Na Editha Karlo
JESHI la Polisi mkoani Kigoma limewauwa watu watatu wanaosadikika kuwa ni
majambazi na kukamata risasi 42.
Inaelezwa
majambazi hao walikuwa wamejipanga
kufanya uporaji katika baadhi ya nyumba za wananchi wilayani Kibondo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Louis Bura, alisema
juzi usiku polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna majambazi walikuwa wanataka kuvamia
baadhi ya nyumba.
Alisema
walifika eneo la tukio na kurushiana risasi ambako askari mmoja,
James Mwita (37) na mama mmoja, Sophia
Dicksoni (60) walijeruhiwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kibondo.
Alisema askari huyo alipatiwa matibabu ya awali na sasa amepatiwa rufaa kwenda
kwenye matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha ya mguuni.
DC aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa vyombo
vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanay ifanya kwa kuwa ni kazi ngumu.
“Ujambazi unaotokea ni ujambazi unaoshirikiana na wananchi waliopo hapa wikayani
kwetu.
“Naomba
kutoa rai kwa wote wanaojihusisha na matukio haya kuacha mara moja kwa
kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na matukio
hayo,” alisema DC.
Amewataka wananchi kuacha kuwaingilia katika utendaji kazi wao kwa kuwa wapo
baadhi wanawakamata wakiwatuhumu kwa ujambazi lakini ndugu zao wanawatetea na
kudai siyo majambanzi.
“Niwaambie tu wananchi hatutavumilia kuona majambazi wanaendelea kututesa
Kibondo tumechoka.
“Kuanzia
sasa niwaombe wananchi wale wanaoshirikiana na raia wa Burundi kuvamia watu muache
maana jambazi hawezi kuja bila kupewa taarifa na watu ambao wanafahamu ni nani
ana fedha, ” alisema Bura.
Aliwataka wananchi kuacha kutoka nje wanaposikia milio ya risasi kwa ajili ya
usalama wao kwa kuwa ni hatari kufuata milio hiyo inaweza sababisha madhara
makubwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, Sebasitiani Pima, alisema walipokea watu watatu wakiwa wamefariki dunia na majeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.
Alisema mmoja wa majeruhi amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.