamlaka ya kuunda Sekreterieti, ambapo kutokana na hali hiyo, Rais mstaafu Kikwete alifanya hivyo.

Wajumbe wa Sekreterieti ni Abdulrahman Kinana (Katibu Mkuu), Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti), Dk. Ali Mohamed Shein (Makamu Mwenyekiti Zanzibar), Rajab Luhavi (Naibu Katibu Mkuu Bara), Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar).

Wengine ni  Dk. Asha-Rose Migiro( Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa), Zakhia Meghji (Uchumi na Fedha), Nape Nnauye (Itikadi na Uenezi) na Muhamad Seif Khatib (Oganaizesheni).

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa kutokana na mabadiliko na harakati za makabidhiano ya chama, Rais mstaafu Kikwete juzi alikwenda Ikulu jijini Dar es Salaam na kukutana na Rais Magufuli, huku ikielezwa kuwa moja ya ajenda ya mazungumzo yao ilikuwa ni maandalizi ya mkutano mkuu maalumu wa CCM.

Kauli ya CCM

MTANZANIA ilipomtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuzungumzia suala hilo, alisema hakuna taarifa za kufanyika kwa mkutano huo.

“Siwezi kusema lolote katika hilo kwani kungekuwa na mkutano huo tungeweka kwenye ratiba za chama … kama mwandishi siko tayari kuulizwa swali nitoe maelezo yatakayotoa tarehe maalumu ya mkutano mkuu,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles