22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 29, 2022

LUKUVI APIGA ‘STOP’ NYUMBA KUWEKEWA X  • Ni zile ambazo hazijarasimishwa, aanika janja ya kampuni zinazopima kiwanja kwa maelfu ya fedha
  • Mpango wa kuifumua Dar nao waiva

Na Waandishi Wetu

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amepiga marufuku uwekaji wa alama ya ‘X’ kwenye makazi ya wananchi waliojenga katika maeneo ambayo hayajarasimishwa kote nchini.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa wadau wa ardhi waliokutana kujadili mpango mji wa miaka 20 wa Jiji la Dar es Salaam.

Alisisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba yake kwa sababu amejenga katika eneo ambalo halijarasimishwa, kwa sababu Serikali imewapa fursa ya kurasimisha maeneo hayo.

Pia alizipiga marufuku kampuni zinazojihusisha na urasimishaji wa maeneo kuwachangisha fedha wananchi kutokana na kubaini kuwapo kwa kasoro kadhaa wakati wa zoezi hilo maeneo ya jijini Dar es Salaam.

“Zoezi hili tulilianza tukaona lina kasoro, Dar es Salaam kuna watu walianza kutoza wananchi Sh 500,000 hadi Sh 400,000 ili kupima kiwanja kimoja cha maskini aliyejenga kwenye eneo lisilo rasmi.

“Lakini baada ya kuchunguza nimegundua gharama halisi hazizidi Sh 250,000, kwa hiyo nimetoa agizo kwamba katika urasmishaji wowote hapa Tanzania, mwananchi asichangie zaidi ya Sh 250,000 ili kupimiwa kiwanja chake hiyo ni gharama ya juu.

“Kampuni hizi zishindane kwa sababu tenda zitatangazwa na wilaya ili kila mtu anayetaka kupata kazi lazima atoe bei isiyozidi Sh 250,000 na iwe marufuku kwa kampuni kuchangisha fedha za wananchi katika sehemu ambayo inarasimishwa.

“Dar es Salaam yako makampuni matatu yamechukua fedha, wananchi wamechangisha kwenye akaunti zao na wametoroka hawakufanya kazi, hawa tunawakamata.

Alisema wakati wa urasimishaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali wananchi wenyewe watafungua akaunti zao za mitaa ambazo watazisimamia.

Aliwaonya viongozi wa mitaa kujihusisha na fedha hizo na kwamba, malipo yatafanyika baada ya kazi hiyo kuthibitishwa na maofisa wa wilaya.

Alisema gharama zitakazotumika kurasimisha zitakapokubaliwa ndipo wananchi watatoa fedha kuzilipa kampuni zitakazopewa kazi hiyo.

“Najua watendaji na wapimaji wa Serikali ni wachache, ndiyo maana tumeweza kusajili kampuni nyingi za upimaji, kwa hiyo ni marufuku kwa kampuni binafsi kwenda kuomba kazi huko mitaani, lazima waanzie wilayani na isimamiwe na wilaya. Na iwe kiungo kati ya wale warasimishwaji na warasmishaji.

“Narudia, ni marufuku kwa kampuni kuchukua fedha za wananchi na kuingiza kwenye akaunti zao. Lakini iwe tena ni marufuku kwa madiwani na wenyeviti wa mitaa kwa sababu baadhi yao wamekuwa wanachukua fedha kwa makampuni wakidanganya kuwa wao ndio wanatoa kazi za urasimishaji na upimaji.

“Matokeo yake wanataka kuhongwa fedha na gharama hizo zinaingia kwenye gharama za watu wanaotaka kurasimishiwa. Kazi hazitatolewa na mwenyekiti wa mtaa wala diwani, zitatolewa wilayani kwa hiyo kampuni zisiende kwenye mitaa kuhonga madiwani au wenyeviti wa mitaa ili wapate kazi ya urasimishaji,” alisema.

Waziri Lukuvi aliwataka watendaji wote wa ardhi wa wilaya zote nchini kuhakikisha wanasimamia zoezi la urasimishwaji na uhamasishaji na kwamba, migogoro yoyote itakayotokea watawajibika.

“Isitokee mtu tena akaweka X kwenye nyumba za wananchi kama ilivyojitokeza Babati jana (juzi), katika maeneo ambayo watu wamejenga kiholela isipokuwa kwa watu waliojenga kwenye maeneo yaliyo kwenye hifadhi zilizopo kwa mujibu wa sheria, kama vile hifadhi ya barabara, hifadhi ya misitu iliyosajiliwa au iliyotangazwa kwenye gazeti la Serikali,” alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi alizitaka wilaya zote kuhakikisha zinaainisha maeneo yote ambayo hayajarasimishwa ili kupanga utaratibu wa zoezi hilo ili wananchi wapate barabara, hati miliki za maeneo hayo kulingana na nyumba walizozijenga.

“Barabara watazipata kwa kukubaliana wenyewe ni nani achangie ardhi yake ili barabara iweze kupita na kila mwananchi atachanga fedha kuhakikisha nyumba yake inapimwa kwa gharama zake,” alisema Lukuvi.

MPANGO MIJI

Wakati huo huo, Lukuvi amezungumzia maendeleo ya Mpango mji mpya wa Jiji la Dar es Salaam (Dar Master Plan), ambao unatarajiwa kukamilika mwaka huu na kuondoa kero mbalimbali kama makazi holela na mafuriko akisema pamoja na mambo mengine, utaongeza upatikanaji wa maeneo ili kuendana na ongezeko la idadi ya watu ambao sasa wanazidi milioni sita.

Alisema mpango huo utawezesha wananchi kupata hatimiliki ya ardhi juu ya nyumba (ghorofani) na kuwa na haki sawa kama mmiliki wa kiwanja.

Pia alisema chini ya mpango huo wananchi wenyewe ndio watakaopanga matumizi ya ardhi yao.

“Aidha, licha ya kupangwa kwa matumizi mapya ya ardhi, hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba yake badala yake mtu yeyote atakayetaka kuendeleza maeneo ya wananchi atatakiwa kukubaliana nao na kuwalipa fidia ili wahame.

“Hatua ya mwisho ya uidhinishaji wa mpango mkuu wowote kwa mujibu wa sheria ya mipango miji ya mwaka 2007, inataka wadau wakutane waupitie,” alisema.

Alisema baada ya mpango huo kuidhinishwa utapelekwa kwa wananchi kupitia kata mbalimbali na kwenye vikao vya madiwani kisha Waziri wa Ardhi atautangaza.

Mbali na kuboresha mandhari ya jiji kwa kuwa na vimiji vidogo vidogo, hali kadhalika maeneo yaliyopangiliwa kama masoko madogo madogo, mpango huo pia utaondoa shaka na kutengeneza maisha mapya tofauti na ya sasa.

Alisema baada ya kukamilika kwa mpango mji huo, Manispaa hazitatoa vibali vya ujenzi kinyume cha mapendekezo ya mpango uliowekwa.

“Kama una nyumba Manzese lakini imebomoka utatakiwa sasa uambiwe na watu na Manispaa kuwa ukajenge kitu gani, kwani ‘master plan’ ya hapo Manzese zamani watu walikuwa wakijenga nyumba bila kufuata taratibu.

MEYA MWITA

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya  Mwita, alisema mpango huo umekuja wakati mwafaka kutokana na ongezeko kubwa la watu katika jiji hilo.

“Kuna mambo machache ambayo wataalamu wetu wametueleza yanatakiwa yatiliwe mkazo, ambapo kuanzia Agosti wataanza kupita kata hadi kata kuupeleka mpango huu kwa wananchi ili watu waweze kutoa maoni yao.

Ombi langu kubwa ni kwamba, madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa watoe ushirikiano ili angalau wananchi waweze kutoa maoni yao.

“Tunataka tusikie kuwa wananchi wetu waseme ‘open space’ (eneo la wazi) yao itakua hapa na nini kifanyike katika kata zao.

Tusipowapa nafasi ya kusema tutakuwa na changamoto kubwa, kutokuwa waoga  wa kufikiri kuwa ‘master plan’ inakuja kubomoa nyumba zao, la hasha, si hivyo, ‘master plan’ hii itachukua zaidi ya miaka 20 katika utekelezaji wake.

“Sehemu kama vile Ilala kutaelekezwa kujengwa ghorofa mbili au moja, kwa hiyo ‘master plan’ inaelekeza kuwa katika eneo moja inatakiwa kukidhi viwango na vigezo vya masharti ya Serikali za mtaa na halmashauri zetu tuliyojiwekea,” alisema Meya Mwita.

Habari hii imeandaliwa na Leonard Mang’oha, Ferdnanda Mbamila na Meza Fride (SJMC)

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Habari ya leo..jamani naomba Waziri,diwani na wote viongozi wahusikao na hili.Watilie mkazo Chanika mtaa wa buyuni kuna matatizo mengi mengi ya ardhi.watu wameuziwa maeneo ya barabara na wentlyeviti wa mtaa walipitisha.haswa hawa wenyeviti wa mitaa na wajumbe wafuatiliwe wanakula pesa za watu.Naomba mkipita itangazwe kwa taarifa ya habari watu tuwepo kutoa maoni.tumelizwa sana.Asante

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,204FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles