Kina  Bobi Wine watapata taabu sana kumng’oa Rais Museveni

0
690
Rais Yoweri Museveni

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

MIAKA yake 32 madarakani bila kuonesha dalili za kustaafu karibuni kunaashiria mengi ikiwamo kiasi gani Rais Yoweri Museveni ameweza kuliweka kiganjani taifa lake hilo, ambalo ambalo awali tangu uhuru kabla ya ujio wake mwaka 1986 lilikosa utulivu.

Chini yake ameweza kutengeneza historia, ambayo hapana shaka iwapo atajipanga na kuondoka kwa amani na heshima taifa hilo litakuja mkumbuka kwa vizazi vingi vijavyo bila kujali upande wake wa pili wa shilingi usiofurahisha.

Bila kujali upande huo wa pili, Museveni amejijengea sifa kitaifa na kimataifa kwa kulitoa shimoni taifa hilo lililokuwa limekosa utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kutokana na tawala mbovu na udikteta wenye ukatili wa kutisha.

Chini yake kumeshuhudia amani na utulivu, ustawi wa kiuchumi na kijamii na pamoja na maendeleo ya miundombinu na kulifanya taifa hilo kuwa katika mstari sahihi wa kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa angalau kwa viwango vya mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hata hivyo, upande wake hasi unaohusisha kubakia kwake madarakani kwa miongo zaidi ya mitatu umefanikishwa na mbinu mbalimbali ikiwamo usaidizi wa jeshi kama ilivyo kwa watawala wengi wa Kiafrika wanaopenda kutawala maisha.

Mbali ya hivyo, amehakikisha wote wanaoibuka iwe ndani au nje ya vuguvugu lake la kisiasa linalotawala tangu mwaka 1986 la National Resistance Movement (NRM) wanazimwa wasifurukute kisiasa. Na mikakati hiyo ikihusisha pia mafanikio aliyoleta nchini humo ilimfanya awe akishinda kirahisi chaguzi mbalimbali tangu aruhusu mfumo wa vyama vingi katika miaka ya 1990.

Lakini mwelekeo wa hivi karibuni unaoshuhudia wimbi jipya la shauku hasa miongoni mwa wapiga kura vijana wakiongozwa na wanasiasa vijana wa kariba ya Bobi Wine linatishia uhai wake madarakani.

Upepo huo mpya uliochagizwa na mwanamuziki huyo aliyegeukia siasa, Mbunge wa Kyadondo Mashariki, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, zimekuwa mwiba mchungu kwa Museveni kiasi cha kuelekea kupoteza umaarufu.

Mwelekeo huo unokaribishwa kwa mikono miwili na wapiga kura wengi wa kada hiyo, unamaanisha iwapo haki itatendeka, utawala usio na dalili ya ukomo huenda ukahitimishwa katika miaka ya karibuni.

Nafasi yake itachukuliwa na utawala wenye damu changa kupitia mgombea yeyote wa upinzani watakayeungana kupitia kundi hilo la vijana.

Hata hivyo, ni wazi kutokana na namna Museveni alivyojiimarisha hasa jeshini haitakuwa rahisi kumng’oa kutoka madarakani, kwamba mazingira hayo ya kijeshi serikalini, ambayo Museveni ameyaweka yana uwezekano wa kuja kuwa kikwazo kwa Rais atakayechaguliwa kidemokrasia.

Mifano ya yaliyotokea katika mataifa, ambayo jeshi limehodhi sana siasa na uchumi kama vile Misri na Zimbabwe inaweza kuakisi taswira ya baadaye ya Uganda pale Museveni atakapong’oka au kuelekea kungo’ka kwa namna yoyote ile.

Tangu wakati wa Rais wa kwanza Mohamed Naguib hadi sasa chini ya Rais wa sita wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, wananchi wa Misri ni mara moja tu walichagua rais waliyemtaka, ambaye hata hivyo hakudumu madarakani. Watawala wote waliodumu walitokea na kuwekwa na Jeshi.

Jenerali Naguib aliingia madarakani kwa msaada wa Luteni Kanali, Gamal Abdel Nasser aliyeongoza harakati zilizoupindua utawala wa kifalme uliohitimisha kizazi cha Muhammad Ali na utawala wa Uingereza nchini Misri na Sudan mwaka 1952.

Kanali Nasser kwa kuona kuwa cheo chake ni kidogo akaamua kumwachia urais bosi wake Naguib. Hata hivyo ni Nasser aliyeonekana kuwa na nguvu katika utawala huo, akiunda chama cha siasa kilichojaza wanajeshi.

Haikuwa ajabu Naguib kulazimika kujiuzulu urais Novemba 1954 baada ya kutofautiana na Nasser ikiwamo kuliunga kwake mkono kundi la Muslim Brotherhood, ambalo mmoja wa wanachama wake alijaribu kumuua Nasser.

Miaka miwili baadaye Nasser akajitangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Misri 1956 hadi kifo chake kilichotokana na shambulio la moyo mwaka 1970.

Mmoja wa maofisa walioshiriki Mapinduzi ya mwaka 1952, Makamu wa Rais na msiri wa Nasser, Anwar Sadat akamrithi na kulitawala taifa hilo hadi alipouawa mwaka 1980.  Nafasi yake ikachukuliwa na Jenerali Hosni Mubarak aliyetawala taifa hilo kwa mkono wa chuma kwa miaka 30.

Hata hivyo, upepo wa mabadiliko ulipovuma katika mataifa ya Kiarabu yakiwamo ya Kaskazini mwa Afrika, matukio ya miaka ya 2011-2013 nchini Misri ni ushahidi mzuri wa kinachotokea kwa tawala za kiraia zinazojaribu kutoa changamoto kwa tawala za kisiasa za kijeshi.

Mwaka 2011, Jeshi la Misri liliuruhusu umma kumpindua mshirika wao wa miaka mingi, Rais Hosni Mubarak katika mazingira ambayo yalisifiwa sana si tu nchini humo bali pia na jumuiya ya kimataifa.

Lakini kile ambacho wengi nchini humo na jumuiya ya kimataifa haikukijua ni kuwa Jeshi lilikuwa limemchoka Mubaraka hasa likichukizwa na harakati zake za kutaka kuwarithisha watoto wake urais wakiwahesabu kuwa tishio kwao.

Hivyo, basi jeshi likamruhusu Mohamed Morsi kuchukua urais na kuunda serikali baada ya kushinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia usio na kibali kisicho na shaka cha jeshi.

Lakini lilimruhusu Morsi awatawale kwa mwaka mmoja tu, likiwa limefunga milango na juhudi zozote za kundi la kisiasa la rais huyo, Muslim Brotherhood kuibuka ukizingatia lilipigwa marufuku na Mubarak. likalivunjilia mbali.

Kwa vile  Morsi hakuwa chaguo la jeshi bali wananchi, hivyo basi haikuwa ajabu kutodumu kwani aling’olewa na Mkuu wa Majeshi, Abdel Fattah el-Sisi ambaye ndiye rais hadi sasa.

Kwa maana hiyo, Jeshi la Misri limewachagulia Wamisri viongozi tangu zama za kina Gamal Abdel Nasser, Sadat Anwar, Hosni Mubarak na sasa el-Sisi, wote wakitokea jeshini.

Ni hali ambayo imeonekana katika Taifa la Zimbabwe. Ikipata uhuru wake mwaka 1980, Zimbabwe iliongozwa na Rais Canaan Banana, lakini mamlaka yalionekana zaidi mikononi mwa Robert Mugabe aliyekuwa Waziri Mkuu, mtu wa jeshini.

Kwa msaada wa jeshi, Mugabe akaja kuitawala  Zimbabwe kwa zaidi ya miaka 30 hadi Novemba mwaka jana.

Akiwa na umri wa miaka 94, alipinduliwa na jeshi alilolichukiza kwa kitendo chake cha kuruhusu kizazi cha vijana wadogo wasiojua chochote kuhusu harakati za uhuru wa Zimbabwe wakiongozwa na mkewe Grace Mugabe kuiendesha nchi watakavyo.

Grace akionesha na hata kueleza wazi nia yake ya kutaka madaraka ya mumewe, alimshinikiza na kufanikisha kufukuzwa kwa wale wote walioonesha tishio kwa ndoto yake za kutaka kiti cha Mugabe.

Orodha ni ndefu lakini wa karibuni alikuwa makamu wa Rais na mpigania uhuru na mshirika wa Mugabe, Emmerson Mnangagwa, ambaye aliendeleza ukaribu wake na jeshi.

Likiona namna maslahi yao yanavyojaribiwa, Jeshi likiongozwa na Jenerali Costantino Chiwenga likampindua Mugabe Novemba mwaka jana na kumkabidhi nchi mtu wao Mnangagwa.

Hata hivyo, kama, ambavyo Jeshi la Misri lilijitahidi kuendelea kumstahi mkongwe Mubarak achilia mbali mashtaka dhidi yake, ndivyo la Zimbabwe linavyofanya kwa Mugabe, ingawa mwenyewe ameishia kulalamika.

Chiwenga akateuliwa na Mnangagwa kuwa makamu wa rais na mtihani wao wa kubaki madarakani ukajaribiwa Julai 30, mwaka huu katika uchaguzi wa rais na wabunge.

Ni uchaguzi wa kwanza bila Mugabe, ambao ulifuatiliwa sana na dunia hasa kuangalia iwapo Mnangagwa angetimiza ahadi yake ya chaguzi huru na haki tofauti na zile za mtangulizi wake.

Licha ya kampeni za amani pamoja na upigaji kura usiohusisha vurugu kulinganisha na wakati wa Mugabe, dosari zilijitokeza wakati wa mchakato wa utangazaji matokeo.

Matokeo yalionesha ushindani mkali baina ya Mnangagwa na kiongozi wa upinzani wa MDC Alliance, Nelson Chamisa na pale Tume ya Uchaguzi ilipochelewa kutangaza matokeo ya urais kwa sababu zisizo na msingi, ikifanya tu kwa yale ya ubunge, wafuasi wa mwanasiasa huyo kijana kipenzi kipya cha wengi wakaingiwa na hisia kuwa kura zao zinaibwa.

Hali hiyo ikasababisha maandamano na machafuko yaliyoua watu kadhaa baada ya jeshi kuingilia kati likitumia nguvu nyingi kiasi cha kumshangaza Mnangagwa mwenyewe, aliyekaririwa akisema haelewi  nani aliyetoa amri kwa jeshi kuingilia kati ilhali kulikuwa na askari wa kutuliza ghasia.

Mnangagwa aliyeshinda uchaguzi huo na ambaye amekuwa akijaribu kujenga taswira mpya ili kuvutia wawekezaji pamoja na kuondolewa vikwazo na Magharibi, ameshateua tume inayojumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo Tanzania kuchunguza ghasia hizo.

Nguvu zilizotumika na matumizi ya jeshi badala ya askari polisi zimeashiria namna watawala wa kijeshi wasivyo tayari kuachia madaraka kirahisi kwa tawala za kiraia wanazohisi zitaondoa maslahi waliyoyafurahia kwa miaka mingi.

Kwa mifano ya Misri na Zimbabwe inaonesha namna majeshi yanavyopenyeza watu hadi serikalini na kutoa uwezekano mdogo wa kutokea mtawala wa kiraia asiye na chembe na jeshi.

