NA HADIJA OMARY -Lindi
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zito Kabwe, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungala (Bwege) na mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Lindi, Isihaka Mchinjita, wamakamatwa na polisi kwa madai ya kufanya maandamano bila kuwa na kibali.
Katika tukio hilo, viongozi wengine watano wa chama hicho walikamatwa na polisi wilayani Kilwa kwa madai hayo ya kufanya maandamano yasiyo na kibali.
Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi, Abbas Said Mng’wachi, alisema tukio hilo lilitokea jana saa sita na nusu mchana ukumbi wa mkutano wa Darajani.
Alisema kikao kilichokuwa kifanyike jana kilikuwa na ajenda ya kuwapokea madiwani na viongozi mbalimbali wa Chama cha Wananchi (CUF) waliotaka kuhamia ACT Wazalendo.
Mng’wachi aliwataja viongozi wengine waliokamatwa kuwa ni pamoja na Katibu wa Oganaizesheni ACT Taifa, Shabani Mketo, Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT Wilaya ya Kilwa, Mahadhi Mahadhi na Akida Namwanja ambaye ni mlinzi wa Zitto.
Alisema viongozi hao walikamatwa wakati vikundi mbalimbali vya kwaya vikiimba ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa kikao hicho.
Mng’wechi alisema wameelezwa kuwa dhamana ipo wazi kwa viongozi hao, hivyo jana walikuwa wakishughulikia kuwatoa.
MTANZANIA ilipomtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christoph Ngubiagai, alisema viongozi hao walikamatwa kwa sababu ya maandamano yasiyo na kibali.
Alisema viongozi hao pamoja na wafuasi wao walikuwa katika maandamano wakitokea maeneo ya bandarini kuelekea eneo ambalo kiongozi huyo alikamatiwa.