Rais Yoweri Museveni pamoja na madhaifu aliyonayo, ameweza kujiimarisha madarakani kwa namna inayompa udhibiti usio na kikomo na uaminifu usio na shaka, ambao wapinzani wake kama vile Bobi Wine watapata taabu sana kuuvunja.

Hivyo basi, moja ya changamoto kuu, ambazo mwanasiasa yeyote anayenyemelea kiti cha Rais Museveni ni uwapo wa jeshi, ambalo halitakubali kirahisi kumwachia yeyote asiye na damu ya jeshi madarakani.

Kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Rais Museveni ameweza kuigeuza serikali yake kuwa ya kijeshi akitoa nafasi za serikalini na bungeni kwa maofisa wa jeshi.

Mwaka 2005 alianzisha Sheria ya Jeshi la Ulinzi la Watu wa Uganda  ikitoa madaraka makubwa kwa jeshi. Moja ya vifungu vya sheria hiyo ni nafasi kwa maofisa 10 waandamizi wa jeshi kuchaguliwa kuingia bungeni wakitokea Baraza la kijeshi baada ya kuteuliwa awali na Museveni mwenyewe.

Mbali ya matatizo ya wazi ya jeshi kuwa na usemi bungeni, uwapo wake humo pia umesababisha mwingilio wa moja kwa moja bungeni kuwapa vipigo wabunge wa upinzani au wanaoonekana viherehere.

Kitendo hicho kimesababisha jeshi kuwashtaki raia katika mahakama za kijeshi. Bobi Wine mwenyewe alifikishwa katika mahakama ya kijeshi Agosti mwaka huu kwa mashtaka ya kumiliki silaha bila kibali.

Jeshi pia lina nguvu na ushawishi ndani ya baraza la mawaziri huku Jenerali Kahinda Otafire akisimamia Wizara ya Mambo ya Ndani na Jenerali Elly Tumwine akiongoza Wizara ya Usalama.

Museveni ameenda mbali zaidi ya Misri na Zimbabwe, amehakikisha ni yeye mwenye nguvu na sauti jeshini na kwa sababu hiyo amepenyeza watu walio karibu naye jeshini akiwashughulikia wale wanaoonesha dalili ya uasi dhidi yake au familia yake kama ilivyomtokea Jenerali David Sejusa aliyehoji mwelekeo wa kumrithisha mwana wa Museveni urais.

Kaka wa Museveni Salim Salehe ni jenerali mstaafu aliyekuwa akidhibiti “Operesheni ya Kutengeneza Utajiri’, mradi wa kiuchumi na kijamii wenye bajeti kubwa serikalini. Kwa sasa ni mfanyabiashara mkubwa aliye mmoja wa matajiri wakubwa nchini humo.

Mwanae Museveni Muhoozi Kainerugaba, pia ni jenerali wa ngazi ya juu aliyewahi kuongoza kikosi cha walinzi wa rais, mshauri wa usalama wa rais na kadhalika. Licha ya kuwapo taarifa za kumshusha cheo mwanae huyo, minong’ono ya miaka mingi imeendelea kusalia kuwa anamwandaa mwanae huyo mzaliwa wa Dar es Salaam kumrithi.

Ukosefu wa utenganisho wa jeshi, watu washikao bunduki na serikali ya kiraia una uwezekano wa kukwamisha ndoto za kina Bobi Wine kujaribu kumng’oa Museveni.

Hata wakifanikiwa kupata wingi wa kura na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, wapinzani watapata taabu sana kumuangusha rais anayeungwa mkono na jeshi.

Na hata iwapo wapinzani watafanikiwa, majenerali watabakia na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha fursa ya kisiasa na kiuchumi wanayofurahia kwa miaka mingi haziondoki.

Hivyo, wana uwezekano wa kuhujumu juhudi za kuleta mageuzi makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yataondoa stahili wanazofurahia maofisa hao wa jeshi kama ambavyo inashuhudiwa Misri na Zimbabwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here